Machinjio Vingunguti na hali halisi ilivyo-3

Muktasari:
- Nje kidogo ya lango kuu la kuingilia ndani ya machinjio utapishana na watu wengi wa kila rika, hasa nyakati za alfajiri, kwani baadhi ya watu huwa katika harakati za kwenda kazini na wengine hukimbilia hapa kujipatia mahitaji yao ya kitoweo.
Dar es Salaam. Nje kidogo ya lango kuu la kuingilia ndani ya machinjio utapishana na watu wengi wa kila rika, hasa nyakati za alfajiri, kwani baadhi ya watu huwa katika harakati za kwenda kazini na wengine hukimbilia hapa kujipatia mahitaji yao ya kitoweo.
Unapoingia ndani ya lango hilo utakutana na umati wa watu. Ni vigumu hata kukisia idadi yao. Wengi wakiwa wabeba mapande ya nyama kwenye mifuko au vyombo vya plastiki kama ndoo.
Kwa wale wanye usafiri hufika na magari yao ili kuwarahisishia usafiri wakati wa kurejea walipotoka. Asilimia kubwa wakiwa ni wafanyabiashara wa nyama katika mabucha mbalimbali mjini pamoja na wafanyabiashara wanaojishughulisha na uuzaji wa vyakula.
Nazidi kuingia ndani kwenye machinjio. Chini kwenye sakafu kumetapakaa damu, harufu kali inayosababishwa na shughuli za uchinjaji.
Huku nako nakutana na wauza nyama pamoja na wachinjaji wakiwa wamevalia makoti meupe yenye madoa ya damu kutokana na shughuli za uchinjaji na ubebaji wa nyama kutoka sehemu moja hadi nyingine mithili ya madaktari.
Nyama hizo hutolewa ndani ya machinjio na kuwekwa nje ambako hutundikwa kabla ya kuuzwa kwa mamia ya wateja wanaofika hapa kila siku.
Nakutana na mwanamke mmoja anayejitambulisha kwa jina la Shukuru Ezekieli, ambaye anajishugulisha na uuzaji wa nyama ya n’gombe na mbuzi anayesema wanyama wanaochinjwa katika machinjio hayo wengi hununuliwa kutoka mnada wa Pugu.
Pembeni ya machinjio hayo nakutana na jengo jipya la kisasa ambalo limebeba matumaini makubwa kwa wakazi wa eneo la Vingunguti ambalo hata hivyo, ujenzi wake bado haujakamilika ili kuipa jamii hiyo machinjio ya kisasa.
Haya ni machinjio mapya ya kisasa yanayotarajiwa kuanza kufanya kazi hivi karibuni, ujenzi wake ukikamilika.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofanya ziara katika eneo hilo Mei 17, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri alisema machinjio hayo mapya yatakapoanza kufanya kazi yataongeza ufanisi katika shughuli za uchinjaji na kuboresha mazao yatokanayo na wanyama wachinjwao, kwani kutakuwa na mashine za kisasa.
“Machinjio haya ya kisasa yatakapoanza kufanya kazi yataongeza thamani ya nyama na vitu vingine vitokanavyo na wanyama wachinjwao hapa, hivyo kuongezeka kwa soko la ndani na nje ya nchi,” alisema Shauri.
Pia yatawezesha ajira zaidi ya 3,000 hivyo kupunguza idadi ya vijana wasio na ajira mtaani ambao watachangia uchumi wa Taifa.
Usalama wa eneo
Veronica Yohana, ambaye ni kati ya wakazi wa eneo hilo anasema matukio ya wizi yameanza kurudi kwa kasi, hasa nyakati za asubuhi na usiku ukilinganisha na kipindi cha nyuma kidogo ambapo yalipungua kabisa.
“Wizi kwa kipindi hiki umerudi kwa kasi ukilinganisha na hapo awali. Sasa hivi watu huporwa vitu vyao asubuhi na mara nyingine hutoboa madirisha na kuiba nyakati za usiku,” alisema Veronica, ambaye ni mama wa familia.
Naye Zainabu Mfaume alikiri kuwapo kwa matukio ya wizi katika eneo hilo, lakini alisema wizi unaofanyika maeneo hayo mara nyingi hufanywa na watu kutoka mbali ya eneo hilo.
“Kweli wizi unafanyika, lakini mara nyingi na watu wanaotoka mbali na eneo hili,” alisema Zainabu.
Harufu
Veronica alisema harufu ya eneo hilo inawapa kero, hasa kipindi cha mvua inakuwa kali na kuwapa hofu juu ya afya zao.
“Harufu huwa kali, hasa kipindi cha mvua ambapo harufu huwa kali kiasi kwamba tunahisi tunavuta hewa chafu, hivyo kutia hofu juu ya afya zetu,” anaeleza Veronica, ambaye ni mkazi wa eneo hilo kwa muda mrefu.
Zainabu anaungana na Veronika kuhusu harufu hiyo ambayo anasema imekuwa kero, lakini wameizoea kutokana na kukaa maeneo hayo kwa muda.
“Harufu ni kero, lakini tumeizoea kwa kuwa ni ya muda mrefu, pia sehemu ambayo ni chanzo cha harufu ni sehemu ambayo wafanyabishara wa damu wanapata riziki yao,” anasema Zainab, mama wa watoto watatu.
Changamoto zilizopo
Baadhi ya wafanyabiashara wa eneo hilo hawakusita kubainisha changamoto zilizopo katika biashara hiyo, huku wakiiambia Mwananchi kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni ukosefu wa soko rasmi la kuuza bidhaa zao, kwani eneo hilo lina machinjio pekee.
Andrea John, ambaye ni mjasiriamali anayejishughulisha na uuzaji wa makongoro alisema wakipata soko rasmi la kuuza bidhaa zao itakuwa vizuri kwa sababu litaongeza thamani ya kipato wanachokipata ukilinganisha na sasa.
“Sisi kama wafanyabiashara tunaiomba Serikali itutengee sehemu maalumu ya kuuzia biashara kwa uhuru, ili kuepuka kukaa kandokando ya barabara na sehemu hatarishi kwa afya zetu, jambo litakaloongeza thamani ya biashara zetu,” amesema Andrea, baba wa familia.
Kiongozi wa wafanyabiashara katika machinjio hayo, Joel Meshack anasema bado ujenzi wa eneo la mabucha kwa ajili ya kuuza nyama unaendelea na tayari mkurugenzi wa jiji ameagiza kukamilishwa kwa ujenzi huo
“Ujenzi wa mabucha yatakayotumika kuuzia nyama bado unaendelea na mkurugenzi ameshatoa agizo kwa wahusika kukamilisha ujenzi kabla ya kuanza kufanya kazi kwa machinjio mapya,” anasema Meshack na kuongeza:
“Kutokana na ufinyu wa eneo wataanza wauzaji wa nyama kutumia mabucha hayo huku utaratibu mwingine ukiandaliwa.”
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri alipowasiliana na gazeti hili kwa njia ya simu alisema ujenzi wa mabucha ya kuuzia nyama unaendelea na yanatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
“Kuhusu suala la soko hadi sasa ujenzi wa mabucha kwa ajili ya kuuzia nyama unaendelea na unatarajia kukamilika hivi karibuni,” alisema Shauri.
Kuyajua mengi zaidi kuhusu machinjio ya Vingunguti, ungana nasi tena simulizi hii itakapoendelea kesho...