Makaburi mengine 140 yahamishwa Vingunguti

Muktasari:
- Uhamishaji huo unafanyika kutokana na kuwepo kwa mmomonyoko wa ardhi pembezoni mwa Mto Msimbazi, uliosababisha baadhi ya makaburi kusombwa na maji.
Dar es Salaam. Makaburi 140 yamehamishwa katika eneo la makaburi la Vingunguti jijini Dar es Salaam na kupelekwa makaburi ya serikali ya Mwanagati nje ya jiji hilo kutokana na eneo hilo lililo karibu na mto Msimbazi kukumbwa na momonyoko wa ardhi.
Makaburi hayo ni yamehamishwa ikiwa imepita miezi minne tangu makaburi 238 mengine yahamishwe katika eneo hilo.
Shughuli hiyo ya siku mbili, ilianza jana na inatarajiwa kukamilika leo Ijumaa Aprili 22, 2022 ambapo masalia ya miili yanapelekwa kuzika Mwanagati.
Akizungumza na Mwananchi, Kaimu Ofisa Afya kutoka Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, Salim Msuya amesema makaburi wanayoyafukua leo ni yale waliyoyagundua wakati wa shughuli ya ufukuaji iliyofanyika Desemba 27 hadi 29 ilivyokuwa ikiendelea.
"Hii kazi inakwenda kwa bajeti, lakini kwa bahati mbaya tukiwa katikati ya shughuli makaburi mengine yakagundulika ambayo tusingeweza kuyaacha kwa kuwa nayo yapo katika eneo hatarishi.
"Awali ilipangwa kufukua makaburi 200 lakini ndio hivyo tukafukua 238 na kujikuta tunatumia hadi akiba ya ziada tuliyokuwa nayo, hivyo ikabidi kuiombea hela nyingine ya kumalizia hayo 140 tuliyofukua Jana na leo yaliyogharimu Sh17 milioni ," amesema Msuya.
Hata hivyo amesema makaburi hayo yanayofukuliwa ni yale yaliyo ndani ya mita kumi kutoka ulipo mto Msimbazi.
Licha makaburi hayo kuhamishwa, Msuya amesema ni ndugu saba tu ndio waliojitokeza na kukubali kuwa miili ya ndugu zao kwenda kuzikwa katika makaburi hayo ya serikali tofauti na Desemba, ambapo takribani miili 26 ndugu walijitokeza.
Baadhi ya ndugu waliozungumza na Mwananchi Digital, akiwemo Charles Sifioni, aliyemzika baba yake hapo mwaka 2010, amesema ameridhika na namna kazi hiyo ilivyoenda kwa kuwasaidia kwenda kuhifadhi miili ya wapendwa wao eneo salama zaidi.