Lema mbioni kutua nchini, Gambo asema hana hofu naye

Aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Muktasari:
- Chadema Kanda ya Kaskazini yasema mwenyekiti wao Godbless Lema yupo mbioni kurejea Tanzania baada ya kuishi Canada kwa miaka takribani miwili, yaweka wazi majukumu yanayomsubiria.
Arusha. Wakati aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, anatarajiwa kutua nchini kati ya Januari 21 au Februari, mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Mrisho Gambo amesema hana hofu na ujio wa mpinzani wake.
Lema ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema anatarajiwa kupokelewa na maelfu ya wafuasi wa Chadema, katika Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Mbunge huyo wa zamani ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini atarejea nchini, akitokea nchini Canada alikokuwa akiishi baada ya kuondoka Tanzania Novemba akihofia usalama wake na familia yake.
Akizungumza na Mwananchi jana, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa amesema mwenyekiti wake anaweza kurudi kati ya Januari 21 au wiki ya mwanzo ya Februari.
"Tuna ratiba na tumepanga naye kwamba atarejea na tarehe ilikuwa kabla ya Januari 21 ili kuwahi uzinduzi wa mikutano ya hadhara lakini kuna mambo yamejitokeza ya ratiba ya ndege.
"Alikuwa na safari moja ya kwenda New York kwa hiyo, tumebadilisha ratiba yake anaweza akaja wiki ya Februari 4, hiyo ndiyo ratiba ya pili tuliyokuwa tumeitengeneza, iwapo safari yake ya New York ataiahirisha kuna uwezekano akaja kabla ya Januari 21," amesema Golugwa.
Kwa mujibu wa Golugwa, safari ya New York ni muhimu kidogo kwa sababu inahusu masuala ya chama hicho Kanda ya Kaskazini na Marekani.
Golugwa alisema amesema baada ya Lema kuwasili miongoni mwa shughuli za kichama atakazozifanya ni pamoja na kusimamia kikao cha baraza la uongozi la Kanda litakaloshirikisha viongozi kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
Wananchama wengine watakaoshiriki kikao hicho ni pamoja na waliokuwa wagombea 35 wa ubunge kutoka majimbo 35 yaliyopo kwenye mikoa hiyo.Pia atafanya mikutano mikubwa minne ya hadhara katika makao makuu ya mikoa ya kanda ya kaskazini.
"Lema atafanya mkutano mkubwa wa hadhara atashiriki ziara ya kitaifa za mikutano ya hadhara itakayozunguka nchi nzima," amesema Golugwa.
Gambo asema hana hofu na Lema.
Akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Kilombero Gambo, alisema hana hofu na ujio wa Lema akisema alishazungumza naye. Gambo amedai kuwa Lema ni mjomba wake hivyo wale wanaodhani wana ugomvi sio hivyo.
Gambo amesema tangu amekuwa mbunge amefanya mikutano mingi ya kuhamasisha maendeleo tofauti na miaka 10 ya uongozi wa Lema aliyedai alikuwa anahimiza ujasiri wa kuitukana Serikali.
“Fikisheni ujumbe kwa wengine kuwa sasa mna mbunge ambaye akikutana changamoto za mama ntilie anatatua na sio yule…,” amesema Gambo
Katika ziara hiyo, Gambo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Arusha aligawa majiko 100 ya gesi kwa mama Ntilie akiwataka wakazi wa Arusha kufikisha ujumbe wa kwamba hivi sasa wana mbunge anayesikiliza kero zao na kuzitatua.
Makada wa CCM na Chadema wasubiri mchuano Lema na Gambo.
Joram Yohana kada wa CCM amesema walikuwa na hamu ya mikutano kwani hivi sasa wapinzani hawana hoja tena na wananchi wanawapima upya.
"Mama Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) ametatua kero zote sasa tunawasuburi waje na uongo wao na tutawajibu kwa hoja" amesema
Naye, Leonard Masawe mwanachama wa Chadema amesema walikuwa na hamu ya mikutano ya hadhara akisema kuna viongozi walipita bila kupingwa katika chaguzi zilizopita na hawana uwezo.