Mbaroni kwa wizi wa mtoto kumdanganya mume amejifungua

Muktasari:
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Happiness William (18) mkazi wa kijiji cha Nyamaduke kwa madai ya kuiba mtoto wa miezi sita ili amuoneshe mumewake baada ya kumdanganya amejifungua.
Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Happiness William (18) mkazi wa kijiji cha Nyamaduke kwa madai ya kuiba mtoto wa miezi sita ili amuoneshe mumewake baada ya kumdanganya amejifungua.
Taarifa ya jeshi hilo kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa inasema mtoto huyo aliibwa Machi 26, 2023 baada ya mama yake kumuacha kwa dada yake aliyekuwa kambeba mgongoni.
“Huko mtaa wa Migombani, Kata ya Nyampulukano,Tarafa ya Sengerema, kuliripotiwa taarifa ya wizi wa mtoto mwenye umri wa miezi 6 na mtu ambaye hakujulikana. Ni kwamba, Mama wa mtoto huyo aitwaye Agnes Robert (26) alimuacha mtoto huyo kwa binti yake mdogo akiwa amembeba mgongoni kisha yeye kuingia bafuni kuoga,”
Taarifa hiyo inasema baada ya muda binti huyo akiwa amembeba mdogo wake mgongoni aliitwa na jirani yao aitwaye Costancia Deonatus na kumuagiza akiwa na watoto wenzake kufuata ndoo yake kwa mtu aliyekuwa amenunua mkaa kwake ambaye jina lake halikufahamika.
Mama wa mtoto huyo alipomaliza kuoga alitoka na kuanza kuwatafuta watoto wake na ilipofika Saa 7 mchana, watoto wawili walirejea nyumbani bila ya yule mwenzao wa miezi sita aliyekuwa amebebwa mgongoni na dada yake, ndipo wazazi kugundua mtoto wao ameibiwa na kutoa taarifa polisi.
“Baada ya tukio hilo kuripotiwa Askari Polisi walifanya msako mkali na kufika katika kijiji cha Nyamaduke na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa na mtoto huyo aliyetambuliwa na wazazi wake kuwa ndiye aliyeibiwa katika kijiji hicho,
“Baada ya mahojiano ya kina mtuhumiwa amekiri kuhusika na tukio la wizi wa mtoto huyo ambapo alidai kuwa alienda kumuonesha mumewe kuwa amejifungua. Upelelezi wa kesi hii unakamilishwa mara moja na mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani haraka iwezekanavyo kukabiliana na mkono wa sheria,”imesema taarifa hiyo