Urio aeleza alivyomtafutia Mbowe makomandoo na kuahidiwa cheo

Muktasari:

  • Shahidi wa 12 katika kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu leo Jumatano Januari 26,2022  ameieleza mahakama namna Mbowe alivyomuomba amtafutie makomandoo watakaomsaidia kutekeleza mipango ya ugaidi.

Dar es Saalam. Shahidi wa 12 katika kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu leo Jumatano Januari 26,2022  ameieleza mahakama namna Mbowe alivyomuomba amtafutie makomandoo watakaomsaidia kutekeleza mipango ya ugaidi.

Luteni Denis  Urio ambaye ni ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) toka kikosi cha makomando kilichopo Ngerengere, Morogoro amedai Mbowe alimweleza kuwa chama chake kilitaka kuchukua nchi kwa gharama yoyote huku akimwahidi kumpa cheo kikubwa endapo lengo hilo litafanikiwa.

Shahidi huyo ameieleza mahakama kwamba ndiye aliyeripoti tuhuma hizo kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Baada ya kutoa taarifa hizo, Luteni Urio alikabidhiwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha, Ramadhani Kingai aliyemtaka aendelee kushirikiana na Mbowe na wakati huo huo akiwapa taarifa polisi juu ya kinachoendelea.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Joachim Tiganga katika Mahakama Kuu (Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Ifuatayo ni maelezo ya ushahidi wa Luteni Urio siku alipokutana na Mbowe.

Wakili Kidando:  Shauri limekuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa na leo tuma Shahidi mmoja

Jaji: Atakuwa Shahidi wa ngapi

Wakili Kidando: Shahidi wa 12

Shahidi anaingia Mahakamani na anapanda kizimbani kisha Jaji anamuuliza majiana yake

Jaji: Majina yako

Shahidi: Naitwa Luteni Denis Leo Urio

Jaji: Umri wako

Shahidi: Miaka 42

Jaji: Kazi yako?

Shahidi: Afisa wa Jeshi la Wananchi JWTZ

Jaji: Kabila lako

Shahidi: Mchanga

Jaji: Dini yako?

Shahidi: Mkristo

Kisha karani anamuongoza kuapa na anaongozwa na wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula , naye shahidi anasema: Naitwa Luteni Denis Leo Urio, naishi Ngerengere, Morogoro

Shahidi: Kazi yangu ni Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, cheo changu ni Luteni, kituo changu cha kazi Ngerengere Morogoro Kikosi Maalum.

Shahidi: Majukumu yangu ni kusimamia Askari walioko chini yangu, ninaongoza Askari 30 na afisa mmoja wanaofanya kazi katika kikosi Maalumu yaani waliopata mafunzo Maalumu ya ukomando.

Shahidi: Nimetumia Jeshi kwa miaka 18 sasa, nilijiunga na Jeshi  tarehe 16/6/2003.

Shahidi: Majukumu ya Jeshi ni pamoja na ulinzi wa mipaka ndani na nje ya nchi na kulinda amani katika mataifa yenye migogoro.

Shahidi: Nimekuwa na cheo cha Luteni kwa miaka 6 sasa.

Shahidi: Nimewahi kushirki ulinzi wa amani Darfur mwaka 2011 na Sudani ya Kusini mwaka 2019

Shahidi: Halfani Hassan Bwire nafahamiana naye kwa muda mrefu nilimpokea na kufanya naye kazi kituo kimoja cha 92 Kikosi cha Jeshi (KJ) nikamfanyia training. Nimemfahamu tangu 2006 Hadi 2019. Alikuwa kiongozi mdogo na cheo chake alikuwa Koplo

Shahidi: Alianza kuserve kwenye Military Service kuanzia 2006 mpaka 2019 alipofukuzwa kazi jeshini.

Shahidi: Sababu za kufukuzwa kazi ni utovu wa nidhamu (Bwire ni mshtakiwa wa kwanza)

Shahidi: Wakati anafukuzwa kazi mimi nilikuwa Sudan kwenye operesheni.

Shahidi: Nilifahamu mwaka 2020 mwezi wa 3 kwamba amefukuzwa kazi jeshini kwa utovu wa nidhamu.

Shahidi: Nilipata taarifa hiyo kutoka kwa Administration Officer of the Unit (Afisa wa Utawala Jeshini).

Shahidi: Mahusiano yangu na Halfan Hassan Bwire  tangu 2006 Hadi ajira yake ilipokoma yalikuwa mazuri kama kiongozi na afisa wake.

Shahidi: Baada ya ajira yake kukoma nilikuwa naendelea kuwasiliana naye, mahusiano yetu yalikuwa ya kawaida tu kwamba tulikuwa tunawasiliana.

Shahidi: Adamu Hassan Kasekwa (mshtakiwa wa pili) nafahamiana naye toka 2012 sababu ndio alifika kwenye unit na nikampokea mimi akaingia kwenye mafunzo kikosi Maalumu kam-train, akawa staff of the unit. Alifikuzwa kazi jeshini, kwa sababu za utovu wa nidhamu

Shahidi: Alifanya kazi kikosini mpaka mwaka 2018. Mpaka anafukuzwa alikuwa na cheo cha Private soldier, Askari ambaye hana rank.

