Luteni Urio asoma mawasiliano yake na Mbowe mahakamani

Muktasari:

  • Luteni wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Denis Urio amesoma mawasiliano ya ujumbe mfupi wa simu kati yake na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ikiwemo ya yeye kuomba na kutumiwa nauli ya Sh500,000 kwa ajili ya kuwasafilisha washtakiwa.

Dar es Salaam. Luteni wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Denis Urio amesoma mawasiliano ya ujumbe mfupi wa simu kati yake na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ikiwemo ya yeye kuomba na kutumiwa nauli ya Sh500,000 kwa ajili ya kuwasafilisha washtakiwa.

Shahidi huyo wa 12 wa Jamhuri katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mbowe na wenzake watatu amesoma meseji hizo leo Alhamisi Januari 27, 2022 mbele ya Jaji Joachim Tiganga

Ifuatayo ni maelezo ya ushahidi wa Luteni Urio

Jaji ameshaingia Kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali Robert Kidando anatambulisha mawakili na Kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi Wakili Peter Kibatala nae anatambulisha.

Mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi,  Abdallah Chavula anaendelea kumuongoza shahidi wa 12, Komando Luteni Denis Leo Urio kutoa ushahidi kuanzia alipoishia jana baada ya jaji Tiganga kumkumbusha shahidi kuwa bado yuko katika kiapo.

Shahidi: Nakumbuka tarehe 12/8/2020 nilipeleka simu kwa Inspekta Swila simu tatu, makao makuu ya Polisi Dar es salaam.

Shahidi: Simu hizo zilikuwa ni mali yangu. Simu ya kwanza ni Tecno C9, ya pili ilikuwa ni Itel na simu ya tatu ilikuwa ni Samsung ndogo ya Tochi.

Shahidi: Baada ya kufika nilikutana na Inspekta Swila nikakabidhi simu moja baada ya nyingine kwa kujaza nyaraka ambayo niliandika majina yangu, IMEI ya kila simu, nikasaini naye akasaini na tarehe. Jumla nilikabidhiwa nyaraka nne.

Shahidi: Kwa siku hiyo tu niliandikiwa nyaraka tatu, aliziandaa Insp. Swila.

Shahidi: Alinipatia(nyaraka) akanielekeza mahali pa kusaini nikasaini akatoa kopi akanikabidhi.

Shahidi: Nyaraka iliyoandaliwa tarehe 11/8/2020  na Insp. Swila naweza itambua kwa majina yangu, tarehe ya siku hiyo 11/8/2020 halafu nitaitambua kwa saini yangu.

Wakili Chavula anaomba na kumuonesha shahidi nyaraka anamtaka aieleze mahakama Kama anaifahamu

Shahidi: Mheshimiwa Jaji naitambua nyaraka hii kwa majina yangu matatu, Denis Leo Urio, ina tarehe 11/8/2020, saini yangu ipo

Mheshimiwa Jaji ningependa mahakama iitambue nyaraka hii.

Mawakili wote wa utetezi, Nashon Nkungu kwa mshtakiwa wa kwanza, John Mallya (kwa mshtakiwa wa pili) Dickson Matata ( jwa mshtakiwa wa tatu) na Peter Kibatala ( kwa mshtakiwa wa nne), baada ya kuikagua wanaieza mahakama kuwa hawana pingamizi nyaraka hiyo kupokewa kwa ajili ya utambuzi.

Jaji Tiganga: Naipokea (nyaraka hii) Kama ID2.

Shahidi anaendelea akiongozwa na wakili Chavula

Shahidi: Simu yangu Tecno camon ina cover nyeusi kwenye kioo cha juu screen protector yake imepasukapasuka, kama ikiwashwa inatoka picha ya familia yangu, nime-save kwenye screen saver nime-save picha ya mke wangu na mtoto, kwenye program ya telegram Kuna mawasiliano yangu na Freeman Mbowe.

Wakili Chavula: Mheshimiwa Jaji tunaomba kielelezo cha upande wa mashtaka namba 34.

