Mauzo ya sangara nje yaporomoka, ya ndani kicheko

Dar/Mwanza. Wakati taarifa ya hali ya uchumi ya mwaka 2022 ikionyesha mauzo ya samaki aina ya sangara nje ya nchi yamepungua, matumizi ya ndani yanaelezwa kuongezeka.

Taarifa hiyo inaonyesha mauzo yamepungua kwa zaidi ya asilimia 30. Mwaka 2019 ziliuzwa tani 32,609 zenye thamani ya Sh400.2 bilioni, wakati mwaka 2020 ziliuzwa tani 24,173 zenye thamani Sh302.3.

Kwa mwaka 2021 taarifa inaonyesha ziliuzwa tani 21,846 zenye thamani ya Sh337.1 bilioni, huku mwaka 2022 zikiuzwa tani 21,647 sawa na Sh375.4 bilioni.

Taarifa hiyo inaonyesha mauzo hayo ya sangara kwa miaka minne nje ya nchi yaliiingizia Serikali Sh49.9 bilioni kama mapato yatokanayo na ushuru.

Hata hivyo, takwimu za mauzo ya sangara nje ya nchi zimekuwa zikipanda na kushuka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, kiwango cha juu cha mauzo nje ya nchi katika muongo uliopita ni mwaka 2013 ambapo ziliuzwa tani 33,733.

Maoni ya wadau

Baadhi ya wadau ambao Mwananchi imezungumza nao kujua chanzo cha kushuka kwa mauzo ya sangara, wameeleza matumizi ya kitoweo hicho yameongezeka nchini na wengine wakisema uvuvi harama unachangia.

Mmiliki wa mgahawa wa Afrikando uliopo Mwananyamala jijini Dar es Salaam, Fred Uisso anayeuza sangara kwa wingi alisema ana wateja wengi hivi sasa ambao anaamini wametambua samaki huyo ana virutubisho bora zaidi ikilinganishwa na wengine.

“Sangara wakiingia mjini hawachukui muda, wanaisha haraka. Ulaji umeongezeka sana," alisema Uisso.

Alisema bei ndogo ya sangara na elimu ambayo watu wameanza kupata kuhusu umuhimu wa samaki huyo mwilini ni miongoni mwa sababu za mahitaji kuongezeka.

"Bei ya sangara kutoka kwa wasambazaji ni kuanzia Sh8,000 mpaka Sh10,000 kwa kilo moja, tofauti na samaki wengine kama sato ambao bei ni juu zaidi," alisema Uisso.

Alisema sangara wana kiwango kikubwa cha mafuta ya Omega 3 ambayo ni muhimu zaidi kuliko ya Omega 6 yanayopatikana kwa sato na aina nyingine ya samaki.

Wataalamu wa masuala ya lishe wanabainsiha kuwa mafuta ya Omega 3, husaidia sana kurudisha kumbukumbu kwa watu wazima ambao umri wao umeenda na kusaidia kuongeza kinga mwilini.

Yanasaidia kupambana na msongo wa mawazo na kumwepusha mtu kuwa na huzuni, kukata tamaa ya maisha au kuongea peke yake.

Husaidia afya ya macho na husaidia mtu asipate matatizo ya kansa.

Omega 3 pia huwafaa wajawazito, kwani husaidia katika ukuaji wa ubongo wa mtoto aliye tumboni na hata akizaliwa ni vizuri mtoto anapofikia umri wa kula akawa anapewa vyakula vyenye Omega 3, kwani yatamsaidia kukua haraka, kuwa na busara, kuwahi kuongea na kuwa na akili.

Husaidia afya ya macho na husaidia mtu asipate na matatizo ya kansa. Pia, mafuta hayo husaidia mtu kupata usingizi mzuri na kuwa na ngozi nzuri.

Pia husaidia mtu asipate matatizo ya moyo na hudhibiti mafuta mabaya kwenye ini.

Faida nyingne husaidia mwanamke kutopata maumivu wakati wa hedhi.

Mfanyabiashara wa sangara eneo la Ubungo, jijini Dar es Salaam, aliyejitambulisha kwa jina la Anko Msele alisema ulaji wa samaki hao umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na idadi ya wateja anaowahudumia.

Msele aliyesema huhudumia wateja kati ya 75 na 100 kwa siku, alisema kwa sasa hata upatikanaji wa sangara umepungua.

“Kwa sasa huwezi kulinganisha na miaka ya nyuma, wateja wa sangara ni wengi kuliko sato, ukizingatia hata bei yake ni rafiki kwa watu wa matabaka yote tofauti na sato ambao bei yake iko juu na hupendelewa na watu wa tabaka fulani,” alisema Msele.

Alisema huuza sangara kwa Sh8,000 kwa kilo moja ijapokuwa kuna kipindi bei hupanda, lakini haizidi Sh10,000, huku sato huanzia Sh12,000 kwa kilo.

Mohammed Yusuph, mkazi wa jijini Mwanza ambaye ni msambazaji wa sangara nchini alisema samaki hao wameadimika kutokana na ulaji kuongezeka.

“Hali ni tofauti sana ikilinganishwa na siku za nyuma, sasa hivi watu wanakula sana sangara. Uhitaji mkubwa umesababisha kuadimika kwa sangara, kwa hiyo siyo ajabu kusikia mauzo yamepungua nje kwa sababu ya uhitaji kuwa mkubwa nchini,” alisema Yusuph.

Alisema husambaza sangara katika mikoa mingi, ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam ambako hupeleka tani mbili mpaka tano na hufanya biashara mara mbili kwa wiki.

Kwa mikoa ya Dodoma na Arusha anasema hupeleka tani mbili kwa kila mkoa, mara moja kwa wiki.

