Makandege aunganishwa kesi ya Seth, Rugemalira

Aliyekuwa mwanasheria na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya kufua Umeme ya IPTL, Joseph Makandege akiwa chini ya ulinzi baada ya kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba, Wakili Kadushi alidai katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa kula njama.

Dar es Salaam. Aliyekuwa mwanasheria wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuisababishia hasara Serikali ya dola za Marekani 980,000.

Makandege, ambaye aliwahi kuwa katibu wa IPTL alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2017 na jopo la mawakili watatu wa upande wa mashtaka wakiongozwa na wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiwa na Faraja Nchimbi na wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon.

Hata hivyo, kabla ya kusomewa mashtaka yake, Wakili Kadushi aliwasilisha ombi mahakamani hapo la kutaka mshtakiwa huyo kuunganishwa katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa wawili ambao ni Harbinder Seth, ambaye alikuwa mwenyekiti mtendaji wa PAP na mkurugenzi wa VIP Engineering, James Rugemalira.

Kwa maana hiyo, Makandege ambaye anatetewa na wakili Joseph Sungwa, ameunganishwa na Seth na Rugemalira katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba, Wakili Kadushi alidai katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa kula njama.

Anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Kenya, Afrika Kusini na India, ambapo Makandege na washtakiwa wenzake walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kadushi alidai katika shtaka la pili, ambalo ni la kuongoza genge la uhalifu, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo katika nchi hizo, na kwamba akiwa si mtumishi wa Serikali alishirikiana na watumishi wa umma kwa kuratibu na kufadhili mpango wa uhalifu.

Katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Wakili Nchimbi alidai Makandege, anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 23, 2014 na Februari 2014.

Kwamba alijipatia dola 380,000 katika benki ya Stanbic iliyopo Kinondoni na dola 600,000 katika benki ya UBL Bank(T) Ltd iliyopo wilaya ya Ilala, fedha zilizotoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa nyakati tofauti.

Wakili Simon alidai katika shtala kuisababishia hasara Serikali, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 23, 2014 na Februari 10, 2014 katika benki ya Stanbic na UBL Bank (T) Ltd, na kuisababishia Serikali hasara ya dola 980,000. Makandege anakabiliwa pia na shtaka la kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

Wakili Simon alidai kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 23, 2014 na Februari 10, 2014 katika benki ya Stanbic na UBL Bank (T) Ltd, ambapo alitakatisha kiasi hicho cha fedha wakati akijua ni zao tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Simba alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.

Upande wa mashtaka walidai upelelezi haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 2, 2020 itakapotajwa tena na mshitakiwa alirudishwa rumande.