Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo yanayokwamisha vita dhidi ya ukatili wa kijinsia haya hapa

Picha na AI

Muktasari:

  • Wadau wa haki za binadamu wameeleza kuwa hofu ya kuripoti matukio, mila kandamizi na mifumo hafifu ya huduma kwa manusura vinaendelea kukwamisha vita dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Dar es Salaam. Mila na desturi kandamizi, hofu ya kutoa taarifa, elimu kuhusu ukatili na uratibu duni wa huduma kwa manusura katika baadhi ya maeneo unatajwa kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyochelewesha juhudi za kukomesha ukatili wa kijinsia nchini.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi, Juni 18,2026 na Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma na Ufuatiliaji wa Haki za Binadamu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Deogratias Bwire wakati wa mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali kujadili mikakati ya pamoja ya kuimarisha ulinzi na upatikanaji wa haki kwa manusura wa vitendo hivyo.

Mkutano huo uliambatana na uzinduzi wa mradi wa 'Haki Zinalindwa' unaolenga kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma kwa manusura wa vitendo hivyo ukianza Wilaya ya Kinondoni na Temeke jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano huo, Bwire amesema licha ya kuongezeka kwa utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa manusura bado baadhi ya matukio hayaripotiwi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mila na desturi kandamizi, pamoja na baadhi ya watu katika jamii kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu ukatili.

“Changamoto kubwa ni kwamba matukio mengi bado hayaripotiwi. Wapo manusura wanaokumbana na vikwazo vya kijamii, kiuchumi, vinavyowazuia kutoa taarifa mapema, hivyo kushindwa kupata haki kwa wakati,” amesema.

Amefafanua wakati mwingine mtuhumiwa ndiye tegemeo la familia, hivyo manusura au ndugu huogopa kutoa taarifa kwa kuhofia athari za kiuchumi. “Hali hii inasababisha wahanga (waathirika) wengi kukosa haki na kuendelea kuishi katika mazingira ya ukatili,” amesema.

Ameongeza kuwa watoto pamoja na wanawake ndio wanaoathirika zaidi, hususan wale waliopo kwenye ndoa au mahusiano, ambapo tafiti zinaonyesha kuwa ukatili unaofanywa na wenza unaendelea kuripotiwa kwa kiwango kidogo licha ya madhara makubwa yanayowapata.

Amesema kwa mwaka 2025, LHRC ilirekodi matukio 268 ya ukatili dhidi ya wanawake huku zaidi ya asilimia 62 ya matukio hayo yalihusisha ukatili wa kimwili au kisaikolojia, jambo linalothibitisha kuwa vipigo na mashambulizi bado ni aina kuu za ukatili dhidi ya wanawake.

Amesema ukatili wa kingono ulihusisha asilimia 31 ya matukio, ukiongezeka kutoka asilimia 25 mwaka 2024, huku ukatili wa kiuchumi ukirekodiwa kwa asilimia 7.

"Matukio mengi yaliripotiwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Morogoro. Hata hivyo, takwimu hizi ni zile tu zilizofuatiliwa na kurekodiwa na LHRC, na hazioneshi ukubwa halisi wa tatizo kitaifa kutokana na changamoto ya kutoripotiwa kwa matukio mengi,” ameeleza.

Pia amesema kwa mwaka 2025 LHRC ilirekodi matukio 25 ya ukatili wa wenza wa karibu na kufanya jumla ya matukio yaliyorekodiwa tangu mwaka 2021 kufikia 184. Kati ya matukio hayo, asilimia 72 yaliishia katika mauaji ya wenza.

Kwa upande wake, Mwanasheria kutoka LHRC, Nancy Masenha amesema kwa kuiona changamoto hiyo wamekuja na mradi wa Haki Zinalindwa unaolenga kukabiliana na changamoto zinazoathiri juhudi za kuzuia na kushughulikia ukatili wa kijinsia (GBV).

Miongoni ni mifumo hafifu ya rufaa kwa manusura, huduma hafifu za msaada wa kisaikolojia, mila na desturi kandamizi, uelewa mdogo wa jamii, pamoja na mapungufu katika mfumo wa sheria na sera za kulinda manusura wa ukatili wa kijinsia.

Amesema kupitia mfumo unaomweka manusura katikati (survivor-centered approach) na ushirikiano wa sekta mbalimbali, mradi wa Haki Zinalindwa unalenga kuimarisha mifumo ya kinga, ulinzi na mwitikio kwa manusura.

Pia kuboresha huduma za msaada wa kisheria na kisaikolojia, kuwawezesha manusura, kuongeza uhamasishaji wa jamii, kuimarisha ushirikiano wa taasisi mbalimbali, pamoja na kufanya utetezi wa maboresho ya sera na sheria.

“Tunahitaji mfumo mmoja wa uratibu unaounganisha watoa huduma wote kuanzia wasaidizi wa kisheria, polisi, wataalamu wa ustawi wa jamii hadi taasisi zinazofuatilia mashauri mahakamani. Hii itasaidia manusura kupata huduma kwa haraka na kwa ufanisi,” amesema.