Mabeyo asimulia kabla, baada kifo cha Magufuli

Mkuu wa Majeshi Mstaafu wa Tanzania, Jenerali Mstaafu, Venance Mabeyo. Picha na Maktaba

Muktasari:

  •  Miaka mitatu imepita tangu kifo cha John Magufuli, akiwa madarakani katika historia ya Tanzania

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Tanzania (CDF), Jenerali mstaafu Venance Mabeyo, amesimulia kilichotokea kabla ya kifo cha Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli huku akiweka wazi ugumu uliokuwepo kabla ya kumuapisha Samia Suluhu Hassan kuwa Rais.

Mabeyo amesema ugumu uliokuwepo ulisababisha zaidi ya saa 48 kupita kabla Rais mwingine hajaapishwa kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kutokana na kuwepo kwa pande mbili zilizotofautiana kimaamuzi.

Jenerali Mabeyo amesema hayo wakati akizungumza katika mahojiano maalumu na Daily News Digital, katika kumbukumbu ya kifo cha Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021, katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Leo Machi 17, 2024, Hayati Magufuli amefikisha miaka mitatu. Aliongoza Tanzania kwa miaka takribani sita kuanzia Novemba 5, 2015 hadi mauti yalipomfika.

Kwa mara ya kwanza tangu astaafu wadhifa wake Juni 2022, Mabeyo amesimulia saa 24 za kabla ya Magufuli kuaga dunia na saa 40 kabla ya Samia Suluhu Hassan kuapishwa kuwa Rais wa awamu ya sita.

Mabeyo amesema wakati Magufuli anaugua, wao walishirikishwa kama vyombo vya ulinzi na usalama wajue hali ya Rais inakwendaje na wakati wote walikuwa wanakwenda kumuona, asubuhi na jioni.

Hivyo walikuwa na nafasi yao kama wakuu wa vyombo, akiwa kama mwenyekiti wao walikuwa wanashauriana wanafanyaje.

“Baadaye tukampeleka Mzena, pale palikuwa na utulivu si watu wengi wanaweza kuingia pale ni wachache na tukadhibiti watu ili awe na nafasi ya kupumzika vizuri, matibabu yakahamia pale na madaktari wote wakapelekwa pale kumhudumia wakati wote,” anasimulia katika sehemu ya mahojiano hayo ya dakika 19.11.


Kabla ya kifo chake

"Siku moja kabla ya kifo chake hali ilibadilika kidogo na yeye alijitambua kwamba hali imebadilika na nadhani alijua Mwenyezi Mungu alimuongoza kwamba hatapona, alichosema nirudisheni nyumbani. Nikafie nyumbani. Nikasema mheshimiwa hapana hapa upo kwenye mikono salama, madaktari wapo waendelee kukutibu.

"Niseme jambo moja ambalo halikuwahi kusemwa huko nyuma kwa sababu nilikuwepo pale aliniita CDF (Mkuu wa Majeshi) njoo, akaniambia siwezi kupona, waamuru hawa madaktari wanirudishe nyumbani.

“Nikamwambia mheshimiwa sina mamlaka hayo, akasema “yaani CDF unashindwa kuwaamuru madaktari wanirudishe nyumbani?,” nikamwambia suala la afya siyo la CDF mheshimiwa naomba ubaki utulie, madaktari watatuambia."

Mabeyo amesema alipoona amekuwa na msimamo huo, akamwambia “niitieni paroko wangu.”

 Paroko wa St Peters alikuwa anaitwa Father Makubi, lakini akaongeza akasema namuomba Kardinali (Polycarp) Pengo naye aje na kwa wakati huo ilikuwa ni asubuhi.

“Tukamtafuta Pengo alikuwa kwenye ibada hakupokea, akaniuliza “CDF haujampata Pengo?,” nikamwambia yuko kwenye ibada, baba atakapotoka atakuja nimeshampelekea na dereva wa kwenda kumchukua, akanyamaza.”

“Kwa hiyo wakaja wote Kardinali Pengo na Father Makubi wameongozana, sasa katika taratibu za kikatoliki wanamsalia ibada na kumpa sakramenti ya upako wa magonjwa aliyekuwa katika hatari ya kufariki," amesema.

Amesimulia walipomaliza kumsalia akapumzika lakini ilipofika saa nane mchana, walipigiwa simu na watu wa hospitali.

“Wakanipigia mimi kama Mkuu wa Majeshi, wakampigia DGS (Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa) na (Inspekta Jenerali wa Polisi) IGP wakatuambia hali ya mheshimiwa siyo nzuri sana hebu njooni, tukaenda kule tukamkuta ametulia, lakini alikuwa hawezi kuongea tena.

“Tukawaita madaktari wengine, nakumbuka tulimuita Profesa (Lawrence ) Maseru, Profesa (Mohamed) Janabi alikuwepo muda wote kwa hiyo yule aliongezea nguvu yule wakajaribu kumuangalia, tukaendelea kukaa mpaka jioni, ikafika jioni saa kumi na mbili na nusu hivi au saa moja kasoro akakata roho, tukiwepo wakuu wa ulinzi wa vyombo watatu mimi (CDF), IGP na DGS," amesimulia Mabeyo.

