Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbaroni akidaiwa kumuua mzee aliyelala msibani

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro linamshikilia Godbless Kawiche (26), mkazi wa Kitongoji cha Faru, Kata ya Njia Panda kwa tuhuma za mauaji ya mzee mwenye umri kati ya miaka 70-75 kwa kumkatakata na panga akiwa amelala msibani.

Moshi. Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia Godbless Kawiche (26), mkazi wa Kitongoji cha Faru, kata ya Njia Panda, wilayani Moshi kwa tuhuma za mauaji ya mzee wa Kimaasai mwenye umri kati ya miaka 70-75 kwa kumkatakata na panga akiwa amelala msibani.

Mtuhumiwa huyo ambaye ni fundi ujenzi anadaiwa kufanya mauaji hayo juzi Januari 18, 2024 baada ya kuanzisha vurugu na kuwafukuza waombolezaji waliokuwepo kwenye msiba wa kaka yake, aliyefia nchini Kenya Januari 16.

Katika vurugu hizo, ndipo alimvizia mzee huyo akiwa usingizini na kufanya tukio hilo, kisha kumchoma moto sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Abel Mtagwa amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa jana Januari 19 baada ya kufanyika msako mkali na kwamba wanamshikilia kwa mahojiano zaidi na taratibu za kisheria zitakapokamilika atafikishwa kwenye vyombo ya sheria.

"Ni kweli tumemkamata mtuhumiwa huyu wa mauaji, taratibu za mahojiano zinaendelea," amesema Kamanda Mtagwa.

Akielezea tukio lilivyotokea, Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Erasmus Assey amesema kabla ya mauaji hayo kijana huyo alianza vurugu msibani hapo na kuwafukuza waombolezaji wote waliokuwepo msibani kisha kutekeleza mauaji hayo wakati mzee huyo akiwa amelala kwenye chumba cha kijana huyo.

"Kuna familia moja ilipata msiba wa kijana wao aliyefia nchini Kenya, ambapo alipata ajali iliyosababishwa na shoti ya umeme wakati akiwa kwenye shughuli zake ambapo alidondoka na kukonga kichwa chini na kufariki siku ya Jumanne Januari 16," amesema Assey.

"Tukiwa kwenye msiba, tunasubiri mwili kwa ajili ya maziko siku ya Jumamosi, palikuwa waombolezaji hapo nyumbani waliofika kuifariji familia, sasa usiku huyu kijana (mdogo wa marehemu), alikuwa akifanya vurugu na kuanza kuwafukuza waombolezaji na majirani waondoke, alifanya vurugu kubwa akaanza kuvunja viti na mali nyingine."

Amesema waombolezaji waliolala msibani hapo waliweza kumdhibiti na kumzuia kuendelea na vurugu hizo, lakini baadaye alizidisha vurugu, hali ambayo iliwafanya hata wazazi wake kuondoka na kwenda kuomba hifadhi nyumba jirani.

"Wakati waombolezaji wameondoka, huyu mzee ambaye ni wa jamii ya Maasai alikuwa amelala chumbani kwa huyu kijana, kwa hiyo baada ya watu wote kuondoka ndio akapata nafasi ya kumuua huyu mzee, na baadaye alimchoma moto sehemu mbalimbali za mwili wake," amesema Assey.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, Polisi walipofika eneo la tukio, walikuta damu kwenye chumba alichokuwa amelala mzee huyo lakini hawakukuta mwili na walipofuatilia waliukuta mwili eneo ambalo kulikuwa kumewashwa moto, huku ukiwa umeunguzwa baadhi ya maeneo.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC kwa ajili ya taratibu za kiuchunguzi.