Shahidi: Wakati anafukuzwa kazi mwaka 2018 mimi nilikuwa Arusha Kozi.

Shahidi: Baada ya kurudi kwenye kituo changu cha kazi ndipo nilipata taarifa kuwa amefukuzwa kwa utovu wa nidhamu. Nilipata taarifa kwa Admin Officer ofisini kwake.

Shahidi: Mahusiano yetu na Adamu Hassan Kasekwa yalikuwa mazuri. Baada ya kufukuzwa pia bado mahusiano yetu yaliendelea kuwa mazuri.

Shahidi: Mohamed Abdillahi Ling'wenya (mshtakiwa wa tatu) namfahamu kwa sababu nimefanya naye kazi kituo kimoja.  Kikosi cha 92 KJ.

Shahidi: Nilianza kufanya naye kazi kuanzia mwaka 2010 mpaka mwaka 2017.

Shahidi: Mohamed Ling'wenya alifikuzwa kazi kwa utovu wa nidhamu. Wakati anafukuzwa kazi alikuwa private soldier (Askari mwenye cheo cha mwisho).

Shahidi: Mahusiano yetu wakati tunafanya kazi pamoja tulikuwa na mahusiano mazuri.

Shahidi: Hata baada ya kufukuzwa mahusiano yetu yaliendelea kuwa Kama alipokuwepo kazini.

Shahidi: Wakati Mohamed Abdillahi Ling'wenya anafukuzwa kazi mwaka 2017 mimi nilikuwa kwenye kazi maalumu.

Shahidi: Nilifahamu baada ya kurudi kwenye kituo changu cha kazi nilipata taarifa kutoka kwa Admin Officer. Alinipatia taatifa hizo ofisini.

Mwendesha mashtaka anamuongoza shahidi kuwatambua washtakiwa kwa kuwaelezea kwa ufupi walivyo Kisha anaielekeza mahakama mmoja mmoja akianzia na Bwire, Kasekwa kisha Ling'wenya.

Wakati shahidi anaelezea kwa ufupi wasifu wao, mara kadhaa Kasekwa na Ling'wenya wananong'onezana na kutabasamu, lakini Bwire yuko kimya tu na kivyakevyake, hana ushirikiano na makomando wenzake japo walifanya kazi pamoja.

Shahidi: Askari hao ambao hawakuwa na cheo, majukumu yao yalikuwa ni kutekeleza majukumu ya kijeshi, wao ni watendaji.

Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling'wenya, wakati wa utumishi wao, Bwire alikuwa anaishi Ngerengere, Kasekwa Chalinze na Ling'wenya pia Chalinze.

Shahidi: Mwaka 2011 wakati nikiwa kwenye operesheni Darfur sikumbuki kama kuna niliyekuwa naye( Kati ya washtakiwa wasio na cheo).

Shahidi: Kwenye nyumba niliyokuwa naishi wakati niko Dafur nilikuwa naishi na viongozi wenzangu na hata mwaka 2019 nikiwa Sudan ya Kusini, wale wa cheo cha chini( private) sijawahi kuwa nao hata mmoja.

Shahidi: Freeman Aikael Mbowe nilifahamiana naye kutoka mwaka 2008 mpaka mwaka 2020.

Shahidi: Nakumbuka mwaka 2008 Freeman Aikael Mbowe alinipigia simu akaniita kwa majina yangu. Siwezi kukumbuka mwezi wala tarehe.

Shahidi: Simu yangu ilikuwa ya mtandao wa Voda 0754612518. Namba yake ilikuwa mtandao wa Airtel na hiyo namba sikumbuki.

Shahidi: Alinipigia simu akaniuliza wewe ndio Denis Urio nikasema ndio ni mimi akaniuliza askari wa Jeshi, nikasema ndio, akajitambulisha kuwa ni Freeman Aikael Mbowe. Nilikuwa namfahamu kwa sababu nilikuwa namuona kwenye vyombo vya habari hivyo alikuwa anafahahamika.

Shahidi: Akaniuliza profile yangu alikuwa ana-confirm, akanuliza wewe si wa Kilimanjaro nikamwambia ndio, akaniambia inabidi tufahamiane wewe ni ndugu yangu.

Shahidi: Sifahamu alikotoa namba yangu ya simu. Nilipomuuliza ulipata wapi namba yangu akaniambia ukitaka namba ya mtu kuipata siyo tatizo wewe unafahamika Sana. Aliniambia hivyo nilipotaka kujua alipata wapi namba yangu.

Shahidi: Alinitamkia maneno hayo wakati ule aliponipigia kwa mara ya kwanza.

Shahidi: Baada ya siku hiyo mawasiliano yetu yaliendelea. Alikuwa akinitumia ujumbe wa kuni-wish kama ni sikukuu au Kama ni event yoyote.

Shahidi: Mawasiliano yaliendelea mpaka mwaka 2012 ndipo tulipokuja kuonana ana kwa ana. Ilikuwa ni baada ya kurejea nchini kutoka Darfur Sudani mwezi wa 10/2011

Shahidi: Sikumbuki tarehe wala mwezi tuliyokutana.

