Mbarawa awaagiza Latra kufanyia utafiti ongezeko la ajali
Muktasari:
- Ripoti ya Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA), imefichua kuwa watu 3,609 wamepoteza maisha katika ajali za barabarani kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, huku vikionekana kupungua kwa asilimia 8.31 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.
Arusha. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameiagiza mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kufanya utafiti na kuwasilisha majibu ya utatuzi wa wingi wa ajali za barabarani nchini.
Mbarawa ametoa maagizo hayo leo Desemba 6, 2023 alipotembelea banda la mamlaka hiyo, katika maonyesho yaliyofanyika sambamba na mkutano wa 16 wa wadau wa uchukuzi, unaoendelea jijini hapa.
Profesa Mbarawa amesema kuwa wingi wa ajali nchini unatishia nguvu kazi ya Taifa, lakini pia unanyong'onyeza juhudi za Serikali katika uwekezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kuwapatia vijana ajira.
"Ajali zimekuwa nyingi sana, awali mlileta ajenda kuwa mwendokasi ndio chanzo na mkaleta suluhu kuwa kifungwe kitufe cha kupiga kelele pale dereva anapozidisha mwendo, lakini mnaona bado ajali ni nyingi.
"Sasa rudini tena kazini kachunguzeni upya chanzo cha ajali hizi maana kila kukicha inazidi kupunguza nguvu kazi ya Taifa mje na majibu," amesema.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA), watu 3,609 wamepoteza maisha katika ajali za barabarani kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, huku vikionekana kupungua kwa asilimia 8.31 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.
Akizungumzia swala hilo, Mkurugenzi Mtendaji Latra, Habibu Suluo amesema kuwa wamegundua kuwa ajali nyingi zinatokea usiku, hivyo wanatarajia kuwekeza nguvu zaidi za utafiti katika eneo hilo.
Amesema vyanzo vingine vya ajali mbali na uchovu lakini pia kupasuka kwa tairi, mwendokasi na uzembe wa madereva.