Makalla aanza na kufungua baa, kumbi za starehe zilizofungiwa

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla akizungumza leo Ijumaa Mei 26, 2023 na wamiliki, mameneja na wafanyabiashara wa baa, hoteli na kumbi za starehe jijini Mwanza.

Muktasari:

  • Hivi karibuni Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilitangaza kuzifungia baa na kumbi za starehe 89 nchini kutokana na oparesheni ya wiki moja iliyofanyika katika majiji ya Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza baada ya kubaini kupiga muziki kwa sauti ya juu ambayo ni kinyume cha Sheria ya Mazingira ya mwaka 2014.

Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla ameagiza baa na kumbi za starehe zilizofungiwa na Baraza la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) zifunguliwe huku akipiga marufuku kamata kamata ya nguvu na kuvizia inayofanywa na baraza hilo kwa kushirikiana na jeshi la polisi.

Hivi karibuni NEMC lilitangaza kuzifungia baa na kumbi za starehe 89 nchini na Mwanza zikiwa 31 kutokana na oparesheni ya wiki moja iliyofanyika katika majiji ya Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza baada ya kubaini kupiga muziki kwa sauti ya juu ambayo ni kinyume cha Sheria ya Mazingira ya mwaka 2014.

Mei 22, mwaka huu Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hasan Masala alisema Serikali mkoani humo haijasitisha huduma za chakula na vinywaji katika baa 31 zilizobainika kukiuka sheria, badala yake imezuia upigaji wa muziki na kuzitaka zitoe faini na kufuata taratibu walizopewa na NEMC.

Licha ya kuwa anakabidhiwa ofisi Mei 28 mwaka huu, Makalla ambaye aliteuliwa Mei 15 kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza akitokea Dar es Salaam ametoa maagizo hayo leo Mei 26, 2023 baada ya kukutana na kusikiliza kero za wamiliki, mameneja na wafanyakazi wa baa, hoteli, kumbi za starehe na burudani jijini Mwanza.

Amesema Serikali na wafanyabiashara hao wanashirikiana na wanategemeana katika kodi, leseni, tozo na ushuru mbalimbali na kuwataka wafanyabiashara hao kutoutumia vibaya uhuru waliopata bali wafuate taratibu zilizowekwa kwa kuwajali wananchi.

“Baa zote zilizokuwa zimefungwa kwa sababu ya kelele sasa zifunguliwe na napiga marufuku ukamataji wa nguvu hawa siyo majambazi,”amesema Makalla

Ameongeza “NEMC iendelee kukaa na wafanyabiashara kuona namna bora ya kufanya hiyo biashara bila kuathiri jamii na kutosababisha uchumi, ajira kusimama na kodi za Serikali kupungua,”

Kuhusu mapendekezo mengine yaliyotolewa na wafanyabiashara hao ikiwemo faini kubwa na upatikanaji wa vifaa vya kupima sauti, amewataka NEMC kumalizana nao kwa kufikia makubaliano, kutoa elimu huku akiwataka wamiliki hao kufuata taratibu zinazoratibiwa na baraza hilo akidai Serikali imeonyesha nia njema hivyo wanapaswa na wao kuonyesha nia njema kwa kutovunja taratibu.

Awali akisoma risala kwa niaba ya wafanyabiashara hao, Richard Rongwet amelalamikia oparesheni iliyofanywa na NEMC tangu mwanzo wa Mei, mwaka huu na kuwatoza wafanyabiashara hao kati ya Sh2 milioni mpaka Sh5 milioni huku wakiitaka kutoa elimu kwanza kwa wahusika kabla ya adhabu.

“Tunapingana na adhabu hizi kwa sababu kumekuwa na vitisho vya kupelekwa Mahakamani na kufungiwa biashara hivyo tunaiomba Serikali iwatake Nemc waondoe faini zote walizotupiga kwani hazilipiki na ni mzigo mkubwa kwetu,”

“Kitendo cha NEMC kuwakamata wafanyabiashara na kuwafungia maeneo yao kwa vitisho wakiwa na askari na bunduki imehatarisha biashara yetu na kutishia wateja ambao wamekuwa wakikimbia na kuacha hawajalipa bili,”amesema Rongwet

Naye, mmoja wa maofisa wa NEMC aliyekuwa kwenye kikao hicho ambaye hakutaka kutajwa, amesema “Tayari Serikali imeshatoa maelekezo siwezi kuzungumza tena, lakini tumepokea na utekelezaji utafanyika, kama kutakuwa na cha kuzungumza basi karibu wakati mwingine,”