Shahidi: Nakumbuka siku hiyo nilikuwa maeneo ya Mgulani Sabasaba, nikapokea simu kutoka kwa Freeman Aikael Mbowe, akaniuliza uko wapi nikamwambia niko Mgulani.

Shahidi: Nilimuelekeza location eneo nilikokuwa, akaniambia ana kitu cha muhimu anataka tuongee je tunaweza kuonana?

Shahidi: Nikamuuliza yeye tutaonana wapi?

Shahidi: Akaniambia njoo Mikocheni Casam Hotel.

Shahidi: Mimi nilimwambia sijui iliko na maeneo ya Mikocheni mimi sipafahamu, si mwenyeji

Shahidi: Akaniambia niende kituo cha teksi nimwambie dereva anipeleke Casam Hotel.

Shahidi: Nilienda kwenye kituo cha teksi nikamtafuta dereva anayejua hotel hiyo ilipo nikampata Basi tukaanza safari ya kwenda Casam Hotel.

Shahidi: Hicho kituo cha teksi nilichoenda ni cha Sabasaba kwa Aziz Ali Wilaya ya Temeke.

Shahidi: Nilenda nikafika Casam Hotel nikiwa kwenye teksi nikampigia simu kumwelezea kuwa nimeshafika.

Shahidi: Akanielekeza pale nikaenda mahali alikokuwa.

Shahidi: Wakati huo dereva teksi alikuaa anadai hela yake.

Shahidi: Akaniambia huyo anadai shilingi ngapi? Nikamwambia elfu 20.

Shahidi: Aliilipa elfu 20 gharama ya teksi alimpa mhudumu ndio akampelekea dereva teksi nauli yake.

Shahidi: Hayo yote yalitokea majira ya alasiri kuanzia saa 7 mpaka saa 9, yalikuwa majira ya mchana mchana.

Shahidi: Pale tulipokaa hapakuwa na mtu mwingine tofauti yangu mimi na yeye.

Shahidi: Baada ya kukutana alinieza mambo makubwa matatu, la kwanza akitaka kujua profile yangu, Mimi ni nani Nina elimu gani nafanya kazi gani ndio alikuwa ananiulizia.

Shahidi: Mimi nilimjibu kadri alivyoniuliza.

Shahidi: Akiniluza nina rank gani  nilimwambia Mimi sina rank (sina cheo chochote)

Shahidi:  Kazi nikamjibu nafanyia kazi Morogoro.

Shahidi: Lingine nililomjibu ni nyumbani nikamwambia nyumbani ni Kilimanjaro Wilaya ya Moshi Vijijini.

Shahidi: Hoja ya pili alitaka kujua msimamo wangu dhidi ya vyama vya upinzani.

Shahidi: Nilimjibu kwamba mimi taratibu za kazi yangu siruhusiwi kufungamana na chama chochote, ila kwa kiongozi akiyeko madarakani.

Shahidi: Hoja ya mwisho aliniuliza anahitaji makampuni ya kufunga mifumo ya mawasiliano kwenye ofisi zao Kama jeshini Kuna makampuni yanayofunga mifumo ya mawasiliano.

Shahidi: Nikamuuliza swali kwa nini unataka makampuni yaliyoko jeshini kufunga mifumo ya mawasiliano kwenye ofisi zako akasema anataka kufuatilia viongozi wanaotoa siri za chama chao.

Shahidi Luten Urio: Baada ya swali hilo nilimshauri aende kwenye taasisi za elimu ya juu atapata majibu hayo.

Shahidi Luten Urio: Baada ya hapo tuliachana akaagiza teksi ikaja pale akalipa hela nikaondoka. Sikujua kuwa alilipa kiasi gani.

Shahidi: Tuliachana majira  ya jioni, kuanzia saa tisa mpaka saa 11.

Shahidi: Baada ya kuachana nilirudi nyumbani.

Shahidi: Mawasiliano baina yetu yaliendele kama kawaida, ananipigia simu ananitumia ujumbe kuni-wish kama ni sikukuu.

Shahidi : Baada ya siku hiyo tulikutana tena mwaka 2020 mwezi wa 7 tarehe za katikati.

Shahidi : Nakumbuka ilikuwa mwezi wa 6 mwishoni kati ya tarehe 27 mpaka 30. Nilikuwa nimeacha simu kwenye gari, nikakuta namba ngeni imepigwa.

Shahidi : Nilikuta missed call zaidi ya tano, yaani simu ambazo zilipigwa hazikupokewa.

Shahidi: Namba haikuwa saved, ilikuwa ni namba ngeni kwenye simu yangu.

Shahidi: Kwanza nilihisi Kuna tatizo kwenye familia yangu nikapiga simu ya kwanza akapokea akajitambulisha ni mwenyekiti, akakata simu.

Shahidi: Nikapiga tena wewe ni nani akasema alikuwa anakutafuta mwenyekiti, akakata tena.

