Prime
Mambo manne yanavyokwaza walimu kazini
Mwenendo wa idadi ya wanafunzi na waalimu kuanzia 2018 hadi 2022, Wanafunzi katika shule za umma wanaongezeka kwa asilimia 16.5 (rangi ya buluu) huku waalimu wakipungua kwa asilimia 7.2 (rangi nyekundu). Imeandaliwa na George Helahela
Dar es Salaam. Wakati walimu duniani wakiadhimisha siku yao leo Alhamisi Oktoba 5, 2023, wa hapa nchini wametaja changamoto nne zinazowakwamisha kwenye utendaji wao, huku wakitaka Serikali kuzitafutia suluhisho.
Changamoto walizotaja ni ukosefu wa makazi, upungufu wa walimu, ucheleweshaji wa stahiki zao na kutokuthaminika ndani ya jamii.
Akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, Mwalimu Samson Sombi wa mkoani Morogoro alieleza kero ya makazi, akisema japo Serikali imejenga baadhi ya nyumba za walimu, bado tatizo ni kubwa.
“Kuna maeneo hakuna kabisa makazi ya walimu, ni muhimu Serikali iendelee na ujenzi wa makazi ya walimu,” alisema.
Kero ya ukosefu wa makazi bora kwa walimu pia imeelezwa na mwalimu wa Shule ya Sekondari Nyumbu, iliyoko mkoani Pwani, Diana Mwakajila akisema ni changamoto kubwa hasa kwa shule zilizoko maeneo ya mjini.
“Kwa mfano hapa tuko walimu zaidi ya 100, lakini nyumba za walimu ziko mbili tu, nani akae nani asikae?” aliuliza Diana.
Mwalimu akiwa darasani. Picha na Maktaba
Mwalimu Joseph Makori aliishauri Serikali, wazazi, walezi na wadau wa elimu nchini kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba za walimu kama inavyofanyika katika vyumba vya madarasa, ili kuwaondolea walimu adha ya kuishi mitaani, tena wakati mwingine mbali kutoka shuleni.
Mazingira magumu ya kazi
Mzigo mwingine unaowakabili walimu ni mazingira magumu ya kazi, huku wakitakiwa kuwaelewesha watoto wote wawe na uelewa kwa usawa.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Tanzania in Figures ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS) ya mwaka 2022, wakati udahili wa wanafunzi ukiongezeka kati ya mwaka 2018 hadi 2022, idadi ya walimu ilishuka kwa asilimia 7.2 kutoka 185,527 mwaka 2018 hadi 172,156 mwaka 2022.
Akizungumzia hali hiyo, mdau wa elimu, Alistidia Kamugisha alisema, “mwalimu kuendesha darasa kubwa, ni vigumu kutoa umakini wa kibinafsi kwa kila mwanafunzi. Hii inaweza kusababisha baadhi ya wanafunzi kutofanya vizuri”.
Takwimu hizo ndizo zinamfanya Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Kagera, Costa Paul kueleza kuwa idadi ya wanafunzi ni kubwa kuliko idadi ya walimu waliopo nchini.
Kwa upande wake, mwalimu Diana wa Pwani alisema changamoto kubwa ni uelewa mdogo kwa wanafunzi wanaotoka shule ya msingi kujiunga na elimu ya Sekondari.
“Siku hizi wanafunzi wanafaulu wengi kutoka shule za msingi, tofauti na zamani, jambo ambalo unakutana na wanafunzi hawana uwezo wa kusoma na kuandika,” alisema Diana.
Alisema changamoto hiyo inawapa jukumu la kuhakikisha wanawatoa katika uwezo wa chini hadi kufika hatua ya kujitambua.
“Kuna ambao wana uwezo, lakini wengine uwezo wao ni wa chini sana, kuna madarasa kama wawili hapa kwetu wanafunzi wanapata ufaulu wa daraja F karibu masomo yote, angalau somo la Kiswahili ndio wanajitahidi,” alisema.
Hata hivyo, mwalimu Lucas Barabara wa Sengerema aliipongeza Serikali kwa kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika shule za umma, huku akishauri nguvu sasa ielekezwe kwenye maboresho ya masilahi kwa walimu na watendaji wa sekta ya elimu.
''Serikali pia iongeze uwekezaji katika vifaa, vikiwemo vitabu vya ziada na kiada,'' alisema.
Kecheleweshewa stahiki
Jambo lingine ni malimbikizo baada ya walimu kupandishwa madaraja, mwalimu Paul alisema walimu wamekuwa wakicheleweshewa malipo yao huku wengine wakicheleweshwa kupandishwa madaraja.
“Kitu hiki kinavunja moyo walimu, uliyeanza naye kazi anapandishwa daraja, mmoja anaachwa utaondoa morali ya kazi,” alisema.
Suala hilo pia limegusiwa na mwalimu Diana akisema; “Kuna wakati malipo yanachelewa mpaka miaka miwili, kuna wakati wakisema lete madai ya likizo unashindwa upeleke madai yapi, sababu unakuta kuna likizo zaidi ya moja hujalipwa,” aliongeza Diana.
Takwimu za walimu
Kwa mujibu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, mwaka 2020, Tanzania ilikuwa na walimu 263,000 wanaofundisha shule za awali, msingi na sekondari.
Pia, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Elimu (Unesco), walimu milioni 69 wanahitajika kufikia lengo la elimu msingi kwa wote kufikia 2030. Uhaba mkubwa ukiwa nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.