Mbaroni akidaiwa kuiba mtoto

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Wilibroad Mtafungwa
Muktasari:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Wilibroad Mtafungwa alisema jana kuwa mtuhumiwa huyo alimwiba mtoto huyo Desemba 17 saa sita mchana.
Njombe. Polisi wanamshikilia mkazi wa Mjimwema Makambako kwa tuhuma za wizi wa mtoto wa kiume mwenye umri ya miezi mitatu katika Hospitali ya Kibena, Njombe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Wilibroad Mtafungwa alisema jana kuwa mtuhumiwa huyo alimwiba mtoto huyo Desemba 17 saa sita mchana.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa usiku wa kuamkia jana baada raia wema kutoa taarifa polisi kutokana na kumtilia shaka la kumuona na mtoto ghafla bila ujauzito.
“Wananchi wa Makambako walisikia mtoto analia nyumbani kwa mama huyo wakati hawakumuona akiwa mjauzito...baada ya kuhojiwa na polisi mama huyo alikiri kuiba huyo mtoto,” alisema Kamanda Mtafungwa.
Alisema mtuhumiwa huyo alikwenda hospitalini hapo na kumuona mama wa mtoto huyo akiwa na mwanaye.
“Mtuhumiwa huyo alimuomba mama huyo amwachie mwanaye amsaidie kumbeba atakapoingia wodini kumwona mgonjwa.
Alipotaka kuingia wodini alimwanchia, lakini baada ya kuingia tu ndipo akapata mwanya wa kuondoka na mtoto,” alisema.
Mama wa mtoto huyo, Irene Kayombo ambaye ni mkazi wa Mtaa National Housing, alisema mama huyo alifika hospitalini na kumzoea ghafla.
“Nilipotoka wodini sikumuona yule mama nikamwambia mama mkwe kwamba aliyeniomba mtoto amshike simuoni ndipo tukaanza kumtafuta hapo hospitalini bila mafanikio, lakini tukatoa taarifa polisi,” alisema Kayombo.
Baba wa mtoto, Alex Makweta alisema alipata taarifa za kuibiwa mtoto wake baada ya kupigiwa simu na kaka yake.
“Kwa kweli nilipata mshtuko baada ya kaka yangu kunipigia simu nikiwa kwenye mizunguko ya kazi, nikawahi Kibena (hospitali) nikakuta kweli mtoto kaibiwa ndipo tukashauriana na kutoa taarifa polisi,” alisema Makweta.