Shahidi: Baadaye ilipigwa tena simu kwa namba ambayo sijaisevu, nikamuuliza ni nani? Akasema ni kaka yako.  Nikamuuliza kaka yangu wa wapi akasema kaka yako wa Dodoma, nikamwambia mimi sina kaka Dodoma, nilipotaka kuachana naye akaniambia ni Freeman Mbowe.

Shahidi: Nikamsalimia akaniambia kuna mambo muhimu yakuongea na wewe nikamwambia niambie kwenye simu akasema nijitahidi tukaongee kuna mambo ya muhimu ya kuongea na mimi.

Shahidi: Nikasema sawa nikipata muda nitakuja Dar es Salaam.

Shahidi: Ilikuwa ni majira ya saa 10 jioni

Shahidi: Wakati huo Mimi nilikuwa niko likizo ya mwaka Morogoro.

Shahidi: Baada ya hapo tuliendelea kuwasiliana sasa akawa hatumii namba yake akawa anatumia namba tofauti.

Shahidi: Baada ya hapo nikawa nimekuja Dar kwa mambo ya kibinafsi ilikuwa mwezi wa 7. Majira ya saa 10 najiandaa niende Mgulani ndio nikakumbuka kuwa nilikuwa nimemuahidi kuwa nikija Dar es Salaam, Basi nikampigia simu haikupokelewa. Nikawa naenda stesheni wakati nasubiri daladala akanipigia simu mwenyewe Mbowe akaniambia nilikuwa busy ndio maana sikuweza kupokea simu.

Shahidi: Akaniuliza uko wapi? Nikamwambia niko stesheni nataka kwenda Mgulani, akaniambia Home Boy hatuwezi kukutana? Huwa anapenda kuniita homeboy.

Shahidi: Aliniambia naweza kumfuata Mikocheni nikamwambia Sasa hivi muda umeshaenda halafu siijui vizuri Mikocheni naweza nikapotea.

Shahidi: Akaniambia huwezi kupotea akaniambia angalia kwenye simu Kama Kuna bodaboda mpe simu nimuelekeze mahali akulete

Shahidi: Basi nikampa bodaboda simu akamuelekeza nikaondoka naye. Bodaboda nilimpata hapo hapo stendi.

Shahidi: Basi akampa maelekezo nikaondoka na huyo bodaboda kuelekea maeneo alikosema.

Shahidi: Tulienda mpaka kwenye mgahawa mmoja maeneo ya Mikocheni, ambao sikufahamu.

Shahidi: Kuna parking ya magari, bodaboda akasimama tukaenda mpaka kwenye mgahawa huo bodaboda akapaki pembeni ya magari hayo.

Shahidi: Nikampigia simu haikupokewa, wakati naendelea kupiga simu akaja kijana mmoja akaniuliza wewe ndiye Denis Urio?

Shahidi: Nikamwambia ndio Mimi. Akatoa elfu 19 akampa bodaboda, akaniambia kuwa Mwenyekiti yuko huku, nikamfuata yule kijana tukaenda mpaka alikokuwa Freeman Mbowe. Akafungua mlango akatoka nje.

Shahidi: Wakati huo ilikuwa ni majira ya saa moja kasoro, jua lilikuwa limeshazama japo kuwa kulikuwa bado na mwanga.

Shahidi: Wakati nampigia simu yeye akanipigia baadaye (kituoni stesheni) alitumia namba ambayo si ya kwake.

Shahidi: Nilipokutana naye nilipompigia simu nilikuwa na namba yake ya tigo na ya airtel.

Shahidi: Ndani hapakuwa na mtu mwingine, tulikuwa wawili tu mimi na yeye.

Shahidi: Nilipofika nilimkuta yuko peke yake anakunywa Red Bull akamuita muhudumu anisikilize na mimi nikaagiza Malta Guiness.

Shahidi: Tulisalimiana baada ya salamu akaniambia, Homeboy, mwaka huu wa 2020 kuna uchaguzi mkuu, hivyo chama changu kimepanga kuchukua dola kwa namna na kwa gharama yoyote ile.

Shahidi: Akaniambia wewe si unaona watu  wanyonge, watu wa chini wanavyoishi maisha ya shida? Homeboy tulifahamiana muda mrefu, tunatoka mkoa mmoja, pia wewe ni mchaga mwenzangu, tukichukua dola unafikiri wewe utakosa cheo cha juu jeshini?

Shahidi: Akaniambia hivyo, najua jeshini unafahamiana na watu waliostafu au kufukuzwa kazi ya Jeshi, wale ambao walifanya mafunzo maalumu ya ukomando, hivyo homeboy nakuomba unitafutie vijana hao wenye mafunzo maalumu ya ukomando ambao nitaambatana nao kwenye harakati za kuchukua dola.

Shahidi: Najua watakuwa na uwezo wa kunisaidia kuifanya nchi isitawalike, kuleta taharuki na kusiwe na amani.

Shahidi: Kwa hiyo tutafanya hayo kwa kufanya mambo haya, kulipua vituo vya mafuta, kuchoma moto masoko makubwa na kwenye mikusanyiko mikubwa ya watu, kukata miti mikubwa iliyoota pembezoni  mwa barabara zote zinazoingiza na kutoa magari hasa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Mwanza, Kilimanjaro especially mji wa Moshi na kwenye barabara ya Morogoro Iringa.

