Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majaliwa: Wananchi hifadhini chakula

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akisoma hoja ya kuhitimisha Bunge la 12 mkutano wa 16 leo Septemba 6,2024 bungeni Jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha

Muktasari:

  • Serikali yaagiza wananchi kutumia chakula kilichopo sasa kwa uangalifu

Dodoma. Serikali imetoa tahadhari kwa wananchi kutumia chakula kwa uangalifu kuanzia ngazi ya familia na kuzingatia kanuni bora za hifadhi ya mazao ya chakula kutokana na utabiri wa hali ya hewa kubashiri msimu huu kutokuwa na mvua za kutosha.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hayo leo Septemba 6, 2024 akitoa hotuba kuahirisha Mkutano wa 16 wa Bunge, ambao umepitisha miswada minane, huku maswali ya msingi 154, ya ngongeza 459 na manane ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa. Bunge limeahirishwa hadi Jumanne ya Oktoba 29, 2024.

“Nitoe wito kwa wananchi kutumia vizuri mavuno yaliyopatikana katika msimu wa 2023/2024 kwa kutunza chakula cha kutosha katika ngazi ya kaya kwa kuzingatia kanuni bora za hifadhi nzuri ya mazao ya chakula.

“Nitumie nafasi hii kuwakumbusha wananchi kuendelea kutumia chakula kilichopo sasa kwa uangalifu mkubwa, kuhifadhi chakula cha kutosha katika ngazi ya familia na kuepuka matumizi mabaya ya chakula au yasiyokuwa ya lazima,” amesema.

Amesema katika baadhi ya maeneo ya nchi ni vema wananchi wakachukua tahadhari mapema ili kuzalisha mazao yanayokomaa kwa muda mfupi.

“Nitumie fursa hii kuwahimiza wananchi kupanda aina ya mazao yanayokomaa kwa muda mfupi na yanayostahimili ukame. Kwa upande mwingine maofisa ugani wawaelimishe wananchi wetu kuhusu mazao yanayopaswa kupandwa katika maeneo yao,” amesema.

Majaliwa akizungumzia kuhusu uhifadhi wa chakula, amesema Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, inaendelea kununua ziada ya mavuno yaliyopatikana kutoka kwa wakulima kwa ajili ya kuyahifadhi na kwamba, sehemu ya hifadhi hiyo itatumika katika kuongeza upatikanaji wa chakula kwenye maeneo yatakayobainika kuwa na upungufu nchini.

Tahadhari hiyo ameitoa baada kuelezea mwenendo wa hali ya hewa nchini unaokwenda sambamba na msimu wa kilimo utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) umeonyea katika msimu huu wa kilimo mvua katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2024 kwenye maeneo mengi ya nchi zitanyesha chini ya wastani.

“Hapa nchini mvua za vuli ni mahususi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua ambayo yanajumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Simiyu na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma. Mikoa mingine ni Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro.

“Utabiri unaonyesha kuwa mvua zitakuwa chini ya wastani katika maeneo mengine yanayopata mvua hizo na zinatarajiwa kuanza kwa kusuasua na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha,” amesema.

Majaliwa amesema, “utabiri huu unaashiria kuwa shughuli za uzalishaji wa mazao ya chakula zitaathirika hali inayoweza kupunguza utengemano wa upatikanaji wa chakula katika maeneo yanayopata mvua hizo na maeneo mengine ya nchi.”

Katika hatua nyingine, amesema katika msimu huu wa kilimo wa mwaka 2024/2025, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima kama ilivyofanyika katika misimu iliyotangulia.

Kwa kutambua mwenendo wa uzalishaji wa mahindi na ongezeko la mahitaji yake ndani na nje ya nchi katika msimu wa 2024/2025, amesema Serikali itatoa ruzuku ya mbegu bora za mahindi kwa wakulima.

Majaliwa amesema uzalishaji wa ndani wa mbolea na mbegu bora unaendelea kuimarika kutokana na jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi. Amesema uzalishaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 84,696 mwaka 2022/2023 hadi kufikia tani 158,628 msimu wa mwaka 2023/2024.

“Uzalishaji wa ndani wa mbegu zilizothibitishwa ubora za mazao mbalimbali nao umeongezeka kutoka tani 42,096 kwa msimu wa mwaka 2022/2023 hadi kufikia tani 56,114 msimu wa mwaka 2023/2024 ikiwa ni hatua mahususi ya kuchangia utoshelevu wa pembejeo za kilimo ndani ya nchi,” amesema.

Ameiagiza Wizara ya Kilimo isimamie kwa ukaribu upatikanaji na usambazi wa pembejeo za kilimo hususani mbolea ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu ujao wa kilimo na kwa kuzingatia jiografia za kanda za kilimo nchini.

Amewataka maofisa ugani waendelee kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya teknolojia bora za uhifadhi wa mazao ya chakula na matumizi sahihi ya chakula hicho katika ngazi ya familia.

Uchaguzi Mkuu 2025

Majaliwa amewatoa wasiwasi wapigakura nchini wenye kadi za kupiga kura zenye jina la zamani la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya kupata kadi mpya zenye jina jipya la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kwamba hawana haja ya kubadili na kupata mpya.

Amesema kadi hizo kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ni halali na zitaendelea kutumika.

“…niwatoe wasiwasi wananchi wote walioandikishwa mwaka 2015 na mwaka 2019 hadi 2020 kuwa kadi zao ni hali kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha sheria ya uchaguzi ya Rais, wabunge na madiwani na zitatumia kwenye uchaguzi mkuu wa 2025,” amesema.

Amesema INEC inaendelea na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura. “Hadi sasa Tume imekamilisha uboreshaji wa daftari katika mikoa saba ya Kigoma, Tabora, Katavi, Kagera, Geita, Mwanza na Shinyanga. Kuanzia Septemba 4 hadi Septemba 10, 2024 uboreshaji wa daftari unaendelea katika mikoa ya Mara, Simiyu na sehemu ya Mkoa wa Manyara katika halmashauri ya wilaya za Babati, Hanang, Mbulu na Mji wa Babati,” amesema.

Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Jumatano ya Novemba 27, 2024 amesema kazi za msingi zilizokamilika ni kuandaliwa kwa kanuni za uchaguzi wa viongozi wa mamlaka wa serikali za mitaa, ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa katika mamlaka za wialaya na miji.

“Mwongozo wa elimu ya mpiga na mwongozo wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaendelea kutolewa. Maandalizi mengine ya uchaguzi yapo katika hatua za ukamlishaji ambayo yanajumuisha kutangaza orodha ya maeneo ya utawala, uhakiki wa vituo vya kupigia kura awamu ya pili na manunuzi ya vifaa vya uchaguzi.

“Kwa sasa mamlaka husika zinaendelea na utoaji wa elimu ya mpigakura kupitia vyombo vya habari mapango na mitandao ya kijamii,” amesema.


Treni ya SGR

Majaliwa ameitaka Wizara ya Uchukuzi iendelee kulisimamia kwa karibu Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kuhakikisha huduma za treni ya kisasa ya umeme (SGR) zinaboreshwa na miundombinu inaimarishwa ili mradi huo uweze kudumu kwa muda mrefu.

Amesema treni hiyo inaendelea kutoa huduma kwa wananchi na imechangia kuimarisha sekta ya usafirishaji.

Majaliwa amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali itaendeleza sekta ya uchukuzi ambayo pamoja na mambo mengine itasimamia sekta ya reli ikiwemo ujenzi wa SGR na uendeshaji wa treni ya kisasa ya abiria kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.