Matumizi ya P2 yawashtua wabunge

Muktasari:

Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi imebaini ongezeko la matumizi ya vidonge vya kuzuia mimba (P2) miongoni mwa wasichana hasa wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 24, jambo ambalo ni hatarishi kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi imebaini ongezeko la matumizi ya vidonge vya kuzuia mimba (P2) kwa baadhi ya wasichana hasa wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 24, jambo ambalo ni hatarishi kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

 Hayo yamesema leo Alhamis Februari 10, 2022 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatma Tawfiq wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa kipindi cha kati ya Januari mwaka 2021 hadio Februari mwaka 2022.

“Licha ya kuwa na lengo la kuzuia mimba, matumizi ya vidonge hivi ambavyo vimekuwa vikiuzwa kwa bei ya chini yamekuwa yakichochea maambukizi ya Virusi vya Ukimwi,”amesema.

Amesema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, baadhi ya wasichana wamekuwa wakiogopa zaidi mimba kuliko maambukizi ya VVU na hivyo wamekuwa wakitumia vidonge vya P2 kama njia mbadala ya kuzuia mimba na kuacha kutumia kondomu ambazo zingewakinga dhidi ya maambukizi ya VVU na magonjwa ya ngono na mimba zisizotarajiwa.

Amesema ili kukabiliana na tabia hiyo hatarishi, kamati inashauri kwamba wakati wa mauzo ya dawa za kuzuia mimba (P2) ni vizuri zikauzwa pamoja na kondomu kwa lazima ili kuwawezesha wasichana kuwa na tabia ya kutumia kondomu hizo bila ya kunyanyapaliwa.

Amesema uzoefu unaonyesha iwapo watakuwa na hizo kondomu basi wasichana wengi watazitumia ili kupunguza maudhi na madhara ya dawa za kuzuia mimba.

“Dawa hizi huharibu mzunguko wa hedhi na mfumo wa hormone za wasichana. Mara nyingi wasichana wakitaka wavulana watumie kondomu huwa wanapata tatizo la upatikanaji wake kwa kuwa maduka ya dawa yenye kuuza kondomu yanakuwa yamefungwa wakati wa usiku,”amesema.

Amesema matumizi ya kondomu huwa hayapendwi na wavulana kwa kuwa wanajua wasichana watatumia dawa za kuzuia mimba ambapo huchangia kasi kubwa ya tabia hatarishi inayopelekea kupata maambukizi mapya kwa vijana hususani wasichana.

“Ununuaji wa kondomu na dawa ya P2 kwa pamoja utasaidia kupunguza unyanyapaa miongoni mwa vijana na kusaidia kufanya utafiti wa maambukizi ya VVU kwa wasichana,”amesema.