IGP wa wakati huo alikuwa Simon Sirro kwa sasa ni Balozi mpya wa Tanzania nchini Zimbabwe. DGS alikuwa Diwani Athuman.


Ugumu kutangaza taarifa

Mabeyo amesema kwa kuwa ilikuwa ni mara ya kwanza Rais wa nchi kufia madarakani ilikuwa ni changamoto kubwa. Swali walilojiuliza ni nani wa kumtaarifu wa kwanza.

Amesema wakati huo Makamu wa Rais, (Samia Suluhu Hassan) hakuwepo alikuwa Tanga, Waziri Mkuu hakuwa Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi (Dk Bashiru Ally) naye hakuwepo Dar es Salaam alikuwa Dodoma, hivyo ni viongozi watatu pekee wa kijeshi ndiyo waliokuwepo Dar es Salaam.

“Tukasema kwakuwa Makamu wa Rais yuko Tanga hebu tumwambie kwanza, tukawaambia Katibu Mkuu Kiongozi na Waziri Mkuu waje bila kupepesa maneno. Bahati nzuri wakaja mapema.

“Sasa mimi kama mwenyekiti wa wakuu wa vyombo natakiwa kusema kwamba mhemishiwa Rais ameshatutoka, kwa hiyo tukaanza kushauriana unafanyaje na nani anatakiwa atangaze hizi habari kwenye vyombo vya habari wananchi wajue.

“Ndiyo tukaanza kutafuta katiba sasa inasema nini (akacheka kidogo) sasa mtu pekee anayeweza kutangaza kwenye vyombo vya habari ni Makamu wa Rais, yeye yupo Tanga tunamwambiaje?

“Tunampigia simu au tunamwambia aje. Lakini sasa ikabidi yafanyike mawasiliano mengine kumweleza akiwa Tanga, lakini kabla ya kutangaza tukasema familia yake haijui, mke wake yupo hapa Ikulu hajajua, mama yake anaumwa yupo Chato hajaambiwa,” anasimulia.

Mabeyo amesema waliona hawawezi kumwambia kwa simu hivyo ilibidi wateue nani anakwenda kumweleza mke wa Rais wakiwaza ataipokeaje, pia wakaandaa utaratibu mwingine kwenda Chato wakatafuta ndege ndogo kabla ya kutangaza kwenye vyombo vya habari ili wawe wamepata taarifa.

“Wasipate taarifa kupitia vyombo vya habari, watu wakaenda Chato na ndege tayari usiku na ndiyo maana unaona suala la kutangaza kwenye vyombo vya habari lilichukua muda mrefu mpaka saa 5 usiku ilipokuja kutangazwa na Makamu wa Rais tayari familia ilikuwa na taarifa,” amesema.


Kutangazwa Rais

Mabeyo amesema suala la kutangazwa msiba lilikuwa moja, lakini kazi kubwa ilikuwa namna ya kumuapisha Rais, kwani kulikuwa na mawazo ya aina mbili kuna wanaosema Rais aapishwe baada ya kuzikwa au aapishwe kabla ya kuzika.

Amesema kulikuwa na mjadala mkubwa lakini ‘logic’ ikaja kwamba kuna marais wengine watatoka nje ya nchi kuja kumzika mwenzao, watapokelewa na makamu wa Rais au Rais, lazima awepo Rais.

“Ndiyo maana tukapokea maamuzi kwamba lazima makamu wa Rais aapishwe kama Rais. Ndiyo maana ilipita siku mbili, kikatiba hairuhusiwi inatakiwa kabla ya saa 24 awe ameshaapishwa Rais mwingine, sasa ilipita tarehe 17, 18 mpaka tarehe 19 ndiyo akaja kuapishwa kulikuwa na majadiliano hapo lakini tunamshkuru Mungu likapita, lakini namna ya kumuapisha nako ulikuwa mjadala tunamuapishaje.

“Lakini wakasema isiwe sherehe, wengine wanasema iwepo. Kama Mkuu wa Majeshi nikasema paredi lazima iwepo, bendera ya Amiri Jeshi Mkuu lazima ipandishwe kwa gwaride. Lakini kidogo kulikuwa na kamvutano tupo kwenye msiba lakini paredi iwepo kwanini.

“Nikasema huyu ni Amiri Jeshi Mkuu anayeapishwa, asipoapishwa kwa taratibu hizo za kitaifa Jeshi halitamtambua.


Amiri Jeshi Mkuu, Amirat Jeshi Mkuu

Miongoni mwa mabo yaliyoibuka kabla ya Rais Samia kuapishwa ni pamoja na jinsi yake, ambayo ilizua maswali huku wengine wakisema ataitwa Amirat Jeshi Mkuu, suala ambalo Mabeyo alilikataa.

