Mbaroni kwa tuhuma za kumuua mtoto wa kaka yake

Mbaroni kwa tuhuma za kumuua mtoto wa kaka yake

Muktasari:

  • Ni mkulima anayedai kuoteshwa na mungu wake aliyemuagiza amuue binti na kula maini yake ili apate mavuno mengi shambani msimu huu wa mavuno.

Mbulu. Mkazi wa Mtaa wa Silaloda Mji wa Mbulu mkoani Manyara, Harold Hhando anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mtoto wa kaka yake, Emmanuela Hhando (13) na kumtoa viungo vya mwili.

Inadaiwa Hhando alimuua mtoto huyo kwa kumpasua katikati ya miguu na kumtenganisha vipande viwili kisha kukata sehemu za siri, kumtoa maini na kutaka kuyapika ili ayale.

Akizungumza kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Marrison Mwakyoma amesema tukio hilo lilitokea jana kijijini hapo.

Kamanda Mwakyoma amesema chanzo cha tukio hilo ni ushirikina kwani Hhando ameeleza kuwa aliambiwa na mungu wake amuue mtoto wa kaka yake na kula maini ili avune mazao mengi.

Amesema Hhando ni mkulima wa eneo hilo la Silaloda hivyo imani za kishirikina zimesababisha akamuua mtoto huyo kwa kumpasua na kudai kuwa ameoteshwa kufanya hivyo.

“Mtuhumiwa anadai ameoteshwa na mungu wake na ana akili zake timamu hivyo alitarajia kula viungo hivyo ili aweze kupata mazao mengi zaidi shambani kwake,” amesema Kamanda Mwakyoma.

Ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuepuka imani za kishirikina zinazosababisha mauaji ya kikatili.

Mkazi wa Mtaa wa Silaloda, Johna Baynet amesema wananchi wa eneo hilo wamesikitishwa na kitendo hicho cha Hhando kumuua binti huyo mdogo.

“Hhando hakuwa na matukio mabaya ila tumeshangazwa na mauaji hayo ya kikatili aliyomfanyia mtoto wa kaka yake kwani hana rekodi za matukio ya uhalifu,” amesema Baynet.