Makonda ajitetea kutaja majina dawa za kulevya

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Muktasari:

Amesema Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alipigiwa kelele akitakiwa awataje wahusika wa dawa za kulevya lakini yeye aliamua kuacha vyombo vyenye mamlaka vifanye kazi yake.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema uamuzi wa kutaja majina ya watuhumiwa wa biashara na utumiaji wa dawa za kulevya hadharani ulitokana na maombi ya Watanzania wakati wa uongozi wa Serikali iliyopita.

Amesema Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alipigiwa kelele akitakiwa awataje wahusika wa dawa za kulevya lakini yeye aliamua kuacha vyombo vyenye mamlaka vifanye kazi yake.

“Mzee Jakaya mlimpigia kelele... ooh taja, taja, taja taja, sasa tulipoingia sisi tukaona wacha tufanye kama mlivyokuwa mnataka... wakaibuka tena, haaa hapana hiyo siyo busara haa... uliona wapi giza linaondolewa kwa kutumia giza? Aliyefanya mafichoni anawekwa hadharani na harudii tena,” alisema Makonda jana Jumamosi katika semina ya masheikh, wanazuoni, maimamu na walimu wa Qurani Tanzania kupitia Jumuiya ya Walimu Wanaosomesha Qurani Tanzania (Juwaquta).

Alidai kwamba katika mapambano anayoyaendesha dhidi ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, kuna waumini 12 waliokuwa wamepanga njama za kutaka kumtupia majini lakini hawakufanikiwa kutokana na kinga ya maombi kutoka kwa viongozi wa dini.

Alisema waumini hao waliandaa mbuzi mweupe ili kumtoa kafara na aliwatambua kupitia mtandao wake.

Alisema haamini kama waliofanya hivyo walikuwa ni Waislamu, bali kundi la watu waliokuwa wamevaa kanzu kwa utambulisho huo na kwamba huenda walitumika kuwalia watu fedha zao.

Februari 13, Makonda alikabidhi majina 97 ya watuhumiwa dawa za kulevya kwa Kamishna Mkuu wa Tume ya Kudhibiti na Kuzuia Dawa za Kulevya, Rodgers Sianga ili ayashughulike.

Kabla ya kukabidhi majina hayo, alianza kwa kutangaza hadharani orodha ya kwanza ya watuhumiwa hao Februari 3, alianza kwa kutangaza majina 12 wakiwamo wasanii maarufu akiwataka kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kuhojiwa kuhusu mihadarati hiyo.

Februari 8, mkuu huyo wa mkoa alitangaza orodha nyingine ya watu 65 ambayo safari hii iliwajumuisha wafanyabiashara, viongozi wa dini pamoja na wanasiasa.

Mtindo huo wa kutaja majina uliibua mjadala katika jamii wengi wakiupinga kabla ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuufunga kwa kupiga marufuku kutaja majina ya ya watuhumiwa hadharani.

Alirejea kauli yake kwamba baada ya awamu ya tatu, kuna awamu nyingine inakuja ya watu wanaojishughulisha na biashara au matumizi ya dawa hizo.

Pamoja na kupingwa na wengi kwa mtindo wake wa kuwataja watu hadharani, Makonda alisema juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda akisema, “unga sasa umeadimika na hata bei imepanda hawauzi kama njugu tena kwa uwazi, badala yake wanauza kwa kujificha.”

Awali, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum aliwataka Waislamu nchini kubadili mtazamo kwa kufanya kazi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kaulimbiu ya Rais John Magufuli ya “Hapa Kazi Tu”.