Mapendekezo Mkoa wa Chato kuwa na wilaya tano

Mapendekezo Mkoa wa Chato kuwa na wilaya tano

Muktasari:

  • Kikao maalumu cha ushauri cha Mkoa wa Geita, kimeridhia kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Chato na kupendekeza mkoa huo mpya kuwa na wilaya tano, huku mkoa mama wa Geita ukibaki na wilaya tano.


Geita. Kikao maalumu cha ushauri cha Mkoa wa Geita, kimeridhia kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Chato na kupendekeza mkoa huo mpya kuwa na wilaya tano, huku mkoa mama wa Geita ukibaki na wilaya tatu.

Kikao pia kimeridhia hifadhi ya Taifa ya Rubondo kutoka Geita na kwenda mkoa mpya wa Chato.

Kikao hicho kilichokuwa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule, kimependekeza mkoa mama wa Geita kubaki na wilaya tatu ambazo ni Geita, Mbogwe na Nyang’wale.

Kikapendekeza pia wilaya ya Sengerema iliyopo Mwanza na Busanda (inayopendekezwa) ziwe sehemu ya Geita.

Mkoa mpya wa Chato umependekezwa kuwa na wilaya ya Chato, Bukombe zilizopo mkoa wa Geita kwa sasa na wilaya mbili za mkoa wa Kagera ambazo ni Biharamulo na Ngara, huku ikimega kata tatu kutoka wilaya ya Muleba pamoja na baadhi ya maeneo kutoka wilaya ya Kakonko iliyopo mkoani Kigoma.

Kuanzishwa kwa mkoa mpya wa wilaya ya Chato kunatokana na ombi la mwakilishi wa wazee wa wilaya ya Chato, Samwel Bigambo, alilolitoa kwa Rais Samia Suluhu Hassan Machi 26, wakati wa mazishi ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli.

Mwakilishi huyo alisema kuwa wakati wa uhai wake, Magufuli aliwaahidi kuwa wilaya ya Chato ingekuwa mkoa.

Kutokana na ombi hilo, Rais Samia alisema mchakato wa Chato kuwa mkoa ulishaanza na aliwataka wawasilishe serikalini hatua za mchakato huo, ili iangaliwe kama wilaya hiyo inakidhi vigezo vya kuwa mkoa.

Alisema kama vigezo vimekidhi suala hilo litakamilishwa, na kama havijakidhi watashauri namna ya kufanya ili vikidhi.

Kulingana na maelezo ya kikao hicho, Mkoa wa Geita utakuwa na tarafa 16, kata 108, vijiji 379 katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 23,697.55 lenye wakazi 2,668,173.

Aidha, mkoa mpya wa Chato utakuwa na tarafa 18, kata 87, vijiji 360 huku ukiwa na ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 30,215.85, lenye watu 1,557,139.

Sinyamule alisema baada ya mapendekezo hayo kukamilika yatapelekwa kwenye wizara husika kwa ajili ya utekelezaji.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Chato, Charles Kabeho alisema kikao cha ushauri cha wilaya kiliomba kuwa na wilaya sita kwa kuzingatia kigezo cha uchumi, hivyo waliomba wilaya pendekezwa ya Busanda na kisiwa cha Rubondo kwenda Chato.

Kwa upande wake, Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Geita, Hadija Said alisema lengo la Rais Magufuli kutaka kuanzishwa kwa wilaya mpya ya Busanda, ilikuwa kuwasogezea wananchi huduma kutokana na umbali wa kufika Nzega iliko halmashauri.

Alisema kwa sasa wananchi wa Busanda wanalazimika kutembea kilomita 83 kwenda Geita kupata huduma, na endapo watapelekwa Chato watalazimika kwenda umbali wa kilomita 195.

Vigezo vya uanzishwaji mkoa

Kwa mujibu wa mwongozo wa Tamisemi wa mwaka 2014, vigezo vya kuzingatia katika kuanzisha mkoa ni pamoja na kuwa na ukubwa wa eneo lenye kilomita za mraba usiopungua 20,000.

