Masoko 14 ya kimataifa kwa wakulima wa Tanzania haya hapa

Muktasari:
Nchi 14 zilizofungua masoko ya mazao ya kilimo kwa Tanzania ni pamoja na wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU), Marekani, Zambia, Pakistan, Afrika Kusini, India, Brazil, Mexico, Singapore, China, Malaysia, Canada, Uturuki, Iraq, na Israeli.
Dodoma. Wakulima wa Tanzania sasa watakuwa na fursa ya kuyafikia masoko ya kimataifa kwenye 14 duniani yenye thamani ya takriban dola bilioni 3.4.
Nchi hizo ni pamoja na wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU), Marekani, Zambia, Pakistan, Afrika Kusini, India, Brazil, Mexico, Singapore, China, Malaysia, Canada, Uturuki, Iraq, na Israeli.
Mazao yatakayopokelewa katika nchi hizo ni pamoja na parachichi, vanilla, pilipili manga, nanasi, karafuu, kakao, ndizi, na viazi mviringo.
Hayo yamebainishwa katika nakubaliano yaliyofikiwa Septemba 18, 2024 jijini Dodoma, kati ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) kupitia mradi wake wa STREPHIT unaotekelezwa na kwa ufadhili kutoka Umoja wa Ulaya (EU).
Akizungumza katika makubaliano hayo, Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde amesema hatua hiyo ni ya kimabadiliko katika kufungua masoko mapya nje ya nchi.
“Makabidhiano haya ni hatua muhimu kwa sekta ya kilimo ya Tanzania,” amesema Silinde kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Ameongeza, “Kwa kutimiza mahitaji ya soko ya nchi hizi 14, tunaunda fursa kwa wakulima wetu, hususan wale wanaolima mazao ya kipaumbele, kufikia masoko mapana ya biashara, kuboresha maisha yao, na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika soko la kimataifa.”
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo wa Zanzibar Shamata Shaame Khamis, aiyewakilishwa na Idrisa Abdallah, Katibu Mkuu Msaidizi wa Wizara ya Kilimo Zanzibar, amesisitiza umuhimu wa hatua hiyo kwa mauzo ya nje ya kilimo ya Zanzibar, hususan kwa karafuu, ambayo ni moja ya mazao makuu ya kisiwa hicho.
“Kupata ufikiaji wa sehemu hii kubwa ya soko la kimataifa hakika kutawanufaisha wakulima wetu na kuimarisha sekta yetu ya kilimo inayochangia takriban asilimia 85 ya mapato ya mauzo ya nje Zanzibar na asilimia 27 ya pato la Taifa,” alibainisha.
Mradi wa Kuimarisha Huduma za Afya ya Mimea Tanzania kwa Usalama wa Chakula Ulioboreshwa (STREPHIT) unalenga kuhakikisha kuwa bidhaa za kilimo za Tanzania zinakidhi viwango vya kimataifa.
Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Asilia katika Ujumbe wa EU kwa Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Lamine Diallo, amesisitiza kujitolea kwa jumuiya hiyo katika kusaidia sekta ya kilimo ya Tanzania.
“Maendeleo ya taarifa hizi za soko yanaonyesha kujitolea kwa Umoja wa Ulaya kuboresha viwango vya usalama na afya, kuongeza upatikanaji wa masoko, na kuhimiza uwekezaji katika bidhaa za kilimo za Tanzania. Hii itachochea ukuaji wa biashara ya mauzo ya nje na kunufaisha kilimo cha Tanzania na wakulima,” amesema.
Naye, Mkurugenzi mkaazi wa FAO nchini, Dk Nyabenyi Tipo aliyewakilishwa na Mshauri wa Kiufundi wa shirika hilo, Dk Monday Ahonsi amepongeza makubaliano hayo.
“Mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja chini ya mradi wa STREPHIT, unaolenga kuimarisha huduma za afya ya mimea za Tanzania ili kufikia viwango vya afya ya mimea vinavyohitajika na masoko ya kimataifa,” amesema.