Shahidi: Kwa kufanya vitendo hivyo vitatu itapelekea watu kuwa na taharuki na kuandamana nchi nzima.

Shahidi: Ina maana yatakapofanyika matukio hayo watu wataandamana na mikoa mingine iliyobakia nayo itasapoti.

Shahidi: Pointi nyingine ya mwisho ni kuwadhuru viongozi wa Serikali ambao ni vikwazo kwenye vyama vya upinzani.

Shahidi: Hivyo homeboy nisaidie niwapate hao watu nina haraka sana nao, mwisho wa maelezo yake.

Shahidi: Alivyoniuliza hayo makusudio yake nilimkubalia nikamwambia nipe muda wa kutafakari.

Shahidi: Experience yangu kwa uzoefu wangu kwenye ulinzi (tactical appreciation) yaani kuna ubinadamu yaani kuna Mimi na Tanzania, Mimi si kitu kuliko Tanzania.

Shahidi: Nilifikiria Freeman Mbowe Ni ndugu yangu yeye ameshakuja na mawazo yake, nilitafakari kuwa nini effect ya hayo matukio lakini nikimkatalia atachukua hatua gani, nimesolve yasitokee matatizo ndio inakuja plan A na B, ili plan A iki-fail  natumia B nayo iki faille natumia alternative way

Shahidi: Hiyo tactical appreciation niliyoitumia ndio ikaniongoza kwamba nimkubalie kwamba nipe muda.

Shahidi: Hakuwa na nikomo cha watu aliwataka.

Shahidi: Baada ya kukubaliana tukaridhiana akaita teksi pale nikarudi Mgulani. Muda huo ilikuwa ni majira ya saa mbili saa tatu.

Shahidi: Huyo dereva teksi sijui alimlipa shilingi ngapi?

Shahidi: Baada ya kurudi Mgulani nilitaka nivumilie mpaka kukuche lakini nilishindwa kulimeza yaani kukaa nalo kwa sababu ya nature ya taarifa yaani kuleta taharuki.

Shahidi: Nilichukua hatua ya kumpigia simu DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai), Kamishna Robert Boaz.

Shahidi: Nikampa taarifa nilizopewa na Freeman Mbowe za mipango ya uvunjifu wa amani kwamba nimekutana naye akaniambia nimtafutie watu wa kuchoma vituo vya mafuta, nilipoanza kumueleza  hivyo akasema subiri, unaweza ukaja ofisini kwangu kesho, unielezee vizuri, nikasema ndio akasema basi uje ofisini kwangu kesho unielezee vizuri.

Shahidi: Namba yake ya simu (DCI) niliyompigia sijaikariri kichwani mwangu.

Shahidi: Aliniambi (DCI) niende ofisini kwake makao makuu ya Polisi maeneo ya Posta Dar es Salaam.

Shahidi: Alinitaka niende ofisini kwake majira ya asubuhi.

Shahidi: Baada ya kupambazuka asubuni nilichukua hatua ya kwenda makao makuu ya Polisi nikajitambulisha kuwa nina ahadi ya kuonana na DCI kisha nikapanda juu ofisini kwake DCO ghorofa ya 7.

Shahidi: Kabla ya siku hiyo kwenda kwa ofisi ya DCI nilishafika mara mbili, 2017 na 2014.

Shahidi: Nilipanda kwa ngazi mpaka ghorofa ya 7 kwa sababu lift hazifanyi kazi.

Shahidi: Nilijitambulisha kwa PS wake (katibu muhtasi) kuwa naitwa Lut. Denis Urio nina appointment na DCI, akaniambia nikae pembeni kwenye kochi akampigia (DCI), baada ya PS kufanya mawasiliano naye DCI aliniambia ingia utamkuta Msaidizi wake nikaingia nikaka kwenye makochi.

Shahidi: Baada ya muda kidogo yule PS wake akaja akaniambia niingie kwa DCI.

Shahidi: Nilipoingia ndani nikamkuta Afande DCI yuko peke yake nikamsalimia, nikajitambulisha  kuwa naitwa Luteni Denis Urio kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania, nikamkumbusha kuwa ndiye niliyekupigia.

Wakili Chavula: Mheshimiwa Jaji samahani, hivi sasa ni saa Saba kasoro dakika nne, na sisi makubaliano yetu ni kwamba ikifika saa Saba kamili tunapumzika na sisi bado tuna maswali mengi zaidi ya kumuuliza shahidi, ni hayo tu

Jaji: Difference:

Wakili Peter Kibatala (kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi): Nasi hatuna pingamizi Mheshimiwa Jaji

Jaji: Basi tunaahirisha kwa muda kwa health break, kwa dakika 45

Mahakama imerejea baada ya mapumziko ya muda mfupi, kwa ajili ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula kuendelea kumuongoza shahidi wa 12 lutein Denis Urio kutoa ushahidi.

Wakili wa Serikali Robert Kidando: Kolamu yetu iko vilevile haijabadilika na tuko tayari kuendelea.

