Mahakama yatoa siku 30 Seth na mwenzake kujadiliana na DPP

Mahakama yatoa siku 30 Seth na mwenzake kujadiliana na DPP

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru majadiliano  ya kukiri mashtaka yaliyowasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) dhidi ya mwenyekiti mtendaji wa PAP, Harbinder Seth na aliyekuwa mwanasheria wa kampuni ya  kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege yasikilizwe  ndani ya siku 30 kuanzia leo Alhamisi Februari 25, 2021.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru majadiliano  ya kukiri mashtaka yaliyowasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) dhidi ya mwenyekiti mtendaji wa PAP, Harbinder Seth na aliyekuwa mwanasheria wa kampuni ya  kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege yasikilizwe  ndani ya siku 30 kuanzia leo Alhamisi Februari 25, 2021.

Mahakama imefikia uamuzi huo leo baada ya Seth ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2017, kuwasilisha mahakamani hapo maombi mawili ambayo ni kuletwa mahakamani kila kesi yake inapotajwa na kukutana na DPP kwa ajili ya kufanya majadiliano ya kukiri mashtaka yake.

Hakimu Haruna Shaidi baada ya kusikiliza hoja za pande zote alikubaliana na hoja za upande wa utetezi akisema DPP ana mamlaka ya kukubali au kukataa maombi hayo lakini pia halazimishwi kukubali. 

"DPP halazimishwi kukubali lakini pia lazima akubali au akatae na sio kukaa kimya, mahakama pia ina uwezo wa kuelekeza ndani ya siku 30 makubaliano hayo yafanyike na jibu litolewe, hivyo mahakama inaelekeza jambo hilo lifanyike ndani ya siku 30 kuanzia leo," amesema Shaidi. 

Kuhusu washtakiwa kushindwa kupelekwa mahakamani, Shaidi alielekeza washtakiwa hao kupelekwa mahakamani kila tarehe ya kesi hiyo inapotajwa kwani sheria iko wazi.

"Mahakama inasisitiza sheria ifuatwe na mahabusu waletwe mahakamani kila tarehe ya kesi hiyo inapoitwa," amesema hakimu huyo.

Awali, wakili wa Serikali Faraja Ngukah alidai kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Ngukah baada kueleza hayo, ndipo Melchisedeck Lutema ambaye ni wakili wa Seth alipoieleza mahakama hiyo kuwa licha ya kuandika barua hizo mbili kuomba kufanya majadiliano moja ya  Julai Mosi 2019 iliyopokewa Julai 23,2019 na ya pili ya Julai 20,,2020 iliyopokewa Septemba 10,2020.  mpaka sasa zote hazijajibiwa.

"Kwa mujibu wa kanuni mpya za Pre-bargain zilizotolewa na Jaji Mkuu, mwaka huu, mahakama ina mamlaka ya kutoa muda kwa pande zote kujadiliana na kukamilisha majadiliano kwa muda usiozidi siku 30. Hivyo tunaomba mahakama itoe maelekezo hayo," amedai Lutema.

Wakili Lutema amesema ni jukumu la DPP kujibu barua za wateja wake na  kama hataki kuingia majadiliano aseme ili waendelee na hatua nyingine.

"Ofisi ya DPP imekaa kimya kwa kutojibu barua za wateja wetu za kukiri makosa,” amesisitiza.

Alidai, mteja wake aliandika barua Julai mosi, 2019 na kupokelewa Julai 23, 2019,na barua ya pili aliiandika Julai 20, 2020 na ilipokelewa ofisi ya DPP Septemba 10, 2020.

Amedai mteja wake yupo tayari kufanya makubaliano na anatoa taarifa mahakamani kwa mujibu wa kanuni ya tatu ya kanuni mpya za makubaliano zilizotolewa na jaji Mkuu mwaka 2021 na chini ya kifungu cha 5 cha kanuni hizo. 

"Mahakama ina mamlaka ya kutoa muda wa pande husika wa kujadiliana na kukamilisha makubaliano, muda huo ni ndani ya siku 30, " amedai.

Katika hatua nyingine wakili huyo alikumbushia barua aliyoandika mteja wake akilalamika kutoletwa mahakamani kwa muda wa miezi saba sasa ambapo hakimu aliamuru mshtakiwa huyo kuletwa mahakamani kila baada ya siku 14 kwani ni haki yake kisheria. 

Akijibu hoja hizo, wakili Ngukah alikiri kwamba ni haki ya mshtakiwa kuletwa mahakamani kila baada ya siku 14 na anachokumbuka mara ya mwisho mshtakiwa  aliletwa Desemba 17, 2020 na kwamba jana walishindwa kupelekwa mahakamani  kutokana na shida ya usafiri.

Kuhusu barua ya maombi ya kukiri makosa,  Ngukah amedai mawakili wafuatilie suala hilo kwa DPP.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza hoja za pande zote alitoa uamuzi na kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 11, 2021.

Mbali na washtakiwa hao, mshtakiwa wengine ni mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa kampuni ya IPTL, James Rugemalira.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 12 likiwemo la kutakatisha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh309,461,300,158.27.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam na kwamba walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.