Mama asimulia bintiye alivyonusurika kuuawa

Friday November 27 2020
mama pic
By Mwandishi Wetu

Morogoro. Grace Jacob ambaye ni mama mzazi wa Christina aliyenusurika kuuawa kwa kuchinjwa shingo kwa madai ya ushirikina, amesimulia namna tukio hilo lilivyotokea na alivyonusurika.

Tukio hilo linalodaiwa kufanywa na baba mzazi wa mtoto huyo, Jacob Taholo lilitokea Novemba 15 saa saba usiku katika Kijiji cha Kibedya Wilaya ya Gairo na kumuacha Christina anayesoma darasa la pili na majeraha shingoni, hali iliyosababisha kulazwa kwa siku tano katika Kituo cha Afya Gairo.

Hata hivyo, baba wa mtoto huyo, alifariki dunia akiwa katika Kituo cha Afya Gairo siku moja baada ya kudaiwa kutenda jambo hilo, chanzo cha kifo kikielezwa ni shinikizo la damu.

Grace alisema siku ya tukio mumewe alikwenda matembezi na kurejea nyumbani usiku na alipomfungulia mlango, yeye alikwenda kulala na kumuacha sebuleni wanapolala watoto wao watatu.

Alisema akiwa usingizini aliota kama anakabwa na mume wake, lakini kwa mbali alianza kusikia kilio cha bintiye huyo na za majirani waliokuwa nje ya nyumba hiyo.

“Nilishtuka na kutoka chumbani. Nilimkuta Christina akiwa amelala chini huku akiwa ametapakaa damu mwili mzima zilizokuwa zikitoka kwenye jeraha lililokuwa shingoni,” alisema Grace.

Advertisement

“Baada ya kufanya tukio hilo alikimbia (mumewe) nilipata msaada wa majirani na viongozi wa kijiji kumpeleka mwanangu kwenye kituo cha afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.” Grace alisema hajui sababu ya mumewe kutaka kumchinja bintiye kwa kuwa hawakuwa na ugomvi.

“Mume wangu hajawahi kuugua ugonjwa wa akili. Hadi sasa nashindwa kuelewa kwanini alifanya kitendo hicho,” alisema Grace.

Alisema alichukua jukumu la kurudi kwa wazazi wake kwa sababu ya kuhofia usalama wake kwa kuwa hana mwanamume mwingine wa kuishi naye katika nyumba hiyo.

Mmoja wa majirani wa mama huyo, Janeth Taholo alisema, “kweli sifahamu chanzo cha tukio hilo na wala sijui kwa nini Jacob alifanya hivyo, nilikwenda tu kutoa msaada baada ya kusikia kelele za mtoto.”

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Jackson Mndewahanga alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo alifika eneo la tukio na kukuta majirani huku damu nyingi zikiwa zimetapakaa ndani.

Alisema hatua ya kwanza aliyoichukua ni kumwahisha mtoto zahanati ya kijiji ambako alipatiwa huduma ya kwanza na kupewa rufaa ya kwenda Kituo cha Afya Gairo kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi.

Mndewahanga alisema baada ya mtoto huyo kupokewa katika kituo hicho alirudi kijijini akiwa na sungusungu, ndipo walipomkamata Jacob na kumpeleka ofisi ya kijiji na kuwaita polisi.

Alisema ilipofika alfajili polisi walifika katika ofisi hiyo ya kijiji na kuondoka na Jacob hadi Gairo kwenye makao makuu ya polisi wilaya.

Alisema siku iliyofuata asubuhi alipigiwa simu na mkuu wa upelelezi wa Wilaya ya Gairo na kuambiwa Jacob alishikwa na homa ya ghafla usiku na alipopeleka kituo cha afya, daktari aligundua kuwa na tatizo na shinikizo la chini la damu na wakati wakimpatia matibabu alifariki dunia.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Dk Mshana Dastan alikiri kumpokea na kumpatia matibabu mtoto huyo aliyekuwa na jeraha shingoni.

Advertisement