Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mafuriko yaua wanane Tanga, wamo watoto watatu

Muktasari:

  • Mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Tanga kwa takriban wiki tatu sasa zimeendelea kusababisha maafa ambapo watu wanane wamefariki dunia kutokana na mafuriko.

Tanga. Wakati watu wanane wakiwemo watoto watatu wakipoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Tanga kwa takriban wiki tatu sasa, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuchukua tahadhari na kuepuka kuingia kwenye madimbwi.

Taarifa za matukio ya vifo hivyo zimetolewa leo, Jumanne Novemba 8, 2023 na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu athari za mvua zinazoendelea kunyesha

Kamanda Mchunguzi amesema mvua zimesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu na kusababisha madimbwi kwenye maeneo mbalimbali hivyo ni vema wananchi wakawa makini na kuwazuia watoto wasicheze kwenye madimbwi.

Kuhusu vifo vilivyotokana na mvua, Kamanda Mchunguzi amesema baadhi ya watu walisombwa na mafuriko huku watoto wakitumbukia kwenye madimbwi

Amewataja waliokufa ni Fabius Masalu (23) mkazi wa Kijiji cha Ngomeni Kata ya Ngomeni Tarafa ya Ngomeni Wilayani Muheza ambaye alisombwa na mafuriko wakati akivuka mto akitokea shambani na Aboubakar Said (7) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza wa Shule ya Msingi Maweni Kichangani jijini Tanga.

Mwingine ni Nganahe Masai (8) aliyesombwa na mafuriko wakati akichunga mbuzi Kijiji cha Gombero Wilaya ya Handeni na Simon Arod (3) wa Wilaya ya Kilindi ambaye alitumbukia kwenye dimbwi.

Kamanda Mchunguzi amesema Mhina Gabriel (45) wa Kijiji cha Mianga Songa wilayani Muheza na Mbwana Makame (48) wa Kijiji cha Kicheba Wilaya ya Handeni ni miongoni mwa waliopoteza maisha mutokana na mvua hizo.

Amesema watu wengine wawili waliopoteza maisha mpaka sasa majina yao bado hayajapatikana hivyo amewaomba wakazi wa Tanga kujihadhari mvua zinazoendelea kunyesha.

Itakumbukwa kuwa Oktoba 8, 2023 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitabiri uwepo wa mvua za El-Nino kati ya Oktoba na Desemba mwaka huu na kuzishauri sekta na taasisi mbalimbali, zikiwamo za kilimo, mifugo, uvuvi, utalii, wanyamapori, uchukuzi, mamlaka za miji, nishati, maji na madini, sekta binafsi, Wizara ya Afya na Menejimenti za Maafa kuchukua hatua mapema kabla ya kuanza kwa mvua hizo.