Mafunzo ya vitendo yageuka changamoto kwa wanafunzi

Mafunzo ya vitendo yageuka changamoto kwa wanafunzi

Muktasari:

  • Wakati Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ikisema muda wa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu unatosha, baadhi ya wanafunzi na wahadhiri wamekosoa wakitaka kuongezwa kwa muda zaidi ili kuwafanya wanafunzi wapate uzoefu.

Wakati Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ikisema muda wa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu unatosha, baadhi ya wanafunzi na wahadhiri wamekosoa wakitaka kuongezwa kwa muda zaidi ili kuwafanya wanafunzi wapate uzoefu.

“Mtaala huandaliwa na wahadhiri wa vyuo vikuu na kuidhinishwa na bodi za wataalamu kwa kushirikiana na wadau wengine, kisha hupewa ithibati na TCU ili kuruhusiwa kufundishwa. Kwa hiyo kwamba muda wa mafunzo unatosha au hautoshi, inahitaji utafiti wa kisayansi ili kufanya maamuzi sahihi,” alisema Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Kihampa.

Muda wa mafunzo ya vitendo hutolewa kulingana na kozi na chuo husika. Baadhi ya kozi wanafunzi hupewa wiki tano, wengine wiki nane na wengine hadi miezi mitatu.

Kwa baadhi ya kozi, mafunzo hayo hutolewa kila mwaka na kozi nyingine mara moja kwa miaka mitatu.

Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wametaka taasisi za elimu kutafakari uwezekano wa kuongeza muda wa mafunzo hayo kwa kuwa hautoshi.

Waliyasema hayo hivi karibuni baada ya kuhitimu mafunzo ya vitendo katika taasisi ya Malembo Farm jijini Dar es Salaam.

Janet James anayesoma shahada ya kwanza ya Mazingira na Jiografia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka wa tatu anasema mafunzo hayo yamempa uzoefu wa kile alichojifunza chuoni.

“Nilichojifunza ni jinsi kilimo kinavyoathiri udongo na kinyume chake. Kwa mfano, udongo unaweza kuathiuri mimea na mimea inavyoweza kuathiri udongo na jinsi ya kukabiliana na athari hizo.

“Pia nimejifunza jinsi ya kuandika ripoti na hivyo ninaweza kuandika ripoti za miradi na uwezo wa kujitegemea kiuchumi na pia mbinu za kilimo bora zikiwemo za kukinga mmomonyoko wa udongo,’’ alisema.

Hata hivyo, Janet alisema muda wa mwezi mmoja aliopewa kwa ajili ya mafunzo hayo, haukuwa rafiki kwake kuelewa kila kiu, hivyo kuomba muda uongezwe.

Maoni hayo yanafanana na ya Anthony Sekumbo aliyehitimu shahada ya sayansi ya wanyama katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).

“Nashauri vyuoni waongeze muda wa mafunzo kwa vitendo ili tupate uzoefu wa kazi na tuweze kujiajiri. Kwa mfano, sasa tunatumia wiki tano kujifunza kwa vitendo masomo ya mwaka mzima,’’ alisema na kuongeza:

“Pia tunaiomba Serikali izisaidie taasisi binafsi kama hii Malembo Farm kwa kuzipa ufadhili kutokana na mchango mkubwa wanaofanya kwa jamii. Kwa mfano, ukitaka kufuga samaki ni gharama kubwa wanazoingia sekta binafsi.’’

Kwa upande wake Lucy Maselle anayetokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua shahada ya Kilimo Biashara alisema mafunzo hayo yamempa uelewa mkubwa wa kile anachofundishwa darasa licha ya kubanwa na muda.

“Changamoto tuliyopata ni ufinyu wa muda wa mafunzo haya, Kwa mfano, mimi nimesoma miaka miwili chuoni, lakini mafunzo kwa vitendo nimekuja kuyapata kwa wiki nane tu ambazo hazitoshi,” alisema Lucy.

Mwanafunzi mwingine aliyezungumzia hilo ni Glorian Sulle anayesoma stashahada ya uandishi wa habari Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Muda hautoshelezi kabisa kwa mwanafunzi kuelewa kiundani kuhusu kazi husika. Vyuo ikiwezekana waongeze muda wa mafunzo maana pia uelewa unatofautiana. Wapo watu wanaoelewa taratibu na wengine wenye uelewa waharaka,” alisema mwanafunzi huyo aliyefanyia mazoezi yake katika Kampuni ya Mwananchi Communications Limited.