Wakili wa utetezi Peter Kibatala: Na sisi Kolamu yetu iko vilevile na tuko tayari kuendelea.

Jaji: Shahidi nakukumbusha bado uko chini ya kiapo, utaendelea kutoa ushahidi wako

Shahidi Luteni Urio: Nilimkumbusha DCI kuwa mimi ndiye niliyekupigia simu kukujilisha suala la Mbowe lakumtafutia watu atakaoshirikiana nao katika harakati za kuchukua dola.

Shahidi: Wakati naendelea kumueleza alifanya mawasiliano kwa simu kisha akaja mtu akamsalimia Afande DCI.

Shahidi: Alimkaribisha na kumwambia akae ilikuwa baada ya kama dakika kumi, mtu huyo ilikuwa ni mara ya kwanza kuonana nae.

Shahidi: Nakumbuka Afande DCI alinitambulisha kwake kuwa anaitwa ASP Ramadhani Kingai.

Shahidi: Alinitaka nianze kusimulia tena upya, kwamba nilipigiwa simu na Freeman Mbowe akinitaka nikutane nae maeneo ya Mikocheni

Shahidi: Nilifanya hivyo na akanieleza yafuatayo kwamba mwaka huu kuna uchaguzi hivyo amedhamiria kuchukua dola kwa namna yoyote na kwa sababu anafahamiana na mimi muda mrefu wakichukua dola nitapata nafasi kubwa.

Shahidi: Hivyo akaniomba nimtafutie askari waliofukuzwa au kustafu ambao wamepitia mafunzo maalum ili waambatane nae katika harakati za kuchukua dola.

Shahidi: Wa kufanya matukio yatakayofanya nchi isiwe na amani, isitawalike kwa kufanya matendo haya kwa kulipua vituo vya mafuta katika majiji matano makubwa ambapo ni Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza Arusha na mji wa Moshi

Shahidi: Pia watachoma moto kwenye masoko makubwa na mikusanyiko ya watu kwenye majiji hayo.

Shahidi: Pia watakata miti mikubwa pembezoni mwa barabara zinazoingia na kutoka kwenye miji hiyo ili kusiwe na Mawasiliano.

Shahidi: Nikifanya matendo hayo wananchi wataona serikali imeshindwa kuongoza hivyo watatangaza maandamano makubwa na kuwaambi Serikali imeshindwa kusimamia usalama wao.

Shahidi: Pia alimueleza Kingai Mbowe alipanga kuwadhuru viongozi wa Serikali ambao ni kikwazo kwa vyama vya upinzani.

Shahidi: Baada ya kutoa taarifa hiyo DCI walianza kuteta na SP Kingai lakini sifahamu walichokuwa wanaongea.

Shahidi: Baada ya dakika kumi SP Kingai alitaka tupeane mawasiliano na DCI akanitaka kuendelea na utaratibu huo na kila hatua niripoti kwa SP Kingai.

Shahidi: Nisisite kufanya kile anachokitaka ili mradi nitoe taarifa, maelekezo mengine niliyopokea kutoka kwa DCI ni kwamba nikishawapata na kama huko kwa Mbowe kutakuwa na kitu chochote cha kihalifu ni mwambie.

Shahidi: Niliagana na DCI na kwenda kuendelea na shughuli zangu na kuanza mchakato wa kuwatafuta watu hao.

 Shahidi: Nlianza Kumtafuta mtu anaitwa Moses Lijenje nae alikuwa ni askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania aliyefukuzwa mwaka 2008 Kikosi cha 92 KJ.

Shahidi: Nilifahamiana nae toka mwaka 2003 hadi 2008, lakini alifukuzwa kwa utovu wa nidhamu.

Shahidi: Nilimtafuta wakati huo alikuwa anafanya kazi kwenye kampuni iliyokuwa inajenga reli ya kisasa kipande cha Morogoro Dodoma.

Shahidi: Nilimtafuta kwa njia ya simu na baada ya kupata nikamwambia kuna kazi ya ulinzi kwa Freeman Mbowe kama anaweza kufanya, nilipomwambia unaweza kufanya akasema yuko tayari kwa sababu amepunguzwa kazi kwa muda kutokana na ugonjwa wa corona.

Shahidi: Nilimwambia asubiri Freeman Mbowe akiwa tayari ntamjulisha baada ya hapo nilimtafuta Halfan Bwire namba alivyokuwa anatumia ilikuwa hapatikani nikamtafuata kwa njia ya meseji mesenja na nilipompata nikamwambia Freeman Mbowe anahitaji walinzi je yuko tayari akasema yuko tayari kufanya kazi kwa mujibu wa maelezo yake aliniambia anasafirisha Magari ya IT kwenda Tunduma, nikamwambia muda atakaohitajika nitamjulisha.

Shahidi: Baada ya siku chache Mbowe kanipigia simu akaniambia Home boy mbona mpaka sasa hivi kimya wale watu hujanitafuta?

Shahidi: Hapo ndipo nikajua yuko serious kinachotakiwa ni kutuma nauli ili waaweze kuja akaniuliza gharama zao nikamjibu ni Sh500,000.

