Mbarawa aanza kazi Uwanja wa Msalato

Mbarawa aanzia kazi Uwanja wa Msalato

Muktasari:

  • Awamu ya kwanza ya ujenzi wa Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato jijini Dodoma utakaowezesha abiria milioni 1.5 kuhudumiwa kwa mwaka utakamilika baada miezi 36.

Dodoma. Awamu ya kwanza ya ujenzi wa Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato jijini Dodoma utakaowezesha abiria milioni 1.5 kuhudumiwa kwa mwaka utakamilika baada miezi 36.

Hayo yalisemwa jana na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanrods), Rogatus Mativila wakati wa hafla ya utiliaji saini wa mktaba wa ujenzi wa uwanja huo jijini Dodoma.

Mkataba huo ulisainiwa na Tanroads na Kampuni iliyoshinda zabuni ya kujenga uwanja huo ya Synohydro Company Limited na kushuhudiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.

Mativila alisema ujenzi huo utakuwa wa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa barabara za kuruka na kutua ndege na majengo likiwemo la abiria.

“Awamu ya kwanza itakapokamilika kiwanja hiki kitakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka. Awamu ya pili itatekelezwa kwa kutegemea mahitaji yatakayojitokeza ndani ya kipindi cha miaka 20 baada ya ujenzi wa awamu ya kwanza kukamilika,” alisema.

Alisema mradi huo unatekelezwa kwa ufadhili wa mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) ambayo itatoa dola za Marekani milioni 329.47 na Serikali ya Tanzania Sh127 bilioni.

Alisema fedha zitakazotolewa na Serikali ni pamoja na fidia kwa ajili ya wananchi watakaopisha mradi huo, zikiwemo zaidi ya Sh14 bilioni ambazo zimetumika kulipa fidia watu 1,777 huku watu 28 wakiwa bado hawajajitokeza.

Akizugumza katika tukio hilo la kwanza tangu aapishwe kushika nafasi hiyo, Profesa Mbarawa aliitaka Tanroads kusimamia mradi huo kwa viwango vinavyotakiwa kwa sababu wananchi walisubiri kwa muda mrefu ujenzi huo.