Karani anampatia wakili Chavula kielelezo hicho na wakili Chavula anamkabidhi shahidi ili aweze kukitambua kwa vigezo alivyovitaja. Anamwambia shahidi akitazame kielelezo hicho kisha aseme ni nini na shahidi baada ya kuitazama anasema:

Shahidi: Mheshimiwa Jaji kwa mwonekano wa nje hii ndio simu yangu. Nilisema ina cover nyeusi na simu yenyewe ni Tecno Camon.

Wakili Chavula anaiomba mahakama shahidi aiwashe simu ili aendelee na utambuzi.

Jajii anauliza upande wa utetezi na wakili Kibatala anasema hawana pingamizi kwa ombi Hilo.

Shahidi anawasha simu inatokea picha ya mkewe mtoto na shahidi anaielekeza kwa jaji kumuonesha picha hiyo.

Wakati shahidi anaendelea kuikagua simu hiyo kuangalia kigezo kingine alichokitaja, wakili Chavula anawasogelea mawakili wa utetezi wananong'onezana kidogo kisha anatabasamu na kumrudia shahidi.

Shahidi aneendelea na utambuzi wa simu hiyo baada ya kufungua sehemu ya mawasiliano ya ujumbe mfupi kupitia mitandao wa Telegram Kisha anasema: hapa Kuna mawasiliano yangu ya ujumbe mfupi na Freeman Mbowe.

Wakili Kibatala anakwenda kwa shahidi kujiridhisha mawasiliano hayo, anafuatiwa na wakili John Mallya, Kisha wakili Dickson Matata na hatimaye wakili Nashoni Nkungu

Wakati hayo yakiendelea Mbowe ametulia kizimbani akifuatilia kwa umakini huku akiwa ameweka mkono wake wa kulia shavuni kabla ya kuushusha lakini akiendelea kufuatilia taratibu hizo, huku washtakiwa wenzake wawili, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling'wenya wakinong'onezana mara kwa mara na kutabasamu.

Wakili anamuuliza Shahidi Kama anaweza kusoma meseji hizo na shahidi anaanza kuzisoma:

Hayo ni majadiliano baina ya Shahidi, Luteni Denis Leo Urio na Mbowe wakijadili kuhusu Makomando ambao shahidi alidai kuwa Mbowe alimuomba amtafutie.

Shahidi: Meseji ya kwanza inasema “Kaka wale mtu tatu au nne ni muhimu sana siku zinakwisha”

Shahidi: Kilichokuwa kinazungumzwa hapo ni baada ya mazungumzo siku za nyuma kumtafuta Moses Lujenge na wengine kwa hiyo waende maana siku zinakwisha.

Shahidi: Ujumbe ulikuwa unatoka kwa Freeman Aikael Mbowe kuja kwangu.

Shahidi: Saa 2:14:50: tarehe 20/7/2020:

" Mmoja kazaliwa mwaka 1980 na mwingine 1986

Shahidi: 1980 ni Moses Lujenge na 1986 ni Bwire

Tarehe hiyohiyo ujumbe wa saa 2:02 unasema

" Broo kuna member wawili mmoja yuko Tunduma anasafirisha magari nje ya nchi ( Halfan Hassan Bwire) na mwingine yuko Dodoma anafanya kazi kampuni ya Yapi ni Moses Lujenge. Hi ilitoka. Kwangu kwenda kwa Mbowe.

Ujumbe mwingine unasomwa: Simu siyo salama sana niwezeshe niweze kukutana nao waje.

Shahidi: Hii ilikuwa inatoka kwangu kwenda kwa Mbowe.

Meseji nyingine; Kikubwa ni kuwa na security ya hizo shughuli zao wanazofanya ili wasije kutelekezwa baadaye.

Shahidi: Hii ilitoka kwangu kwenda kwa Freeman Aikael Mbowe.

Meseji nyingine: Hao wawili kwa kuanzia siyo mbaya hawawezi kutelekezwa, watakuwa na Mimi, fulltime, wamekwambia wanataka nini?.

Shahidi: Hii ilitoka kwa Freeman Aikael Mbowe kuja kwangu.

Hao wawili ni Halfan Bwire na Moses Lujenge.

Inayofuata: Sema tu kaka nifanye?

Shahidi: Ilitoka kwa Freeman Aikael Mbowe.

Inayofuata: Mmoja kazaliwa 1980 mwingine 1986

1980 ni Moses Lujenge na 1986 ni Halfan Hassan Bwire.