Maduka ya kuuza samaki yako katika maeneo mbalimbali na hata bucha za nyama pia zimekuwa zikitumika kuuza kitoweo hicho.

Serikali

Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdallah Ulega alipowasilisha hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24 bungeni Mei, mwaka huu, alisema wizara imeandaa vijarida sera viwili kuhusu hitaji la kuongeza kiwango cha upatikanaji wa sangara kwenye Ziwa Victoria na matumizi ya satelaiti kwa shughuli za uvuvi kiuchumi, vitakavyosaidia Serikali kufanya uamuzi katika usimamizi wa rasilimali za uvuvi.

Pia alieleza mikakati ya Serikali katika kahakikisha kiwango cha mauzo ya samaki nje ya nchi kinaongezeka.

“Katika mwaka 2023/24, Wizara itaviwezesha vituo 11 vya udhibiti ubora, viwango na masoko ya mazao 111 ya uvuvi kwa kufanya kaguzi 9,200 na kutoa vyeti vya afya 12,000 kwa ajili ya usafirishaji wa samaki na mazao yake nje ya nchi,” alisema Ulega.

Alisema Wizara itaendelea kudhibiti ubora na usalama wa mazao ya uvuvi ili kuendelea kukidhi viwango vya masoko ya samaki na mazao yake nje ya nchi.

Bajeti ya wizara hiyo ilionyesha hadi Aprili mwaka huu, jumla ya tani 183 za sangara ziliuzwa nje ya nchi, zikiwa na thamani ya Sh2.8 bilioni wakati ushuru uliolipwa ukiwa ni Sh122 milioni.

Hata hivyo, ripoti ya mapitio ya uchumi ya kila mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Juni inaonyesha mauzo ya samaki na bidhaa za samaki nje ya nchi yameongezeka kwa mwaka mmoja kutoka tani 133.5 Mei mwaka jana hadi tani 191.6 Mei mwaka huu.

Kauli ya wavuvi

Akizungumza na Mwananchi Juni 30, mwaka huu kuhusu upungufu huo, Katibu wa Umoja wa Wavuvi Tanzania (Tafu), Jephta Machandalo alisema uvuvi haramu wa sangara ndani ya Ziwa Victoria una mchango mkubwa katika upungufu wa mauzo yake nje ya nchi.

"Kumekuwa na ongezeko la wavuvi wa dagaa ambao badala ya kutumia nyavu zao kuvua dagaa wanazitumia kuvua sangara na sato. Ndiyo maana siyo ajabu tena kukuta sokoni kuna sangara na sato walioko chini ya sentimita 25," alisema Machandalo.

Alitaja kuongezeka kwa mahitaji ya samaki ikilinganishwa na upatikanaji wake katika jamii kuwa kunasababisha uhaba huo.

Sababu nyingine alisema ni kukosekana kwa miongozo na kanuni zinazodhibiti na kuratibu shughuli za uvuvi wa Sangara.

"Tunahitaji kanuni zinazoweka wazi kuwa mvuvi wa dagaa akikutwa na sato, sangara au aina nyingine ya samaki anachukuliwa hatua gani. Ukiingia kwenye mwalo wa dagaa utakuta sangara na sato, ukiwauliza wavuvi wamewavua kwa njia gani wengi watakwambia kwa kutumia nyavu za dagaa," alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Umoja wa Viwanda vya Samaki (TIFPA), Onesmo Sulle alisema upungufu wa biashara ya samaki ndani na nje ya nchi umesababishwa na kuruhusiwa kwa biashara ya mabondo.

Alisema biashara hiyo ambayo alidai katika soko la dunia inauzwa hadi Sh230,000 kwa kilo imesababisha wavuvi kutumia mbinu haramu kuwinda samaki aina ya sangara kwa lengo la kujipatia bondo.

"Serikali iweke utaratibu unaoeleweka wa biashara ya bondo kwa wavuvi na wafanyabiashara ili kuepuka visa vya wavuvi kumwaga sumu na kuua samaki hata ambao hawajafika muda wa kuvuliwa kwa lengo la kupata bondo," alisema Onesmo.

Mbali na uhitaji wa bondo, Onesmo alisema juhudi za kulinda mazalia ya samaki hazijafanyika ipasavyo na matumizi ya taa za nishati ya jua katika uvuvi wa dagaa yamechangia kupunguza mazalia ya samaki ndani ya Ziwa Victoria.

"Uvuvi haramu na mahitaji ya bondo kupita kiasi umechangia kupunguza rasilimali za viwanda vya samaki Kanda ya Ziwa, matokeo yake uzalishaji nao umepungua na uzalishaji ukipungua hata ajira za ndani na nje ya viwanda zinapungua," alisisitiza.

Mwaka 2018 wizara hiyo ilianzisha ‘Operesheni Sangara’ iliyolenga udhibiti wa uvuvi haramu ambao husababisha upungufu mkubwa wa samaki, uharibifu wa matumbawe ambayo ni mazalia ya samaki na kuharibu ikolojia ya viumbe wa majini.

Hata hivyo, kuliibuka malalamiko kutoka kwa wavuvi kuhusu namna operesheni hiyo ilivyotekelezwa, ikielezwa ilikiuka misingi ya haki za binadamu kwa kuwa utekelezaji wake uligubikwa na vitisho, ubabe na viashiria vya rushwa.

Malalamiko yaliyowasilishwa bungeni wakati huo yalihusisha masuala ya kuchomwa kambi za wavuvi, nyavu na mitumbwi; kutaifisha nyenzo za uvuvi na mali nyinginezo za wavuvi.