Shahidi: Mawasiliano makubwa tulikuwa tukifanya kwa njia ya Telegram alikuwa hatumii njia ya kawaida kupiga kwenye simu.

Shahidi: Julai 20, 2020 tulianza kuwasiliana kwa kupigiana kwa njia ya Telegram njia ya kawaida alikuwa hapokei kabisa.

Shahidi: Baada ya kumwambia inahitajika Sh500,000 aliniambia nimpe namba ya kutuma nikampa namba yangu ya Airtel 0787555200 na baada ya kumpa namba alinitumia hiyo hela kupitia namba yake ya tigo 0719933386 ilikuwa ni tarehe 20/7,2020.

Shahidi: Fedha hiyo ilikuwa kwa ajili ya kupelekwa watu kwenda kufanya uhalifu.

Shahidi: Baada ya kupokea fedha hizo nilimfahamisha SP Ramadhani Kingai na tayari nimeshapata watu wawili akaniambia endelea watumie waende huko wanakotakiwa kwenda.

Shahidi: Nilimpigia Lijenje nikamwambia aje Morogoro kazi tayari, akasema anakuja mara moja ni kampigia na Bwire naye akasema anakuja.

Shahidi: Baada ya kuzipokea nilitoa Sh499,000 nilienda kukutana nao stendi ya Msamvu nikamwambia nyie ni askari mnakiapo na kiapo chenu hakijavunjwa, mnaenda kwa mwajiri wenu mkiona kama kuna matukio yoyote ya kihalifu yanaendelea mnifahamishe nikatoa Sh300, 000 nikawapa.

Shahidi: Baada ya hapo nikampigia Mbowe nikamwambia vijana wako tayari lakini nani anawapokea? akasema hamna shida nitawatumia namba ya dereva wangu Wile.  

Shahidi: Mawasiliano yote tulikuwa tukifanya kwa njia ya Telegram baadae nikaambiwa wameshafika kwa Freeman Mbowe.

Shahidi: Freeman Mbowe aliniambia bado wengine wawili nikafanya utaratibu wa kuwa pata hao wawili Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya ambao niliwapata kwa njia ya simu.  

Shahidi: Nilipompata Ling'wenya alimtafuta mwenzake Aadam Kasekwa ambapo nliikutana nao stendi ya Msamvu Morogoro mjini.

Shahidi: Kwanza nilipokutana nao nilimwambia Freeman Mbowe anataka askari walifanya mafunzo Maalum kwa ajili ya ulinzi wakasema wako tayari nikawaambia nina 199, 000 lakini nikawaambia mkiona kuna chochote kinachotokea cha uvunjifu wa amani mniambie.

Shahidi: Alinitumia fedha hizo kupitia Wakala kwenye namba yangu 0787555200 kisha akanijulisha kupitia mtandao wa telegram kuhakikisha kama nimepokea.

Shahidi: Niliwapa Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya fedha zao kisha wakaanza safari ya Morogoro kwenda Dar es Salaam nikamfahamisha Freeman Mbowe.

Shahidi: Baada ya kuwapata niliwaambia wanaenda kufanya kazi ya ulinzi kwa ajili ya kiusalama, niliifanya hivyo kwa ajili kuwa wale ni askari wanakiapo hivyo wangekuwa washaondolewa uaskari wao ningewaambi ukweli tungekuwa tumeharibu kile kilichopangwa.

Shahidi: Baada ya kundi la pili kuondoka tarehe 24, Freeman Mbowe alikata mawasiliano na mimi nikaonekana useless kila nikimpigia hapokei nikimtumia ujumbe hajibu.

Shahidi: Siku zilizofwata sikuwahi kuwasiliana na Kasekwa na sikuwahi kuwa na namba yake, Bwire alikuwa hapokei simu nikawa na wasiliana na Ling'wenya kwa njia ya whatsup kujua kuna nini wameambiwaa nini?

Shahidi: Majibu aliyopewa ni kwamba bosi wao Freeman Mbowe amewaahidi kuwaajiri na atakuwa anawalipa mshahara kila mwisho wa mwezi.

Shahidi: Baada ya kuwa namuuliza Ling'wenya kitu flani ananinjibu kingine nikawa nawasiliana na Hassan Bwire ingawa mara nyingi nilikuwa napigia kila siku.

Shahidi: Julai tarehe za mwisho Bwire aliniambia yuko Dar es Salaam lakini anatakiwa kwenda Moshi kuna kazi ya kwenda kufanya atamwambia .

Shahidi: Baada ya muda nikaona kimya Agost 4, 2020 nikampigia simu tena tukasalimiana akaniambia broo samahani sijakutafuta kama ulivyotuelekeza kwa sababu nimepitiwa.

Shahidi: Kazi ya ulinzi tuliyokuwa tunakuja kuifanya imebadilika sio hiyo, Freeman Mbowe ametushawishi kufanya kazi nyingine hivi tunavyoongea wale madongo (Lijenje, Kasekwa na Ling'wenya) wako moshi sasa hivi wamepewa kazi ya kushambulia Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Shahidi: Kabla ya tarehe Agosti 7,2020 wanatakiwa wawe wamerudi Dar es Salaam kwa vile tarehe 12, 8, 2020 kuna kazi nyingine ya kulipua vituo vya mafuta.