Inayofuata: Naomba unitumie nauli niwa-mobilise nikutana nao Moro. Hii ilitoka kwangu kwenda kwa Freeman Aikael Mbowe. Hao wa kukutana nao Moro ni Halfan Bwire na Moses Lujenge.

Meseji ya saa2:09 Hao wawili kuanzia siyo mbaya walikuwa ni Moses Lujenge na Halfan Hassan Bwire.

Meseji nyingine: Nikutumie kiasi gani na kwa njia gani?

Shahidi: Ilitoka kwa Mbowe kuja kwangu

Hiki kilikuwa ni kiasi cha pesa kwa ajili ya Halfan Bwire, Moses Lujenge kwenda kwa Freeman Aikael Mbowe. meseji ilikuwa inatoka kwangu kwenda kwa Mbowe.

Meseji inayofuta Laki 500000 kwa namba 07875552000,

Shahidi:  ilitoka kwangu kwenda kwa Mbowe

Meseji inayofuata;

Sawa tayari kaka.

Shahidi: Ilitoka kwa Freeman Aikael Mbowe.

Inayofuta

Nashukru niimepata nitakupa majibu jioni.

Shahidi: Hii ilitoka kwangu kwenda kwa Mbowe.

Inayofuata 6/8/2020

Hallow bro nimeshindwa kupokea simu yako kwa sababu... Nadhani umenielewa. Any news?

Shahidi: Ilitoka kwa Freeman Aikael Mbowe kuja kwangu.

Wakili Chavula anairudisha kielelezo hicho(simu) kwa mahakama anaendelea kumuongoza shahidi.

Shahidi: Simu aina ya Tecno C9 niliyopeleka kwa Insp. Swila tarehe 12/8/2020, nikiiona nitaitambua kwa juu kushoto imepasuka, halafu ukiiwasha inawaka halafu inazima, ni ya rangi nyeusi.

Wakili Chavula anaomba kielelezo cha 28 (simu ya Tecno C9) anakuonesha shahidi ili aitambue kama ndio simu yake aliyoipeleka kwa Insp. Swila.

Shahidi baada ya kuiangalia, wakili anamuuliza ni kitu gani na shahidi anasema:

Hii ndio simu yangu Tecno C9. Anamuonesha Jaji kwa kuinyanyua juu na kuelezea hali yake kwamba imepasuka housing juu kushoto.

Wakili Chavula anaomba ruhusa ya Mahakama na shahidi anaiwasha simu hiyo, Kisha anasema kuwa haiwaki.

Wakili Chavula anairejesha kwa mahakama simu hiyo, kisha anaendelea kumuongoza namna ya kutambua simu yake nyingine Aina ya Itel ambayo pia aliikabidhi kwa Insp.Swila.

Shahidi: Ina mfuniko wa bluu, halafu screen protector yake mbele imepasuka, halafu ukiiwasha itatokea picha ya mke wangu na watoto au ya kwangu mwenyewe.

Wakili Chavula anaomba na anapewa kielelezo cha 23(simu aina ya Itel) na anamuonesha shahidi Kama anaitambua na shahidi anasema kuwa ameitambua kwa vigezo alivyovitaja.

Wakili Chavula anairejesha simu hiyo kwa mahakama kisha anamuongoza shahidi kutambua simu aina ya Samsung.

Shahidi: Simu hiyo ni simu ndogo ya tochi nyeupe, eneo la earphone plug imekatika.

Wakili Chavula anaiomba simu hiyo (kielelezo cha 29) na anampatia shahidi aitazame kisha aieleze mahakama ni nini.

Shahidi anasema kuwa ameitambua simu hiyo kuwa ndio simu yake aina ya Samsung ya tochi, nyeupe na imepasuka kwenye earphone plug.

Baada ya kuitambua wakili Chavula anairejesha mahakamani simu hiyo kisha anaendelea kumuongoza shahidi na shahidi anaeleza:

Shahidi: Nilisema kuwa nilifahamiana na Mbowe kuanzia mwaka 2008 mpaka 2020, kwa maana kwamba baada ya kumsaidia kupata vijana wa kwenda kumsaidia kuchukua alikata mawasiliano nami, Julai 24, 2020.

