Mapendekezo kikosi kazi kutathminiwa leo

Muktasari:

  • Tathmini ya mapendekezo ya kikosi kazi inafanyika leo, huku lini na namna gani mchakato wa Katiba Mpya uanze ikitarajiwa kujulikana.

Dar es Salaam. Huenda leo (Mei 26, 2023) ikawa siku itakayozungumzwa kauli ya matumaini na mwelekeo wa utekelezwaji wa Katiba Mpya.

Matarajio hayo yanatokana na kitakachopendekezwa na kikao cha wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa, kinachoketi leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).

Kikao hicho kilichoitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kinafanyika wiki tatu tangu Rais Samia Suluhu Hassan Mei 6, 2023 amwagize kukiitisha.

Pamoja na mapendekezo kuhusu lini na namna gani mchakato wa Katiba Mpya uanze, kikao hicho pia kitajadili maboresho na mabadiliko ya sheria mbalimbali.

Tathmini ya mapendekezo ya kikosi kazi cha Rais Samia kilichoratibu maoni ya wadau kuhusu demokrasia na vyama vingi nchini, ndiyo inayotarajiwa kuwa ajenda mama ya kikao hicho.

Itakumbukwa pamoja na mambo mengine, kikosi kazi hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wake, Profesa Rwekaza Mukandara kilipendekeza mchakato wa Katiba Mpya uliokwama mwaka 2014 kufufuliwa.

Hadi Mwananchi Digital inafika katika kikao hicho, wajumbe mbalimbali walishawasili, akiwemo Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza.

Hata hivyo, hadi saa 2:40 ukumbini hapo hakuonekana mwakilishi yeyote wa vyama vya Chadema wala CCM.

Saa 2:42 Jaji Mutungi aliwasili katika viunga hivyo na kuwapa mkono wajumbe wote waliokuwa wakipata kifungua kinywa.

Imekuwa vigumu wajumbe kueleza matarajio kwa kuwa hakukuwa na ratiba zilizogawiwa, imeelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa AFP, Mark Muhemela.