Machumu: Vijana wanaamini watu kuliko taasisi

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd (MCL), Bakari Machumu.
Muktasari:
- Katika ukuaji wa teknlojia ya habari na mawasiliano (Tehama), taasisi zimeshauriwa kubadilka na kuwa na uwezo wa kutoa uamuzi kwa haraka.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd (MCL), Bakari Machumu amesema watu wengi hasa vijana wamekuwa na mwelekeo wa kuamini watu kuliko kuamini taasisi mbalimbali.
Hali hiyo ndiyo ilifanya kuwapo kwa watu wenye ushawishi (influencers) ambao wanaweza kuelezea kitu katika hali ambayo mtu anaweza kuiamini.
Machumu amesema uwepo wa watu hao wakati mwingine umekuwa ukitumia mbinu ambazo zinaweza kubadilika haraka zaidi kuliko taasisi ambazo zinatumia muda kubadilika.
Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba 10, 2023 katika mahojiano maalumu na Shirika ka Utangazaji Zanzibar (ZBC) katika kipindi cha Asubuhi Njema wakijadili mada isemayo kuelekea miaka mitatu ya Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi.
"Ukiangalia mashirika kama ya kwetu ukilinganisha na kampuni ndogo zinafanya maamuzi ya haraka sana, ila sisi tunasubiri kidogo tuangalie ndiyo utaratibu uko hivyo. Mashirika haya sasa yanatakiwa kufikiri kama mashirika lakini yafanye kazi kama wajasiriamali kwa kuwa na uharaka wa mabadiliko," amesema Machumu.
Amesema yeye anaamini katika mashirikiano na kama chombo cha habari kiko tayaru kushirikiana na watu wenye ushawishi (influencer) ikiwa udambwidambwi watakaotumia katika uwasilishaji wa vitu uwe ule wenye staha.
"Akiweka unaokwenda na kinyume na maadili ambayo sisi tunayasimamia hatutashirikiana naye ila kama anatumia lugha nzuri tutashirikiana naye," amesema Machumu.
Amesema jama chombo kikijitambulisha kwa sura fulani ndivyo watu wanavyokichukulia na endapo kikitaka kujishusha ili kupata wafuasi, wasomaji watakosoa na kusema 'si Mwananchi tunayoijua'.
"Kwa hiyo unapima, msijishushe sana kwa sababu hiyo ndiyo nafasi ambayo jamii imekupa," amesema Machumu.
Mahojiano hayo yamefanyika ikiwa ni utangulizi kuelekea Kongamano la Mwananchi Jukwaa la Fikra (MTLF) lililoandaliwa kwa ushirikiano na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) litakalofanyika Oktoba 31, 2023 katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar likiangazia miaka mitatu ya Dk Mwinyi madarakani, mafanikio, fursa na changamoto.
Kongamano hilo la 14 kufanyika tangu kuanzishwa kwake ila la kwanza kufanyika Zanzibar kwa sababu mengi yamekuwa yakifanyika Dar es Salaam.