Majaliwa aagiza matumizi nishati ya gesi kupanuliwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi na watumisha wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) alipotembelea banda lao katika maonyesho ya Wizara ya Nishati na taasisi zake, katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo. Wa pili Kulia ni Waziri wa Nishati, January Makamba. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza Wizara ya Nishati kupanua matumizi ya nishati ya gesi asilia ili kupunguza athari za kimazingira zinazotokana na ukataji wa misitu nchini.

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza Wizara ya Nishati kupanua matumizi ya nishati ya gesi asilia ili kupunguza athari za kimazingira zinazotokana na ukataji wa misitu nchini.

Akizungumza leo Jumatano Mei 25, 2022 wakati alipotembelea maonesho ya Wizara ya Nishati na taasisi zake kwenye viwanja vya Bunge, amesema kuna umuhimu wa kupanua nishati ya gesi.

Waziri Mkuu amesema kazi iliyopo ni kutengeneza njia za gesi ili iwafikie wananchi na waondokane na ukataji miti.

“Tupanue wigo na huduma hii iwafikie watu, tumeanza na Dar es Salaam, tuje kwenye jiji, manispaa zetu na hata hapa Dodoma tuwe na tawi na kazi hii iendelee,”amesema.

Aidha, Majaliwa amewaagiza watendaji wote katika sekta ya nishati kuhakikisha wanasimamia upatikanaji wa nishati ya umeme na nishati nyingine ikiwamo mafuta ili kuendelea kuiwezesha nchi kupata fursa ya kuendelea kukua kiuchumi.

Amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeitaka Serikali kuhakikisha upatikanaji wa umeme katika vyanzo unaimarishwa, kuendelezwa na kuhakikisha usambazaji wa umeme unawafikia wananchi mpaka vijijini ili kila Mtanzania anufaike kwa kupata nishati hiyo.