Shahidi: Mahusiano yetu yalikuwa mazuri tu sasa sijui ni kwa nini alikata mawasiliano.

Shahidi: Kiasi cha pesa nilichopokea kutoka kwa Mbowe kwa ajili ya kuwapeleka vijana wa kushirikiana naye ni Sh699,000.

Wakili anamuongoza shahidi kumtambua Mbowe (mshtakiwa wa nne) namna anavyomtambua.

Shahidi: Kwanza ni mpole, anapenda kuvaa niwani, mwenywe uso wa duara, mnene kiasi mrefu, mweusi.

Mbowe anavua miwani Kisha anaongea na washtakiwa wenzake Kisha wanatabasamu.

Wakili anamuliza shahidi kuwa ni yupi anasema ni yule pale aliyevaa miwani karibu na askari magereza

Maelekezo hayo yanamfanya Mbowe, wenzake mawakili na baadhi ya wasikilizaji kucheka na kunong'onezana kwa maana wakati huyo Mbowe alishavua miwani kabla ya kuivaa tena.

Shahidi: Hakuna mwingine niliyempa taarifa. Niliamua kumpa taarifa DCI na si wakubwa wangu kwa maana ni taarifa za uhalifu na anayehusika na uchunguzi ni  ofisi ya DCI.

Shahidi: Baada ya ukamataji (watuhumiwa kukamatwa), taarifa hizo nilimwambia kiongozi wangu wa kazi, mkuu wa kituo ninachofanyia kazi, 92 KJ.

Wakili Chavula: Mheshimiwa, kwa upande wetu ni hayo tu

Sasa ni zamu ya mawakili wa utetezi kumhoji shahidi kuhusiana na ushahidi wake, anaanza wakili wa mshtakiwa wa kwanza, Nashon Nkungu.

Wakili:Ulisema we ni mkristo

Shahidi:Ndio

Wakili Nkungu: We ni mkristo wa dhehebu gani?

Shahidi: Roman Katholiki

Wakili Nkungu: Mara ya mwisho kwenda kanisani ni lini?

Shahidi:Jumapili

Wakili Nkungu: Kanisa gani

Shahidi:Ngerengere

Wakili Nkungu: Na iwapo utaeleza sababu za nyuma ya pazia zilizofanya ukafanya haya uliyoyafanya na Jeshi nalo litakulinda?

Shahidi: Nafahamu

Shahidi: Hebu rudia swali sijakuelewa.

Wakili Nkungu: Kwamba iwapo utaeleza sababu zilizokufanya ukafanya haya yote na sababu zilizopo nyuma ya pazia na visa vyote hata Jeshi litakulinda?

Shahidi: Hata sasa Jeshi liko pamoja nami?

Wakili Nkungu: Ni kisema hukutoka kazini kwako utabisha

Shahidi:Nitabisha

Wakili Nkungu: Na kutoka kunahitajika ruhusa?

Shahidi :Ndio

Wakili Nkungu: Huitaji remove order

Shahidi:Kwa lipi

Wakili Nkungu: Una ruhusa hapa

Shahidi :Ninayo

Wakili Nkungu: Iko wap

Shahidi:  Hotelini kwangu

Wakili Nkungu: Ulipewa ruhusa na Kiongozi wako

Shahidi :Ndio

Wakili Nkungu: Anaitwa nani

Shahidi: Siwezi kumtaja hapa hadi nipewe ruhusa

Wakili Nkungu: Ulisema Kikosi cha 92kj kinatoa mafunzo ya ukomandoo

Shahidi:Ndio

Wakili Nkungu: Sehemu gani nyingine hapa nchini wanatoa mafunzo hayo

Shahidi: Siwezi kusema kwa ajili ya usalama

Wakili Nkungu: Nyie kwa mwaka mnatoka makomandoo wangapi

Shahidi :Siwezi kusema kama kiapo changu kinavyosema

Wakili Nkungu: Komandoo mmoja anachukua muda gani

Shahidi:Siwezi kusema kama kiapo changu kinavyosema

Wakili Nkungu: Mafunzo yako ya ukomandoo umefuzu lini

Shahidi:Siwezi kusema

Wakili Nkungu: Mheshimiwa naomba mahakama imuamuru Shahidi huyu kujibu maswali kwa sababu hataki kujieleza yeye ni nani

Jaji: Chini ya kifungu gani?

