Lowassa, Gambo washiriki mazishi ya Laigwanani Monduli

Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowasa ameshiriki mazishi ya Mzee wa Mila ya kimaasai wilaya ya Monduli,Laigwanani Mepukori Mberekeri

Muktasari:

Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amewaongoza waombolezaji kwenye mazishi ya kiongozi Mkuu wa mila wa jamii ya Kimaasai wilayani Monduli leo Jumamosi.

Monduli. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo wameshiriki mazishi ya Mzee wa Mila ya Kimaasai wilaya ya Monduli, Laigwanani Mepukori Mberekeri.

Pia, kulikuwapo na viongozi mbalimbali akiwamo mbunge wa Monduli (CCM), Julius Kalanga na mkuu wa wilaya hiyo, Rashid Taka.

Katika salamu zake alizotoa kwenye mazishi Kijiji cha Mti Mmoja, kata ya Sepekp leo Jumamosi Januari 5, 2019, Lowassa amesema marehemu wakati wa uhai wake alikua kiongozi aliyejihusisha kuhamasisha amani na utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa jamii ya wafugaji.

"Marehemu alitumia kipawa chake vizuri na alikua kiongozi mahiri katika jamii yetu kwa kuunganisha na kuhakikisha tunaishi kwa upendo," amesema Lowassa akimzungumzia marehemu ambaye alizaliwa, Aprili 15, 1959.

Naye Gambo ambaye yupo kwenye ziara ya kuhamasisha ujenzi wa madarasa wilayani humo amesema Mepukori atakumbukwa kwa kupenda elimu wilayani humo.

"Niwape pole familia hii kwa msiba uliowakuta, Serikali siku zote imekua ikishirikiana na viongozi wa mila kuhamasisha maendeleo na amani," amesema Gambo. 

Laigwanani mkuu wa mila ya jamii ya kimaasai nchini, Lekisongo Meshuko Meijo amesema jamii hiyo imepata pigo ambalo halitazibika na kuitaka, jamii na familia ya marehemu kudumisha amani na utulivu kwa kuendeleza mema yote.