Shahidi: Baada ya taarifa hiyo nlimwambia aendelee kuwasiliana na mimi.

Shahidi: Nikimpigia SP Ramadhani Kingai nikamwambia taarifa nilizozipata Mose Lijenje, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya wako moshi wamepewa jukumu na Freeman Mbowe la kushambulia mkuu wa Wilaya ya Hai hivi sasa wanatembelea maeneo ambayo Sabaya anapenda kuyatembelea kati ya Moshi na Arusha.

Shahidi: Agost 4,2020 Nilipoongea na Halfan Bwire ndiye aliyenipa taarifa hizo.

Shahidi: Baada ya kumaliza kumpa taarifa aliniambia anashukuru kwa taarifa Agosti 5,2020 nilipompigia Bwire aliniambia wale madogo wamekamatwa.

Shahidi: Mohamed Ling’wenya na Adam Kasekwa ndio waliokamatwa ni kamuuliza bosi wenu anafahamu? Baada ya hapo nikampigia Freeman Mbowe hakupokea kwani tangu Julai 24, alikata mawasiliano na mimi.

Shahidi: Baadae nilikuta ujumbe wake kwenye account yangu ya Telegram ilikuwa Agost 6,2020 unaosema

"Nimeshindwa kupokea simu yako ya kawaida kwa sababu ya........ najua umenielewa? Any news"

Shahidi: Baada ya hapo sikuhangaika nae Bwire alinipigia simu Agost 6 na 7 kwa hiyo sikutaka kuongea nae tena kwa kuwa Lengo lilikuwa limeshatimia.

Shahidi: Agosti 10,2020 SP Ramadhani Kingai alinipigia simu alinitaka kesho kwenda Makao Makuu ya Jeshi la polisi yaliyopo posta mpya, kukutana na Afisa anaitwa Inspekta Swilla, wakati huo nlikuwepo Morogoro  

Shahidi: Nilichukua hatua ya kutoka Morogoro kuja Dar es Salaam siku hiyo kwa ajili ya kuonana na Inspekta Swilla Agost 11,2020 

Shahidi: Kesho yake nilifika nikafuata taratibu zote ikiwemo kujitambulisha, njlimpigia simu akaja kunifuata nikapanda nae juu gorofa ya nane kwenye ofisi yake.  

Shahidi: Lifti ilikuwa mbovu tukapanda kwa kutumia ngazi, Baada ya kufika gorofa ya nane alinikaribisha na kunieleza kuwa amepewa maelekezo anichukue maelezo ya matukio yote.  

Shahidi: Nilikubali kisha akaanza kunichukua maelezo ya washtakiwa hawa kuhusiana na kilichojiri.

Shahidi: Alinichukua maelezo kisha nikasaini, akaniomba nimuachie simu niliyokuwa nafanya nayo Mawasiliano na Freeman Mbowe pamoja na Halfan Bwire kwa ajili ya uchunguzi .

Shahidi: Nilimwambia nilikuwa nafanya Mawasiliano na simu zangu zote akanitaka nimuachie

Shahidi: Nilikuwa nikitumia mtandao wa Airtel, Vodacom, Hallotel na Tigo kwa Tanzania kwa kuwa kulikuwa na laini nilizokuwa natumia Sudan MTN na ZAIN.

Shahidi: Nilipotakiwa kuziacha nilitoa laini ya Voda kwenye simu ya tecno  nikaweka kwenye Sumsung ya tochi nikamwambia tarehe 12 ntamletea nyingine.  

Shahidi: Alichukua na kunakili IMEI namba kwenye nyaraka na kusaini akanipa na mimi nisaini kisha akanipa nakala.

Shahidi: Hiyo nyaraka nikiiona naweza kutambua kwa kuwa ina sahihi yangu, nyaraka halisi ilibaki kwa Inspekta Swilla.

Shahidi: Niliondoka na kurudi Morogoro siku hiyo hiyo na kesho yake nilimletea simu nyingine tatu.

Shahidi: Taraehe 12,8,2020 Nilienda kuleta simu tatu ambazo ni Tecno C9, Itel na sumsung ya tochi na kuzipeleka makao Makuu ya Jeshi la polisi kwenye Ofisi ya DCI kwa Inspekta Swilla.

Wakili Chavula: Mheshimiwa Jaji tukitazama muda ni saa 11 kasoro dakika kumi na kwa utaratibu saa 11:00 ndio mwisho na bado tuna maswali kwa shahidi ikikupendeza naomba tuahirishe hadi kesho Tarehe 27 kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji.

Wakili wa utetezi Peter Kibatala: Hatuna pingamizi Mheshimiwa

Jaji: Kufuatia maombi yaliyoletwa na upande wa mashtaka na kuungwa mkono na upande wa utetezi naahirisha shauri hili hadi kesho siku Alhamisi Januari 27,2020 kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji saa 3:00 asubuhi.