Makinda: Wananchi washirikishwe matokeo ya sensa

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anna Makinda

Muktasari:

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari kuhusu matumizi ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa lengo la kuwashirikisha wananchi kuhusu matumizi hayo

Dar es Salaam. Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anna Makinda amevitaka vyombo vya habari nchini kuwashirikisha wananchi matokeo ya sensa ya mwaka 2022 kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo.

Makinda amebainisha hayo leo Machi 13, 2024 wakati wa semina ya uwasilishaji, usambazaji na uhamasishaji wa matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Amesema mchakato wa sensa ulikuwa na hatua tatu muhimu; awamu ya kwanza ya kampeni, awamu ya pili ya kuhesabiwa na sasa ni awamu ya tatu ya matumizi ya matokeo ya sensa, na vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika jukumu hilo.

"Lengo la kuwapa mafunzo haya ni kuona matokeo ya sensa yanawafikia wadau wote wakiwamo wananchi. Hivi sasa ni wakati wa kuwashirikisha wananchi matokeo ya sensa kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo," amesema Makinda ambaye pia ni Spika wa Bunge mstaafu.

Kamisaa huyo amewataka wataalamu kupanga mipango yao kulingana na hali ilivyo katika jamii kwa kutumia takwimu zilizopo katika kufanya uamuzi.

Makinda amesema sekta ya habari inaweza kutengeneza habari nyingi kutokana na takwimu zilizotolewa kwenye sensa ya watu na makazi na kwamba hawahitaji kulalamika kwamba viongozi wa Serikali hawatoi ushirikiano.

"Lengo letu ni wananchi waweze kuzungumza mambo yao ya maendeleo kwa kutumia takwimu. Tunategemea tufike wakati nchi yetu izingumze takwimu, sio tuzungumze majungu tu.

"Waandishi wa habari mmepewa taarifa nyingi za kutengeneza habari, hamhitaji kusema tumenyimwa ushirikiano na Serikali. Takwimu zinakuambia kila kitu, huhitaji kiongozi waseme, rejea yako ni sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022," amesema Makinda.

Amesisitiza waandishi wa habari wakitumia takwimu za sensa, watapata mawazo ya habari za kiuchunguzi kwani zinaibua mambo mengi ambayo hayajulikani kwa wananchi au viongozi wa serikali.

"Hizi takwimu ni utajiri ambao hamjawahi kuona," amesema Makinda huku akisisitiza kwamba ni muhimu wakajiweka vizuri na kujiamini kitaaluma katika kufanya shughuli zao.

Meneja wa Takwimu Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Kapala amesisitiza kwamba uandishi mzuri sio kueleza namba, bali ni kuhusianisha hizo namba na maisha ya jamii husika kwa kueleza na kutafsiri hali halisi.

"Takwimu zinatakiwa zieleze jambo kwenye jamii ili hata mwananchi akiona anapata taarifa muhimu inayomhusu katika mazingira yake," amesema Kapala.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), Samson Kamalamo amewashukuru NBS kwa kutoa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari wa Dar es Salaam huku akiwahakikishia kwamba yataboresha utoani wa habari za kina na zenye weledi.

"Tunawashukuru NBS kwa kutushirikisha DCPC mafunzo haya, nisema mmechagua sehemu sahihi itakayofikisha taarifa za matumizi ya matokeo ya sensa kwa wananchi," amesema Kamalamo.