“Sisi tuliwaambia jeshini hatuna mwanamke, yaani hatuwatambui kama mwanamume au mwanamke hapana na ndiyo maana jeshini tuna ofisa na askari hakuna mwanamume na mwanamke kwa hiyo hata Amiri Jeshi litabaki vile vile ni Commender in Chief.

“Hilo Amirat ni la kidini (anacheka kidogo Mabeyo) suala hilo lilikuja kutokana na nchi zinazotawaliwa kidini wao ni sawa lakini kwetu sisi ni hapana. Tuliwauliza Bakita mnasemaje Amirat maana yake ni nini, wakaeleza vizuri nikasema sawa tuendelee palepale na mimi nikasema siku ile wakati nimetoa hotuba yangu kwamba watu walikuwa na mjadala Amirat ni kasema hapana ni Amiri Jeshi Mkuu,” amesimulia.


Utekelezaji

Kutoka hapo Mabeyo amesimulia namna alivyoanza kufanya kazi na Rais Samia kwani wakati huo alikuwa akifanya kazi zaidi na Magufuli.

“Lakini yeye alipoteuliwa kuwa mgombea wa CCM Magufuli alimteua Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza, nafasi ya Makamu wa Rais inaeleweka. Baada ya Rais kuwa Magufuli na kwa mujibu wa Katiba yetu inaonyesha Rais ndiyo mtendaji siyo sawa na nchi zingine mwenye Mamlaka ni Rais, Makamu anamsaidia, anakuja mtendaji wa Serikali ni Waziri Mkuu na wengine wanajipanga Mawaziri na Wakuu wa Mikoa,”amesema Mabeyo.

Mabeyo amesimulia kuwa wakati ule Samia akiwa Makamu wa Rais, waliendelea kushirikiana vizuri maana Rais alikuwa Amiri Jeshi Mkuu moja kwa moja, mara chache sana aliwasiliana na Makamu wa Rais.

Amesema alimuona Makamu kama kuna hitaji jingine la kiutendaji ambalo hawezi kulitoa moja kwa moja kwa Amiri Jeshi Mkuu.

“Hilo mimi ndiyo nalijua tulikuwa tunaendelea vizuri akielekezwa akatekeleze jambo fulani anaenda na anakumbuka, wakati tunaanzisha Jeshi Usu, ilitengenezwa sheria ya kuanzisha na wakati wa uzinduzi Makamu alikuja na tulizindua Rasmi na mimi nilikuwa CDF, ilinibidi niongoze kuhakikisha Makamu wa Rais anazindua,”amesema Mabeyo.

“ Serikali ilikuwa vizuri na sisi anakumbuka kwa kuwa kulikuwa na kazi nyingi zinafanyika na hasa ujenzi wa wizara wakati wa kuhamisha makao makuu kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, wakati Rais Magufuli anaingia madakarani na baadaye yeye alikuwa CDF.

“Samia ameingia madarakani kutokana na tukio la Rais alikuyekuwa madarakani kufariki ni hali ambayo hatujawahi kupitia Tanzania, haijawahi kutokea lakini tunamshukuru Mungu mabadiliko yalikwenda vizuri. Lakini kutokana na Katiba bahati nzuri imeelezwa vizuri endapo Rais atafariki au atashindwa kutekeleza majukumu yake kama Rais atakayeshika madaraka ni Makamu wa Rais.

“Sasa Katiba walikuwa wameisahau kidogo ikatokea maongezi tofauti na nini lakini tukasema tuna taratibu tukizifuata haitakuwa shida, tuzizingatie zile nadhani ndipo alipokuja Rais Samia kwa utaratibu mzuri,” amesema.


Utendaji wa Samia

Akielezea utendaji wa Rais Samia kwa sasa, Mabeyo ameutaja kuwa ni mzuri sana, na kwamba mara nyingine wanaoshauri labda wanakosea lakini wanarekebisha kwa kushauriana.

“Lakini anashirikisha watu wengi maamuzi yake, anashirikisha wengi katika taasisi, kitaaluma, kwa mfano hata alipoanzisha Royal Tour alishirikisha watu akasema hapa tuondoke tulikuwa na kipindi kigumu cha Uviko-19, hali ya mapato ilikuwa imeshuka lakini alisema mapato mengi yanayoshuka ni kutokana na  watalii kupungua, lakini ni kulijenga Taifa letu liweze kuheshimika ndiyo akaanzisha hiyo Royal Tour na naamaini anaendelea kusikiliza ushauri,” amesema.

“Rais Samia hawezi kutekeleza jambo bila kutushirikisha na hata nilipokuwa bado Mkuu wa Majeshi alikuwa anasema CDF kuna jambo kama hili tunalifanyaje, namwambia mheshimiwa Rais nashauri iwe hivi na hivi anasema lakini kuna watu wamenishauri iwe hivi, namuuliza waliokwambia ni wanajeshi au siyo wanajeshi? Ni wanasiasa au watendaji, sasa ukimpa uchambuzi anafikia maamuzi.”