Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yazuia mashahidi kutajwa kesi ya ugaidi, kusikilizwa faragha

Muktasari:

  • Usikilizaji wa shauri hilo linalohusishwa na masuala ya ugaidi, utafanyika faragha kwa lengo la kuwalinda mashahidi na watoa taarifa, ambapo pia Mahakama imetoa amri ya kutotajwa majina ya mashahidi wala maelezo yao yanayoweza kuwatambulisha.

Arusha. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Masjala Ndogo ya Geita, imetoa amri ya kutotajwa majina wala taarifa zozote zitakazoweza kuwaeleza au kuwatambulisha mashahidi katika kesi ya ugaidi inayowakabili watuhumiwa watano.

Kwa mujibu wa hati za kiapo zilizowasilishwa kuunga mkono maombi hayo, inadaiwa kuwa watuhumiwa pamoja na watu wengine walijihusisha na kundi la kigaidi, walielekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujiunga na kundi la Allied Democratic Forces, kwa madhumuni ya kupata mafunzo ya kijeshi na kuratibu makundi yenye nia ya kupindua Serikali.

Watuhumiwa hao ni Athuman Yusuph, Mussa Kisumo, Said Kisia, Abdulrahman Yasin na Kulwa James.

Kwa kuzingatia sababu za kiusalama, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliwasilisha ombi la kuisikiliza Mahakama upande mmoja, akiomba amri ya kuzuia kutajwa kwa utambulisho na mahali walipo mashahidi husika.

Maombi hayo dhidi ya watuhumiwa hao watano, yalisikilizwa na kutolewa uamuzi jana Jumanne Mei 6, 2025 na Jaji Sedekia Kisanya na nakala ya uamuzi huo imewekwa katika tovuti ya Mahakama.

DPP aliwasilisha maombi hayo chini ya kifungu cha 34(3) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi na kifungu cha 188(1) na (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), akiomba mashahidi katika kesi ya jinai itakayosikilizwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita wasitajwe wala kutambulika kwa namna yoyote.

Pia, wameomba mashahidi waruhusiwe kutoa ushahidi kwa njia ya video, kutowekwa wazi utambulisho na nyaraka zinazoweza kuwatambulisha mashahidi wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, kwa lengo la usalama wao katika usikilizwaji wa awali na usikilizwaji kamili wa kesi hiyo.

Aidha, DPP ameiomba Mahakama itoe amri ya kusikilizwa faragha mwenendo wa kesi hiyo na hatua nyingine ambazo Mahakama itaona ni muhimu ili kuhakikisha usalama wa mashahidi hao.

Ombi hilo liliambatanishwa na viapo viwili kikiwemo cha Wakili wa Serikali, Godfrey Odupoy.

Katika hoja za DPP zilizowasilishwa mahakamani hapo na Wakili Odupay, kumekuwa na vitisho hali inayowapa hofu mashahidi na kuwatisha ili kuwazuia kutoa ushahidi kwa uhuru na ukweli mahakamani hapo.

Aliieleza Mahakama kuwa uchunguzi umebaini jitihada zinazofanywa na baadhi ya washirika wa wajibu maombi kutafuta utambulisho wa mashahidi ili kuwatisha au kuwadhuru ili kuzuia kutoa ushahidi wao, hivyo kuomba Mahakama kukubali maombi hayo ili kulinda usalama wa mashahidi na familia zao.

Aliieleza Mahakama kuwa washtakiwa wanakabiliwa na mashitaka chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2022 na kwamba kesi hiyo kwa sasa iko katika hatua ya usikilizwaji.

Kutokana na vitisho hivyo, Wakili huyo aliiomba Mahakama kuridhia ombi hilo na hatua za kiulinzi kuchukulia akitolea mfano kesi ya DPP dhidi ya Yusuph Ally Huta na wengine watano, katika maombi ya mwaka 2022, hatua sawa za ulinzi wa mashahidi zilitolewa.


Uamuzi wa Jaji

Katika uamuzi huo, Jaji Kisanya amesema jukumu la Mahakama ni kupima kama ombi la DPP lina mashiko au la.

Amesema chini ya kifungu cha 188 (1) cha CPA, Mahakama inaweza kutoa hatua za ulinzi, ikiwa ni pamoja na kuruhusu ushahidi wa mashahidi kutolewa kwa njia ya video, kuamuru kutowekwa utambulisho wa shahidi na mahali alipo kwa sababu za kiusalama.

Amesema katika kesi ya hivi karibuni ya DPP dhidi ya Zuberi Ngale na wengine wanane katika maombi namba 6490/2025, hatua za ulinzi wa mashahidi zilitolewa.

Jaji Kisanya amesema katika kuamua uhalali wa ombi hilo, Mahakama lazima itathmini ikiwa usalama wa mashahidi waliokusudiwa kutoa ushahidi ungekuwa hatarini iwapo utambulisho wao utafichuliwa.

Amesema kutokana na taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa wakati wa upelelezi kuonyesha kuwa washtakiwa hao wakishiriana na jamaa zao wamekuwa wakifanya jitohada za kubaini utambulisho wa mashahidi wa upande wa mashtaka kwa nia ya kuwazuia kutoa ushahidi.

Jaji Kisanya amesema kutokana na mazingira hayo Mahakama inakubali hoja ya Wakili huyo wa Serikali kwamba kutoa utambulisho wa mashahidi utahatarisha usalama wao na familia zao hivyo hatua za kiulinzi zitafutwa katika usikilizwaji wa kesi hiyo ili kuwahakikishia usalama wao.

Mahakama imehitimisha kuwa baadhi ya mashahidi watatoa ushahidi wao kwa njia ya mtandao, kutokutolewa utambulisho wa mahali walipo mashahidi na usikilizwaji kufanyika faragha.