Makonda: Kama siyo njaa ningejiuzulu

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amezungumzia kushindwa kujiuzulu nafasi yake kwa sababu ya njaa aliyo nayo. Amesema hata kubali achukuliwe hatua kwa kushindwa kuwasimamia watendaji wa chini yake kwa kushindwa kutekeleza miradi hivyo ameunda kamati maalumu kwa ajili ya kufuatilia miradi yote ya kimkakati katika mkoa wake.

Dar es Salaam. Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amesema kama siyo njaa angejiuzulu nafasi yake ya ukuu wa mkoa ili kuwajibika baada ya Rais John Magufuli kulalamikia ucheleweshaji wa miradi ya ujenzi ya Coco Beach na machinjio ya Vingunguti.

Makonda ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 17, 2019 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwadhamini wanafunzi wa kike 100 wa kidato cha tano wanaosoma masomo ya sayansi lakini wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha.

Kauli hiyo ya mkuu wa mkoa ameitoa ikiwa ni siku moja baada ya Rais Magufuli kumtaka ahakikishe miradi hiyo yenye thamani ya Sh26.47 bilioni inakamilika kwa wakati kwa sababu tayari fedha zipo.

Amesema jana alipata aibu wakati Rais Magufuli alipotembelea machinjio ya Vingunguti na kulalamikia ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo katika mkoa wake licha ya vikao vingi ambavyo amekuwa akifanya na watendaji wa halmashauri na kuagiza kuanza kwa miradi hiyo.

“Jana ilikuwa ni aibu, yaani kwa sababu njaa ni kali, kama siyo njaa leo ilitakiwa niandike barua ya ku-resign (kujiuzulu).”

“Sasa nikifikiria njaa iliyopo huko...naomba sana kila mmoja atimize wajibu wake, ukikwama sehemu waone mamlaka ya juu yako, sio unakaa tu,” amesema Makonda.

Makonda amelalamikia mkoa wake kukwamishwa na wanasiasa kwenye mabaraza ya madiwani kwa maslahi yao.

Amesema mafisadi wengi wako kwenye mabaraza hayo na waligomea ili kutafuta fursa za kufanya ufisadi.

“Huu mkoa una mafisadi wengi hasa huko kwenye mabaraza ya madiwani. Wengi wa wagombea waliingia wakijua watapiga kama awamu nyingine, wakakuta hali ni ngumu kweli kweli,” amesema Makonda.

Kutokana na ucheleweshaji wa miradi hiyo, Makonda amesema anaunda kamati maalumu ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika mkoa wa Dar es Salaam ambayo itahusisha wataalamu mbalimbali wakiwemo maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).