TPSF yashauri adhabu ya kufungia itolewe na mahakama

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga.

Muktasari:

  • Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga ameshauri muhimili wa Mahakama pekee unatakiwa kutumika katika utoaji wa adhabu ya kufungia maeneo ya biashara za starehe badala ya kuachia taasisi ya Serikali inayolalamikiwa pia kiutendaji.

Dar es Salaam. Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga ameshauri muhimili wa Mahakama pekee unatakiwa kutumika katika utoaji wa adhabu ya kufungia maeneo ya biashara za starehe badala ya kuachia taasisi ya Serikali inayolalamikiwa pia kiutendaji.

 Pendekezo lingine, Maganga ameshauri sheria inayohusika katika utoaji wa adhabu hizo itazamwe upya, utoaji wa vibali vya biashara hizo baada ya kujihakishia mazingira yatakayotumika kwa biashara hizo pamoja na kuendelea na utoaji wa elimu katika makundi ya wafanyabiashara hizo.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Mei 10, 2023 wakati wa mjadala unaotafuta suluhisho la fungia fungia kumbi za starehe kwa sababu ya kelele chini ya Jukwaa la Mwananchi twitter space, linaloandaliwa kila Jumatano.

Mjadala huo unaakisi uamuzi wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kufungia  jumla ya baa na kumbi za starehe 89 baada ya kupiga kelele na mitetemo iliyozidi viwango husika.

“Kuna wengine wanapewa leseni za biashara wanawekeza hadi Sh20 bilioni lakini baadaye anafuatwa kwa vigezo hizo na kufungiwa, sasa kabla ya leseni waende kukagua. Wakati mwingine unakuta leseni eneo moja watu kumi, hilo ni changamoto na litazamwe,” amesema Maganga.

“Lakini je suala la kelele linanunulika? Kwa nini wengine wanapewa vibali vya matamasha ya mchana? Huo mkanganyiko inabidi utazamwe.”

Katika ufafanuzi wake, Maganga amesema tukio la kufungiwa maeneo hayo lilitengeneza mshtuko pamoja huku likienda kinyume na malengo ya Serikali inayopambania kuweka mazingira bora ya biashara kupitia hatua za kupunguza vikwazo ili wafanyabiashara kufanya kazi kwa amani zaidi.

“Sheria tulizoweka, zimeundwa na Bunge lakini tunaelewa sheria sio lazima zikate kwa makali kama ilivyokuwa kipindi hiki, nimetembelea athari maeneo hayo na hoja zimeelezwa hapa athari zake kiuchumi, ni kubwa athari za moja kwa moja,” amesema Maganga.

“Baa hizi zimeajiri zaidi 5,000, ukiangalia kodi zinazolipwa huko ni kubwa, kodi za kampuni, NSSF. Sasa hatuangalii upande mmoja tu, pale wafanyabiashara wanapokiuka  basi sheria ya 2004 inaelezea hatua gani zifanyike kabla ya kufungia,” amesema

“Kufungia biashara haitakiwi jambo jepesi, ni sheria ichunguzwe. Mwekezaji atakayekuja atajishauri kama taasisi moja inaweza kufungia baa 89 kwa muda mfupi. Sheria zipo hata ya kunyonga lakini miaka zaidi ya 20 hakuna aliyenyongwa, nafikiri busara itumike kulinda mazingira mapana ya biashara.”