Pia kuwa na wilaya nne, idadi ya watu isiyopungua asilimia tatu ya idadi ya kitaifa, tarafa zisizopungua 15, idadi ya kata zisizopungua 45 na idadi ya vijiji visivyopungua 150.

Mapendekezo ya Wilaya ya Chato

Wilaya ya Chato kupitia vikao vya kisheria vya mabaraza ya madiwani na kamati ya ushauri ya wilaya kilichokaa Aprili 16, 2021, iliridhia na kupendekeza jina la mkoa liitwe Chato na makao makuu ya mkoa yawe wilaya ya Chato.

Kikao hicho pia kilipendekeza mkoa mpya wa Chato uundwe na wilaya za Chato, Bukombe, wilaya tarajiwa ya Busanda, Biharamulo, Ngara na kata za Kimwani, Ikuza na Nyakabango za wilaya ya Muleba pamoja na sehemu ya wilaya ya Kakonko iliyopo mkoa wa Kigoma.

Kikao hicho pia kilipendekeza hifadhi ya visiwa vya Rubondo vilivyoko wilaya ya Geita kwenda mkoa mpya wa Chato kwa kuwa huduma nyingi za wakazi wa Rubondo hupatikana Chato.

Mapendekezo ya wilaya ya Bukombe

Kikao cha ushauri cha wilaya ya Bukombe kilichokaa Mei 7, mwaka huu, kilitoa mapendekezo yanayofanana na yale ya wilaya ya Chato.

Mapendekezo ya wilaya ya Geita

Kikao cha baraza la madiwani na kikao cha ushauri cha wilaya kilichokaa Mei 26, mwaka jana kiliridhia kuanzishwa kwa mkoa mpya na kupendekeza wilaya pendekezwa ya Busanda ibaki Geita, ili kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuwa makao makuu ya wilaya yapo kilomita 83 kufika mkoa mama wa Geita na kilomita 195 kwenda mkoa mpya wa Chato.

Wajumbe pia walisema kwa masuala ya kiuchumi, wilaya pendekezwa ya Busanda ndio iliyobeba mkoa wa Geita kiuchumi kwa kuwa na dhahabu, hivyo kwenda Chato, hali hiyo itaiathiri Geita kiuchumi.

Wajumbe walipendekeza kisiwa cha Rubondo kibaki Geita kwa kuwa ni chanzo cha mapato, lakini pia Geita haina hifadhi wala kivutio kingine tofauti na Chato yenye hifadhi za misitu pamoja na hifadhi ya Burigi.

Akizungumza kwenye kikao hicho, mkuu wa wilaya ya Bukombe, Said Nkumba alisema maamuzi yanayofanyika ni makubwa na yatabaki kwenye historia, hivyo ni vema kukafanyika maamuzi ambayo hayaangalii leo au kesho, bali yatakua maamuzi ya kudumu ya muda mrefu.

Mkuu huyo wa wilaya alisema wakati akiwa mbunge wa Sikonge wakati wa kuunda mkoa wa Katavi, wapo waliopinga kwenda Katavi na mkoa ulianzishwa kwa wilaya ya Mpanda na Mlele na baadaye Tanganyika na kutaka wanaoanzisha mkoa wafanye kazi kusimamisha mkoa wao.

Alisema hakubaliani na suala la Busanda kwenda Chato, kwa kuwa mkoa wa Geita bado unahitaji kuimarika kiuchumi na kushauri kisiwa cha Rubondo kwenda Chato, kutokana na sababu za kiusalama na kufikisha huduma karibu na wananchi.

Mwenyekiti wa baraza la madiwani Chato, Batholomeo Manunga aliridhia Busanda kubaki Geita na kisiwa cha Rubondo kwenda Chato kwa kuwa shughuli nyingi zinafanyika Chato na ndiko iliko njia ya kuingia hifadhini kwa ukaribu.