Wakili Nkungu: Kifungu cha 264 CPA HC itakuwa na mamlaka kwa kuratibu mwenendo katika mashauri ya Jinai. Kwa kuwa ni suala la kisheria pale ambapo shahidi hataki kutoa majibu, tunaomba mahakama yako itoe amri

Wakili Chavula: Ikupendeze Mheshimiwa Jaji, tumemsikiliza msomi mwenzetu wakili Nashon Nkungu hoja zake. Kwa heshima zote  hatukubaliani na maombi yake kwa kuwa hayana mashiko kisheria. Mheshimiwa jaji wakili anaiomba mahamama imlazimishe shahidi kujibu level ya mafunzo yake, ambalo Shahidi amesema ni siri hawezi kutamka hadharani yeye ni wa level gani.

Wakili Chavula: Wakili ameielekeza mahakama kifungu cha 264 sura ya 20 mapitio ya mwaka 2019. kwamba mahakama ina mamlaka ya kum-compel shahidi.

Wakili Chavula: Hapa tafsiri iko wazi kwamba mamlaka ya mahakama katika hili inategemea na sheria nyingine.

Wakili Chavula: Masuala ya kiushahidi yana Sheria yake ambayo ni Sura ya 6 na ina kifungu mahsusi ambacho kinaelekeza ni mazingira yapi shahidi anaweza akaelekezwa na Mahakama kujibu swali

Wakili Chavula: Kifungu cha 158 cha sheria hiyo kimeeleza mazingira ambayo mahakama inaweza kumlazimisha shahidi.

Wakili Chavula: Hata kifungu cha 156, cha sheria hiyo nacho kinatoa mazingira hayo.

Jaji: Ungetusaidia kifungu hicho kinasemaje.

Wakili Chavula: Sawa, Mheshimiwa Jaji Mimi nitajielekeza kifungu cha 158.

Wakili anakisoma kifungu hicho Kisha anasema:

Wakili Chavula: Mheshimiwa jaji swali la level gani ya mafunzo ya shahidi halina uhusiano na kinachojadiliwa mbele ya mahakama hii.

Wakili Chavula: Masuala ya namna hii labda yawe yanapelekea ku- injur character ya witness basi yanapelekea shahidi kulazimishwa.

Wakili Chavula: Mhesjimiwa Jaji, Kinyume na hapo, shahidi hawezi kulazimishwa.

Wakili Chavula: Mheshimiwa jaji Wakili hajaonesha mahakama kuwa lengo la maswali hayo ku- injure character yake. Suala  la force inatoa makomando wapi, wangapi,  ina vituo vingapi vya mafunzo ya ukomando  maoni yetu hayaendi ku-distort character ya shahidi.

Wakili Chavula: Mheshimiwa jaji siye tunachokiona hapa yawezekana  wakili ameshindwa kum- Shake shahidi sasa anataka kuishirikisha mahakama.

Wakili Chavula: Mheshimiwa jaji hata maswali yenyewe haya hayaangukii kwenye section 158. Una-test velocity ya shahidi kwa kutaka kujua Jeshi linatoa Makomando wangapi, kuna vituo vingapi vya makomando?

Wakili Chavula: ni kusimamia maaskari waliochini yake.

Wakili Chavula: Shahidi amekuja kutoa ushahidi kwa kile alichokisikia na kupelekea kesi hii mahakamani.

Wakili Chavula: Sasa Mheshimiwa Jaji katika mazingira haya tunayaona kwamba maswali ya wakili hayana relevance. Hata ukiyaangalia kwa namna yoyote haya-affect character ya shahidi.

Wakili Chavula: Sasa hata Kama angefuata utaratibu bado yasingewezana lakini ameilekeza mahakaam kwenyw utaratibu mwingine bila kujua kuwa mahakama haiwezi kukiwekea utaratibu mwingine tofauti.

Wakili Chavula: Kwa hiyo Mheshimiwa Jaji Ni maoni yetu kuwa maombi ya shahidi hayana mashiko ajielekeze kwenye maswali ambayo yanaweza ku-distort character ya shahidi.

