Kupikia umeme ni nafuu kuliko nishati nyingine - Tafiti

Mhandishi wa nishati na mtaalamu wa matumizi bora ya nishati kutoka UNDP, Sayuni Mbwilo.

Muktasari:

Utafiti wa Tarea umeonyesha unafuu wa gharama unapatikana kama mpishi atatumia majiko sahihi ya presha ya umeme, yanayotumia umeme kiasi kidogo kwa kuwa yametengenezwa kuhifadhi joto

Dar es Salaam. Tafiti zilizofanywa na Chama cha Nishati Jadidifu Tanzania (Tarea) zimebaini nishati ya umeme ikitumika kupikia, hutumia gharama nafuu na muda mfupi kuivisha chakula ikilinganishwa na chanzo kingine cha nishati.

Utafiti huo umeonyesha unafuu wa gharama unapatikana kama mpishi atatumia majiko sahihi ya presha ya umeme, yanayotumia umeme kiasi kidogo kwa kuwa yametengenezwa kuhifadhi joto.

Tafiti hizo zinaonyesha kuwa, maharagwe nusu kilo yanayoweza kuivishwa presha ya umeme wa Sh180, gesi itakayotumika ni ya Sh800, jiko la mafuta ya taa litaivisha kwa Sh600, jiko la kawaida la umeme ni Sh680 na Mkaa wa Sh1180.

Hayo yamesemwa na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda nchini (Tirdo), Tarea na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wakati wa uzinduzi wa kampeni ya pika kijanja inayofanywa na Bongo FM kupitia Shirika la Utangazaji la TBC, ikiwa ni kuunga mkono utekelezaji wa kutumia nishati safi na salama.

Mwenyekiti wa Tarea, Mhandisi Prosper Magari amesema majiko hayo yanaweza kutumika kupikia  maharagwe, nyama, makande kwa muda mfupi wa dakika 25 mpaka 45 na ikatumika uniti moja ya umeme.

“Unatumia uniti moja ya umeme ambayo kwa sasa ni Sh340, maana yake Sh2,000 unaweza kuwa na umeme unaotolesheleza mahitaji yako ya siku nzima, hii tofauti na nishati zingine kama mkaa, kuni na gesi ambapo wanawake hutumia Sh4000 mpaka 10,000 kwa siku,” amesema.

Amesema tafiti zimeonyesha ni nafuu hiyo itapatikana kama utatumia majiko sahihi hasa ya presha ya umeme, pamoja na mengine yanayoshauriwa kitaalamu kwa kuwa yametengenezwa kutumia umeme mdogo.

“Haya ni majiko yanayotumia umeme kiasi kidogo lakini yametengenezwa kuhifadhi joto kwa hiyo yanatumika kuchemsha chakula na kikishachemka lile joto lililohifadhiwa ndiyo linatumika kuivisha chakula,” amesema Magari.

 “Binafsi natumia majiko haya, nimethibitisha nina majiko matatu ya umeme la kwanza ni la presha ya umeme linahifadhi joto kwa kiasi kikubwa, natumia kwenye mapishi kama maharagwe na vyakula vingine vigumu. Ninapoanza mapishi narekodi kiasi kilichobaki cha umeme kilichobaki kwenye mita ya umeme nimefanya hivyo kwa kipindi cha miaka miwili sasa.”

Mhandishi wa nishati na mtaalamu wa matumizi bora ya nishati kutoka UNDP, Sayuni Mbwilo umeme ni gharama kama jiko unalotumia halijafikia ubora unaoweza kupika na usione bili kubwa au umeme mwingi ukitumika.

“Tumekuja na mlengo wa kupunguza matumizi kwa kuanza na sera zetu, TBS anaenda kutengeneza viwango majiko yetu yanayoingia nchini hayataingia hovyo tena, tutakuwa na yale majiko bora pekee ndio yanaingia nchini,” amesema Sayuni.

Elizabeth Ngowe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) amesema tafiti zilizofanyika zimeonyesha umeme ni bei rahisi kuliko nishati zingine na wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi kutumia majiko bora ya umeme au majiko sanifu ili kutumia nishati kidogo kupikia.

Amesema watafanya kwa vitendo kuhusu tafiti hizo kupitia matamasha mbalimbali yatakayofanyika katika miji na vijiji nchini ili kujenga uelewa zaidi.

Akizungumzia kampeni hiyo ya Pika Kijanja Inayofanywa na Bongo FM, Mkurugenzi wa Huduma za Redio TBC, Aisha Dachi amesema lengo ni kuunga mkono Serikali katika utekelezaji wa kutumia nishati safi na salama ambayo ni changamoto kubwa katika mazingira.

“Mwanamke anataabika na anapata athari kiafya pia inayomsababishia mtoto wa kike apate muda wa kutosha kujiendeleza kimasomo,” amesema Dachi.