Mapya yaibuka kesi ya Abdul Nondo

Muktasari:
- Ujumbe wa Nondo kwenda kwa Mange, pia ulisema yeye ndiye aliyeongea na baadhi ya vyombo vya habari kuhusuana na kifo cha Akwilina
Iringa. Kesi inayomkabili mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Abdul Nondo, imeendelea leo Mei18,2018 huku shahidi wa upande wa Jamhuri akisema, Nondo aliwasiliana na Mange Kimambi kwa njia ya barua pepe, Februari 25, 2018.
Nondo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSN) alikamatwa Machi, 2018 akidaiwa kudanganya kuwa ametekwa wakati hakutekwa.
Akitoa ushahidi mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, shahidi namba tano katika kesi hiyo, Koplo Abdulkadiri, Ofisa Upelelezi makosa ya mitandao ya kijamii amesema aligundua mshtakiwa Nondo, aliwasiliana na Mange, Mtanzania aishiye Marekani.
Ameiambia Mahakama kuwa baada ya kuifanyia uchunguzi simu ya mshtakiwa aligundua Februari 25, 2o18 Nondo alimtumia ujumbe kwa njia ya barua pepe, Mange na kumwambia kuwa yeye ni Nondo Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania.
Ujumbe wa Nondo kwenda kwa Mange, pia ulisema yeye ndiye aliyeongea na baadhi ya vyombo vya Habari kuhusuana na kifo cha Akwilina.
“Ujumbe huo pia ulisema, amepata tetesi kuwa anatafutwa na watu wasiojulikana na kushauriwa asitembee peke yake kwa sababu ana hati hati ya kutekwa,” amesema shahidi huyo
Shahidi huyo pia ameieleza Mahakama kuwa, Nondo alituma ujumbe kwa Paul Kisabo akiwa Ubungo, uliosomeka: ‘am at risk’ kwa kutumia simu ya mkononi kupitia whatssap.
Kadhalika, shahidi huyo amesema alikuta simu tatu ambazo hazikupokelewa, katika simu ya Nondo. Simu hizo zilipigwa kati ya saa 8 mchana hadi 3; 45 usiku.