Mabilioni ‘yayeyuka’ upatu mpya

Wawekezaji katika kampuni hiyo, Charles Kapongo (kushoto) na Joseph Missana (kulia) wakizungumza katika mkutanona waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Sunday

Dar es Salaam. Watu wanaotajwa zaidi ya 300 hawajui hatima ya mamilioni yao ya shilingi walizowekeza katika kampuni ya Bestway Capital Management (BCM), na sasa wanamwangukia Rais Samia Suluhu Hassan, wakiomba aingilie kati ili waweze kupata fedha zao.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Charles Kapongo, ambaye ni mmoja wa watu wasiojua hatima yao, alidai kuwekeza mamilioni ya fedha (bila kutaja kiasi) katika kampuni hiyo huku akiahidiwa atapewa faidi ya asilimia sita kwa mwezi, lakini alipewa faida ya miezi minane tu na sasa yapata zaidi ya mwaka hajapewa tena, wala hajui hatima ya fedha zake alizoweka kama mtaji.

“Watu wengi tumeweka hela zetu katika kampuni hiyo na kwa wale ninaowafahamu asilimia 80 ni wazee, wastaafu kwa kuwa tulikuwa tukiambiana juu ya fursa hiyo, lakini ni kama tumelizwa sasa. Wengine ni watu wenye majina makubwa na wafanyabiashara maarufu; hawawezi tu kujitokeza hapa lakini hao vijana wametupiga pesa nyingi,” alidai.

Kapongo alisema yeye alijiunga na kampuni hiyo mwaka 2020 na kwa miezi sita ya mwanzo mambo yalikwenda vizuri lakini baadaye mambo yakabadilika, malipo yakaanza kuchelewa na wasiwasi ukatanda miongoni mwa wawekezaji. Uongozi ulichukua hatua ya kuita mkutano wa wawekezaji kuwaeleza mipango mipya lakini haikuleta nafuu yoyote.

“Kiingilio cha uwekezaji katika kampuni hiyo ni Sh23milioni na kuna watu wameweka hadi zaidi ya Sh1bilioni, kilio ni kikubwa mimi na watsaafu wenzangu tumejaribu kutafuta suluhu bila mafanikio kwa kuwa mkurugenzi sasa hivi hatumpati kwa simu taarifa zilizopo ni kuwa amekimbilia Dubai,” alidai Kapongo.


Alichokisema mkurugenzi

Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Steven Ndaula alisema yeye kama mkuu wa kampuni hiyo, amekuwa akiwasiliana na wateja mara kwa mara kwa barua na mikutano tangu kampuni yake ianze kukumbwa na mdororo na kwa mujibu wa taarifa yake, kampuni inapambana kuona namna inavyoweza kuwalipa wawekezaji wake ndani ya miaka mitatu kuanzia sasa.

Hata hivyo, alisema hali hiyo itatokana na faida itakayozalishwa huku akieleza mdororo uliojitokeza ulitokana na kupungua kwa thamani za sarafu za kimtandao hususani bitcoin kwa asilimia 78 na kampuni hiyo ilikuwa imewekeza kiasi kikubwa cha fedha katika biashara hiyo.

“Tumeona kuimarika kwa sarafu mtandaoni kwa siku za hivi karibuni, lakini tunasikitika kuwa hakutakuwa na malipo kwa robo ya kwanza ya mwaka lakini tuna matumaini na robo ya pili ya mwaka huu (Aprili Juni na Julai) kuwa tunaweza kupata mafanikio zaidi kwa kuzingatia kuwa tuna mradi mpya wa kibunifu tunatarajia kuuzindua Dubai tarehe 3 na 4 ya mwezi Mei,” alisema Ndaula.

Alipotafutwa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani Christina Mwangosi, alisema masuala kama hayo ni ya kipolisi ya yanaripotiwa kwa wingi, hivyo ni vigumu kujua tukio mahususi na kushauri mtu sahihi wa kuulizwa ni Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime, ambaye naye alipoulizwa alisema yupo kikaoni atafutwe wakati mwingine.


Undani wa kampuni

Kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) BCM ilisajiliwa Aprili 7, 2019 na inamilikiwa na watu 24.

Kati yao watatu ndiyo wenye hisa nyingi kuliko wengine na wamesajiliwa kama wakurugenzi.

Ndaula ndiye mwenye hisa nyingi zaidi wa kampuni hiyo iliyokuwa na ofisi zake za kisasa katika jengo la The Luminary Masaki, jijini Dar es Salaam ikijihusisha na masuala ya mitaji, ubadilishaji wa sarafu za kimtandao, hati fungani, hisa na masuala ya makazi ikiwa na dira ya kuwa kampuni ya uwekezaji ambayo ni chaguo la watu.


