Mashine ya kisasa kugundua saratani ya matiti yafungwa Muhimbili

Muktasari:

  • Mashine hiyo, ‘Senographe Pristina 3D Mammography’ yenye thamani ya Sh800 milioni imetolewa na Serikali ya Marekani, itagundua seli ndogondogo zilizoanza kujitengeneza kuwa saratani katika matiti

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefunga mashine mpya yenye uwezo wa juu kugundua saratani ya matiti inayofanya kazi iliyofanywa na mashine nne tofauti.

Mashine hiyo, ‘Senographe Pristina 3D Mammography’ yenye thamani ya Sh800 milioni imetolewa na Serikali ya Marekani, itagundua seli ndogondogo zilizoanza kujitengeneza kuwa saratani katika matiti, huku ikiwa na uwezo wa kuchukua kinyama moja kwa moja iwapo itabaini tofauti katika vivimbe vilivyopo ndani ya titi kwa ajili ya vipimo zaidi.

Takwimu zinaonyesha wanawake 42,000 nchini wanapata saratani ya matiti kila mwaka huku wanaofika katika vituo vya matibabu ni asilimia 38 pekee.

Akizungumza na vyombo vya habari jana katika uzinduzi wa mashine hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohammed Janabi amesema mashine hiyo ina uwezo wa kufanya kazi nne zilizofanywa na mashine zingine za uchunguzi wa magonjwa ambazo ni kipimo cha CT Scan, MRI, X-Ray, ultrasound na mammography wakati wa kipimo cha saratani ya matiti.

Ameeleza utofauti na mashine hiyo inayotarajiwa kupima zaidi ya wanawake 200 kwa mwaka, huku wengine 2,400 wakitarajiwa kunufaika moja kwa moja, alisema haitafanya ugunduzi pekee kwa wagonjwa wa saratani ya matiti.

“Sehemu hiyohiyo tukigundua kwamba kuna uvimbe ambao unatia wasiwasi, pembeni yake kuna mashine inayochukua kinyama. Siyo kama ilivyokuwa unaambiwa kwamba siku nyingine uje uchukue kinyama hii ina faida kubwa."

“Mashine hii ni ya kisasa, sababu itatuwezesha kutazama ziwa katika vipimo vya 2D na 3D hakuna kipande cha ziwa ambacho hatutakiona, pia kuna ultrasound mashine,” amesema.

Profesa Janabi amesema mashine hiyo itawapunguzia kinamama kwenda kufanya kipimo cha MRI kama ilivyokuwa awali kwa kuwa ina uwezo wa kufanya kazi zote.

“Kwa hiyo zile njia zote tatu zinazotumika duniani kuweza kubaini tatizo la saratani zitafanyika katika chumba kimoja hapa hospitali ya Taifa, maana yake ni kwamba tunaweza kukufanyia kama tuna wasiwasi wa vipimo vyote vitatu na tukawa tumemaliza."

“Kwa utaalamu uliopo katika mashine hii, hatuwezi kuikosa saratani kama ipo. Pia huhitaji kufanya vipimo vyote vitatu lakini pale itakapobidi kwa kuona kwenye historia au pale tutakapopima na kubaini kuna shida kama tumekosa sehemu ya kwanza tutahamia nyingine,” amesema.

Kwa mujibu wa Profesa Janabi, gharama za mashine hizo bado hazijawekwa rasmi kwa wale watakaotaka kupimwa bila kufuata utaratibu wa rufaa na kwa sasa wanawasiliana na watu wa bima.

"Bima tumeanza mazungumzo nao kwa sasa kuhusu wachangiaji kulipia kipimo hiki, tumefikia pazuri tutakamilisha na bei itapangwa. Yeyote atakayepimwa wiki hizi mbili mashine hatalipia chochote ni kuangalia inafanyaje kazi, namna ya kupima na wataalamu wetu kupata ujuzi. Gharama haitakuwa kubwa itakua chini ya zile za CT Scan."

Amesema mashine hiyo imefungwa Muhimbili kwa kuwa ndiyo yenye jukumu ya kupima na kubaini saratani kupitia kitengo chake cha Patholojia kabla ya wagonjwa kuhamishiwa Ocean Road.

Naye Mkurugenzi Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea amesema uwepo wa mashine hiyo ni matokeo ya ushirikiano ambao Serikali imeujenga miongoni mwa wadau mbalimbali, hivyo ni hatua kubwa ya matibabu ya saratani ya matiti nchini.

Amesema duniani kila mwaka wanawake milioni 2.3 hugundulika na saratani ambapo kwa Tanzania Shirika la Afya Duniani linakadiria kuwa wanawake 42,000 hupata saratani kila mwaka, lakini wanapofika vituo vya afya kwa ajili ya matibabu ni asilimia 38 pekee.

Amesema Serikali imejitahidi kuongeza vipimo ngazi za chini vinavyoweza kubaini saratani mapema kuna vipimo vingi vinavyoweza kufanyika, hata wataalamu pia wamekua na werevu zaidi.

"Mashine hii haitafanya tiba pekee yake lakini kufundishia wataalamu, hivyo tunaamini utaalamu utaenda mpaka hospital nyingine, pia itatumika kwa ajili ya utafiti," amesema Dk Mambea.

Amesema ushirikiano uliopo unasaidia kupata teknolojia mpya, itakayowezesha kuifikisha nchi kuwa na mashine kama hizo nyingi na Wizara ya Afya inaunga mkono juhudi zinazofanywa na Muhimbili.

Mashine hiyo imetolewa na Serikali ya Marekani kupitia Radiological Society of North America (RSNA) na GE Healthcare.

Mkurugenzi wa RSNA, Meredith McNeil amesema wameiweka mashine hiyo Muhimbili ikiwa ni mpango wa kuendesha mafunzo kwa wataalamu wa afya ili waweze kufundisha wataalamu wengine kufanya uchunguzi wa mammografia,kabla hazijaenda katika vituo vingine.

“Mashine hii uchunguzi wake ni bora zaidi, usio na uchungu, usioogopesha na rahisi kukubalika na mgonjwa. Hiyo pia itakuwa fursa kwa wanawake kuzungumza kuhusu uzoefu wao katika kipimo hiki kwa mama zao, binti zao, dada zao na marafiki na kubadilishana uzoefu chanya, hivyo kuleta mwamko wao wa kupima na kugundulika katika hatua za awali za ugonjwa,” amesema McNeil.