“Muda wa field hautoshi kwa mimi mwanafunzi kuweza kupata ujuzi. Pia kuna aina tofauti ya wanafunzi kuna wenye uelewa wa taratibu muda wa miezi miwili ndio kipindi ambacho unakuta anaanza kuelewa, hivyo angekaa zaidi angeweza kupata ujuzi vizuri,” alisema Rukia Kiswamba anayesomea pia shahada ya uandishi wa habari.

Wahadhiri

Mmoja wa waadhiri wa SUA aliyeomba kutotajwa jina lake gazetini, ameungana na wanafunzi akisema muda wa mafunzo kwa vitendo hautoshi.

“Kwa mfano, mwanafunzi anapewa wiki tano, kati ya hizo wiki moja na nusu anaitumia kuzoea ile ofisi au kampuni aliyopo, halafu zile wiki tatu na nusu zilizobaki ndiyo anakuwa kwenye kilele cha kujifunza, halafu ghafla anaambiwa muda umekwisha, anatoka pale anakuwa bado hajaiva,” alisema mhadhiri huyo anayefundisha Kilimo Biashara.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Alexander Makulilo, amekiri kuwa muda wa mafunzo kwa vitendo hautoshi akisema changamoto hutatuliwa kulingana na taaluma husika.

“Mafunzo yale kwa kweli huwa hayatoshi, ndiyo maana baadhi ya mashirika na taasisi hutoa internship (mafunzo kwa vitendo) ya mwaka mzima au hata miezi sita ili kumwangalia mwajiriwa mpya kama anamudu kazi na nidhamu,” alisema.

“Wiki nane au miezi miwili haitoshi, ndiyo maana hata wanasheria huwa wanatoa mwaka mzima wa kwenda Shule ya Sheria na wanakua wanajiunga na ofisi za sheria wakati wa mafunzo hayo. Nashauri wadau mbalimbali watoe ‘internship’ kwa waajiriwa wapya ili kuwapa uzoefu,” ameongeza Profesa Makulilo.

TCU

Profesa Kihampa alisema kwa kuzingatia makubaliano ya wadau na vyuo husika wakati wa kuandaliwa kwa mitalaa, muda uliopo sasa unatosha.

Alisema kuwa pamoja na kupitishwa kwa mitalaa, bado ipo nafasi ya kufanyiwa mapitio makubwa au madogo na wadau wakati ukiendelea kufundishwa au unapomaliza muda.

“Mtalaa siyo kwamba haurekebishiki, huwa unafanyiwa mapitio na wadau. Kwa jinsi wadau walivyokubaliana mimi naona muda wa mafunzo ya vitendo unatosha,” alisema.

Wahitimu kutoajirika

Alipoulizwa kuhusu hoja ya wanafunzi kutoajirika kutokana na kukosa uzoefu wa kozi walizosomea, Profesa Kihampa alisema;

“Kazi duniani kote hazitoshi, siyo hapa Tanzania tu, hata ukienda Ulaya. Kusema kwamba wanafunzi wa Tanzania hawaajiriki inahitaji kufanya utafiti vinginevyo inakua ni slogan tu. Mbona wote tumesomea hapa hapa na tumeajiriwa?”

Alisisitiza kuwa muda wa mafunzo ya vitendo unatosha na kwamba kama kuna malalamiko yanapaswa kuripotiwa ipasavyo ili yafanyiwe utafiti na kujadiliwa na wadau kufanya marekebisho sahihi.

Malembo Farm

Akizungumzia mafunzo anayotoa, Mkurugenzi wa taasisi ya Malembo Farm, Lucas Malembo alisema wanajitahidi kukidhi kiu ya wanafunzi kwenye mafunzo hayo kwa njia zote, japo muda hautoshi.

“Kwa kipindi chote ambacho wamekuwa kwenye mafunzo, tumeona muda ndiyo changamoto kubwa. Ukumbuke kila mwaka kuna zaidi ya wanafunzi 800,000 wanaingia kwenye soko la ajira, je, wanapata ajira hizo? Je, wanauzika kwenye soko la ajira?” alihoji.

Aliendelea: “Namna bora ni kuwaandaa vijana ili waweze kujiajiri wenywe. Kwa mfano, kwa wanafunzi wanaosoma kilimo bishara, tunataka aweze kuchambua ripoti za kilimo na kuishauri Serikali na wadau wengine kuhusu mwelekeo wa biashara.”

Alitoa wito kwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuona namna inavyoweza kubadilisha mfumo wa mafunzo ya vitendo kwa kuongeza muda, kutoka wiki nane hadi mwaka mzima wa vitendo tu.