Wakili Chavula: Ni maoni yetu kwamba shahidi yuko sahihi na kwa aina ya maswali anayoyauliza mahakama haina mamlaka ya kumlazimisha kujibu

Wakili wa Serikali Mwandamizi Pius Hilla: Mheshimiwa Jaji shahidi aliyeko kizimbani aliulizwa swali kujusiana na level yake ya ukomando akajieleza kwa kinagaubaga kuwa kwa kiapo chake hawezi kueleza level yake.

Wakili Hilla: Mheshimiwa jaji tuna- underline neno kwa kiapo chake. Mheshimiwa Jaji ni kosa la jinai ku- communicate information ambayo ni confidential, kwa mujibu wa The National Service Act.

Wakili Hilla: Kwa kuwa shahidi amekwishaeleza kwamba kwa kiapo chake haruhusiwi ku-communicate level ya kiapo chake, mahakama haiwezi kumlazimisha.

Wakili Hilla: Mheshimiwa jaji nimalizie tu kwa kusema kwamba kwa kuwa imeshafahamika kuwa taarifa kuhusu level ya mafunzo yake na kwa kuwa kuna backup ya sheria, remedy si kumlazimisha.

Wakili Hilla:  Mheshimiwa jaji kwa fact za kesi hii yako maswali mengi ya kuulizwa.

Wakili Hilla: Mheshimiwa jaji pasipo kukuchosha naomba mahakama itupilie mbali maombi haya.

Wakili Nkungu: Mheshimiwa Jaji this is very funny sababu leo nimeshuhudia objection kupinga identity ya shahidi, kama ambavyo ningemuuliza una elimu gani.

Hilla: Mheshimiwa Jaji sisi hatupingi identity ya shahidi bali kumlazimisha kwa kiapo chake.

Nkungu: Mheshimiwa Jaji tunachoomba mahakama yako ikilinde

Nkungu: Hapa shahidi ameapa kiapo kimoja tu. Tunakumbuka kesi moja huko Morogoro ambako Shahidi walikuwa wanakataa kuapa ambapo mahakama iliwalazimisha.

Nkungu: Na hapa Shahidi ameapa kiapo kimoja tu na tunaomba mahakama yako.

Nkungu: Kwa kifungu cha 164 maombi haya relevant kwani tunataka kuona ana ujuzi gani na mambo haya tunayatumia kwenye ushahidi.

Nkungu: Amesema yeye ni kiongozi anaongoza askari 30 na afisa mmoja tunataka kujua ana rank gani.

Nkungu: Kama ambavyo mashahidi wengine wamekuja na kutaja ujuzi wao sioni kwa nini kwa shahidi huyu isiwezekane.

Nkungu: Hatuoni ni namna gani ita- prejudice  ushahidi wake.

Nkungu: Kwa hiyo tunaona hakuna sheria ambayo inamzuia .

Nkungu: Tunawakumbusha tu wenzetu kuna usemi kuaa mwosha huoshwa. Ni katika kesi hii wenzetu at a certain point wakiuliza kuwa komandoo mmoja na uwezo wa kuwamudu watu wangapi, lakini sisi hatuku-object.

Nkungu: Kumzuia shahidi huyu kujibu maswali hayo itakuwa ni Kuzuia ushahidi muhimu sana kwenye kesi hii.

Jaji: Samahani, kuna suala wame- question jurisdiction ya Mahakama hii.

Wakili: Mheshimiwa Jaji mahakama kwa kutumia vifungu hivi vyote vilivyotajwa hapa ni vifungu wezeshi.

Nkungu: Kama hakuna hicho kifungu ambacho kinakataza kwa kuwa tumeonesha relevance basi shahidi yuko compellable.

Nkungu: Mheshimiwa jaji kwa submission hizo na kwa kuwa hakuna sheria yoyote ambayo imetolewa Kuzuia kutolewa kwa information hizo narudia ombi langu kum-compel shahidi kutoa majibu.

Jaji: Mme- cite sheria na vifungu kadhaa ili niweze kutoa maelekezo nahitaji muda. Hivyo naahirisha shauri hili kwa muda wa dakika 30.