Mashirika 40 kuadhimisha siku ya mtoto wa kike duniani

Muktasari:

  • Mashirika 40 yameungana na Taasisi ya Jakaya Kikwete kuzindua wiki kazi ikiwa ni maandalizi ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike dunia inayofanyika kila Oktoba 11 ya kila mwaka.

Dar es Salaam. Muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali 40 (TCACL), yakishirikiana na Taasisi ya Jakaya Kikwete wamezindua rasmi wiki kazi ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto wa kike dunia inayoadhimishwa Oktoba 11 kila mwaka.

Mashariki hayo yanajishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo kutetea na kupinga utumikishwaji kazi haramu kwa watoto. Pia yamekuwa mstari mbele kuhimiza jamii kubadili mtazamo kuhusu ajira kwa watoto kupitia matamasha na mikutano.


Mratibu Mkuu wa siku ya mtoto wa kike duniani, Radhia Malla amewaambia wanahabari leo Oktoba 5, 2021 jijini Dar es Salaam, kuwa wamekubaliana kuadhimisha siku hiyo wiki nzima kuleta hamasa kwa jamii na kutoa elimu katika maeneo ya vijijini ya mkoani Pwani.

Malla amesema shughuli hizo watazifanya Oktoba 10 katika wilaya za Kibiti, Chalinze na Mkuranga. Amesema kutanguliwa na shughuli za uhamasishaji, utoaji elimu, mafunzo na ugawaji wa vifaa vya usafi wa mwili kwa watoto wa kike waishio mazingira magumu katika wilaya ya Chalinze na  Mkuranga.

“Kilele cha siku hii ya kimataifa itakayoadhimishwa Oktoba 11 itafanyika Kibiti ili kutambua thamani, kuongeza hamasa ya ushiriki wa mtoto wa kike katika tasnia ya kidigitali licha ya changamoto wanazozipitia hasa maeneo ya vijijini.

“Kauli mbiu ya maadhimisho haya kitaifa ni ‘kizazi cha kidijitali, kizazi chetu’ tunaungana na Serikalikuikumbusha jamii kutoa haki sawa kwa watoto wote kwenye teknolojia ya kidijitali ili kuitumia kwa maendeleo na ustawi wao,” amesema Malla.

Katika mkutano huo, uliohudhuriwa pia na Janet Sewava ambaye ni mhitimu kidato cha sita aliyeanza kujishugulisha na teknolojia ya kidigitali akiwa sekondari, ambapo amesema tasnia yateknolojia ipo kwa ajili yao, na ina mambo mengi wanayoweza kufaidika nayo.