Korti yawaachia 14, wakaa rumande siku 642 bila kesi kuendelea

Washtakiwa wakiwa ndani ya mahakama ya wazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuachiwa huru. Picha na Pamela Chilongola

Muktasari:

  • Akisoma uamuzi huo, Hakimu Mkazi Mkuu Ramadhani Rugemarila alisema mahakama hiyo imesikiliza maombi ya upande wa mashtaka na utetezi ambapo February 22, 2022 washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao upya na kusomewa maelezo ya awali baada ya kuachiwa na kufunguliwa tena shauri hilo.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru watu 14 baada ya kukaa mahabusu kwa siku 642 wakikabiliwa na mashtaka manne likiwemo la unyang’anyi wa kutumia silaha na wizi wa vinywaji vyenye thamani ya Sh408 milioni.

Pia mahakama hiyo imetoa amri vielelezo vyote vilivyotolewa kwenye kesi hiyo virudishwe kwa wenyewe.

Washtakiwa hao walioachiwa huru ni Severin Mkumi, Erick Rwehumbizi, Engeleberth Chiwalo, Salma Mohamed, na Veronica Ismail. Wengine ni Mohamed Mhidini, Elisha Sayota, Abas Ramadhani na Deo Simon, Victor Mchami, Laurian Swai, Daniel Ucheng, Leonce Sarawat na Arthur Moshiro.

Akisoma uamuzi huo, Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemarila alisema mahakama hiyo imesikiliza maombi ya upande wa mashtaka na utetezi ambapo February 22, 2022 washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao upya na kusomewa maelezo ya awali baada ya kuachiwa na kufunguliwa tena shauri hilo.

Rugemarila alisema kuanzia tarehe hiyo kesi hiyo imekuwa inaahirishwa mara kwa mara kutokana na upande wa mashtaka kutoleta mashahidi.

"Kesi hii ilisomwa kwa mara ya kwanza Agosti 12, 2021 mbele ya Hakimu Joseph Luambano lakini  aliiondoa kwa kifungu cha 225 cha mwenendo wa makosa ya jinai na washtakiwa walioachiwa na kukamatwa tena ambapo walisomewa upya makosa yao na maelezo ya awali  Februari 22,2022," alisema na kuongeza.

"Shauri hili tangu Februari 22,2022 lilipofunguliwa mbele yangu washtakiwa wameshakaa mahabusu siku 462 na tukianzia Agosti 12,2021 kesi ilipokuwa kwa Hakimu Luambano hadi kuamishiwa kwangu washtakiwa wamekaa mahabusu  siku 642 hadi leo hii," alisema Rugemarila.

Rugemarila alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kulazimisha upande wa Jamhuri ifunge ushahidi wake lakini ina uwezo wa kufuta kesi pale inapoona upande wa mashtaka hauiendeshi kesi kama inavyotakiwa.

Alisema kesi hiyo ilikuwa na mashahidi wawili walifika katika mahakama hiyo na walionywa ili wafike bila ya kukosa lakini walikaidi.

Hata hivyo muhanga aliyedai ametishiwa na bastola na kutekwa cha kushangaza kwa muda wote hakuwahi kufika mahakamani hapo kutoa ushahidi wakati yeye ndiye chanzo cha washtakiwa hao kufikishwa mahakamani.

Rugemarila alisema kwa mamlaka aliyo nayo mahakama hiyo imelifuta shauri hilo hivyo washtakiwa hao wanaachiwa huru huku akitoa vielelezo vyote vilivyotolewa kwenye kesi hiyo virudishwe kwa wenyewe.

Awali Wakili wa Serikali, Grory Kiwale alieleza mahakama hiyo kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini mashahidi wawili walikuwa wanawategemea wapo nje ya mkoa.

Naye Wakili wa utetezi, Peter Kibatara aliiomba mahakama hiyo iondoe shauri hilo Mahakamani kwa kuwa upande wa mashtaka umekuwa ukisuasua kuleta mashahidi ambapo washtakiwa hao wamekaa rumande tangu mwaka 2021

Alidai siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja waliiba katoni 717 za pombe kali aina ya Hennessy vyenye thamani ya Sh408, 650,226 mali ya kampuni ya MMI Tanzania PVT Ltd.

Washtakiwa hawa kabla na baada ya kufanya wizi, wanadaiwa kumtishia Philipo Jeremiah kwa bastola ili waweze kuiba vinywaji hivyo bila kikwazo.

Shataka la pili inadaiwa Juni 26, 2021 maeneo ya Mikocheni B Wilaya ya Kinondoni mshtakiwa Daniel Ocheni akiwa kama kiongozi wa ulinzi alishindwa kuzuia wizi wa katoni 700 za kinywaji cha hennessy ambayo ilikuwa mali ya Kampuni hiyo.

Katika tarehe hiyo maeneo hayo mshtakiwa Leonce Swai akiwa mlinzi wa Kampuni ya ulinzi Gardaw alishindwa kulinda na kusababisha vinywaji hivyo kuibiwa.

Shtaka la mwisho inadaiwa tarehe hiyo eneo la Tabata Kinyerezi wilaya ya Ilala mshtakiwa Arthur Moshiro na Elisha Raphael walikuwa na katoni 66 za kinywaji cha hennessy zinazodhaniwa ziliibiwa katika kampuni  MMI Tanzania PVT.