Mbossa aeleza sababu za Tanzania kutaka ushirikiano na DP World ya Dubai

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa

Muktasari:

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa amefafanua mambo yaliyozingatiwa kabla ya Serikali kusaini mkataba na Serikali ya Dubai kwa ajili ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii  katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari.


Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa amefafanua mambo yaliyozingatiwa kabla ya Serikali kusaini mkataba na Serikali ya Dubai kwa ajili ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari.

Mkataba huo uliosainiwa Oktoba 25 mwaka jana kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalumu ya kiuchumi, maegesho ya utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.

Kwa sasa uko mkataba huo uko katika hatua za majadiliano kabla ya Bunge la Tanzania kuuridhia.

Akijibu swali aliloulizwa kwenye mahojiano yaliyofanyika leo Juni 8, 2023 kupitia Kituo cha Matangazo Clouds TV 360, Mbossa amesema changamoto za ufanisi wa bandari, ushindani wa huduma za kibandari na uwezo, uzoefu na mtandao wa Kampuni ya Kimataifa ya huduma za bandari Dubai Port World (DPW)

“Kwanza niseme tumefanya mazungumzo na kampuni nyingi, tumesaini MoU (mkataba wa makubaliano) na Bandari ya Singapore, tuko hatua za awali na kampuni yao kubwa ya APM Terminals, kama kutakuwa na mwelekeo basi tutafanya nao kazi, pia Marekani na hao DP World wanaojulikana ndio yote yameibuka,”amesema.

Kuhusu DP World, Mbossa amesema kampuni hiyo ina uwezo wa kusaidia kuongeza ufanisi wa huduma za meli, shehena katika Bandari ya Dar es Salaam inayohudumia wastani wa meli 12 huku 20 zikisubiri kwa gharama zinazolipwa na wafanyabiashara wa mizigo, tofauti na ufanisi wa bandari ya Mombasa.

Mbossa pia amesema kampuni hiyo yenye mtandao wa huduma za kibandari ndani ya mataifa ya Afrika Mashariki itasaidia kuleta mageuzi katika ushindani wa huduma dhidi ya Bandari ya Mombasa.

“DP World ana bandari kavu kubwa sana Kigali ambako mzigo mkubwa unatoka DR Congo, Je ukimwacha akachukua bandari ya Kenya? na Kenya wametangaza na wenyewe wanaenda kwenye utaratibu kama wa kwetu kwa hiyo tutashirikiana baadhi ya vitu,” amesema Mbossa.

Amesema kampuni hiyo ikienda Mombasa itaathiri mnyororo wote wa shughuli za kiuchumi katika huduma za usafirishaji wa mizigo inayotoka Kigali na DR Congo.

“Jambo lingine tunazingatia mwenye uhusiano mzuri na kampuni za meli, uzoefu wa kutoa huduma nyingi Afrika.”