Kilio cha waliowekeza fedha

Kapongo, alisema baada ya wawekezaji kuona hamna mawasiliano ya moja kwa moja na mkurugenzi na malipo hayatolewi kama inavyotakiwa, walitoa taarifa kituo cha polisi, ubalozi wa Tanzania uliopo Falme za Kiarabu na Wizara ya Mambo ya ndani kitengo kinachohusika na makosa ya utakatishaji wa fedha, lakini mpaka sasa hawajapata utatuzi wa jambo lao.

“Dalili ya mvua ni mawingu, binafsi nilipoona mazungumzo ya fedha yameanza kusuasua na sipati faidi yangu kama awali na hata mawasiliano na mkurugenzi yanakuwa ya tabu, niliomba kuchukua mtaji wangu, lakini niliwasilisha maombi hayo mara kadhaa bila mafanikio. Zaidi mkurugenzi alinisihi niwe mtulivu mambo yatakwenda vizuri siku zijazo,” alisema.

Mwekezaji mwingine ni Joseph Missana aliyeweka zaidi ya Sh300 milioni, alisema imani yake ni kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa Serikali ina mkono hivyo inaweza kufanikisha wao kupata stahiki zao hususani mitaji yao walioiweka wakitarajia kupata faida.

“Mimi nilitumia pensheni nikaweka fedha awamu ya kwanza milioni 86 baadaye nikaongeza hadi kufikia Sh300milioni kwa kutumia vyanzo vingine, nilipata gawio langu miezi sita tu ambazo ni kama Sh30milioni baada ya hapo mambo yakabadilika, mkurugenzi haonekani ofisini, gawio halipatikani miezi inapita hadi mitatu ni barua tu za kututaarifu kuwa fedha itachelewa,” alisema.

Alisema watu wengi waliweka fedha nyingi na kwamba yeye alikutana na kampuni hiyo akiwa amestaafu, akitafuta ni wapi ataweka fedha zake ili zimsaidie kuendesha maisha.

‘‘Wengi wameweka fedha nyingi kuliko hata mimi hususani wastaafu, maana tulikuwa tukiambiana”.

Alisema kampuni hiyo ina usajili kamili wa Brella na ilikuwa ikilipa kodi kwa kila miamala iliyokuwa ikiifanya na kwa kuzingatia kampuni ilikuwa na ofisi, anuani ya kudumu na mipango yao ya kibiashara, ilikuwa ni rahisi kwa yeyote kuwaamini.

Mwekezaji mwingine alidai kampuni hiyo ilikuwa ikitumia watu wenye ushawishi kushawishi watu wengi zaidi kujiunga, akisema yeye alijiunga kwa sababu mchungaji wake alimsihi kujiunga na wengi walijiunga kwa kushawishiwa na mipango ya kampuni hiyo.


Mchungaji KKKT apigwa 200 milioni

Katika orodha ya wakurugenzi watano wa kampuni hiyo wanaosimamia idara mbambali, yupo Mchungaji wa Kanisa la KKKT Kimara Korogwe Joseph Maseghe, anayesimamia mahusiano ya kampuni hiyo.

Anadaiwa kuwaingiza wawekezaji wengi katika kampuni hiyo, huku akisema BCM ni kampuni ya kitapeli iliyokimbia na fedha za watu.

“Mimi niliandikwa tu sina cheo chochote wala sikuwahi kupokea malipo yoyote kwa nafasi ninayotajwa nayo. Baada ya kujua mimi ni mchungaji wakawa wanatumia jina langu kutangaza biashara yao, walikuwa wakitumia viongozi wa dini na wanasiasa kutangaza biashara yao. Binafsi nimepoteza Sh200 milioni na sijapata chochote,” alisema.

Mchungaji Maseghe alisema katika kampuni hiyo yeye ni mwekezaji tu na aliuza shamba na kutumia vyanzo vyake vingine vya mapato ili kupata hiyo Sh200 milioni aliyowekeza lakini sasa hivi anasikia kuwa mkurugenzi wa kampuni hiyo amekimbilia Falme za Kiarabu.

Katika taarifa ya usajili ya Brela Mchungaji Maseghe anatajwa kama miongoni mwa wamiliki wa kampuni hiyo kwa hisa 139, hata hivyo alilieleza Mwananchi kuwa hisa hizo ni za uwekezaji wala sio za umiliki wa kampuni hiyo, huku akiwataka wananchi kujiepusha na kampuni kama hiyo zinazokuja kwa mgongo wa kutaka kuwapa watu faida.

“Ni bora mtu uwekeze kwenye soko la hisa, hati fungani, UTT au kwingine lakini sio kampuni kama hizi, ‘‘alisema. za watu binafsi,” alisema Maseghe.