Mahakama yatoa siku 30 mkurugenzi wa Jatu, DPP kujadiliana

Muktasari:

  • Hii ni mara ya pili kwa Peter Gasaya anayekabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu, kumwandikia barua DPP kuomba kukiri mashtaka.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa siku 30 kuanzia leo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33) anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili likiwemo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu, kufanya majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini( DPP) ya kuimaliza kesi yake.

Hatua hiyo inatokana na mshtakiwa huyo kumwandikia barua DPP ya kukiri na kuomba apunguziwe adhabu dhidi ya mashtaka yanayomkabili.

Gasaya anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya Jatu kwa madai kuwa fedha hizo atazipanda kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua si kweli.

Hii ni mara ya pili kwa Gasaya, kumwandikia barua DPP ya kuomba kukiri mashtaka yake na kuomba apunguziwe adhabu. Mara ya kwanza ilikuwa Aprili 24, 2023.

Hata hivyo, Julai 31, 2023 mshtakiwa huyo aliondoa nia yake ya kufanya majadiliano na DPP kwa kile alichodai kuwa barua aliyoandika na kuiwasilisha upande wa mashtaka, haionekani.

Uamuzi huo umetolewa leo Machi 12, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate wakati kesi hiyo ilipoitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Gasaya, kupitia wakili wake, Kung’e Wabeya amesema: “Mteja wangu ameandika barua ya maombi kwa  DPP akiomba kukiri mashtaka yake ili aweze kuimaliza kesi hiyo, hivyo maombi haya tutayawasilisha leo kwa upande wa mashtaka, sasa kutokana na hali hii  tunaomba tupewe mwongozo," alidai Wakili Wabeya.

Kabla ya mshtakiwa huyo kuwasilisha taarifa hiyo, Wakili wa Serikali Eva Kassa alisema kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na kuwa upelelezi wake haujakamilika, hivyo wanaomba terehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada kueleza hayo, ndipo Hakimu Wabeya, alipoieleza mahakama uamuzi wa mteja wake.

Hakimu baada ya kusikiliza maelezo ya pande mbili, alitoa siku 30 kwa ajili ya mshtakiwa na upande wa mashtaka kukutana na kufanya majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo.

"Ninatoa siku 30 ili muweze kukaa mezani kwa ajili ya kufanya mazungumzo baina ya pande zote," alisema kisha akaahirisha kesi hiyo hadi Machi 26, 2024 itakapotajwa.

Kesi hiyo imesikilizwa kwa njia ya video huku mshtakiwa akiwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili kutokuwa na dhamana.

Gasaya alifikishwa mahakamani hapo Desemba 29, 2022 na kusomewa mashtaka kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu.

April 11, 2023 mshtakiwa huyo alifutiwa kesi hiyo na DPP chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022 na akakamatwa tena na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili, ambayo anatakiwa kumalizana na DPP.

Mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka ya kujipatia Sh5.1 bilioni ya la pili la kutakatisha fedha hizo.