Mbowe alia mfumo mbovu wa upatikanaji wa viongozi nchini

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisalimiana na wakazi wa Kahama, wakati wa maandamano ya amani yaliyoambatana na mkutano wa hadhara jana. Picha na mtandao

Muktasari:

Amesema hayo jana katika  mkutano wa hadhara uliofanyika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, huku akidai  Katiba mpya na sera ya majimbo,  ndiyo suluhisho la kuibadili nchi.

Mwanza. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kinachochangia umasikini nchini,  ni namna viongozi wa Serikali wanavyopatikana.

Amesema Tanzania inahubiriwa kuwa ni masikini wakati imesheheni rasilimali lukuki zikiwamo za madini, ardhi yenye rutuba, misitu na wanyamapori.

Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga baada ya maandamano, Mbowe amesema Katiba mpya na sera ya majimbo ndiyo suluhisho la kuibadili nchi kutokana na mifumo aliyoiita mibovu ikiwemo ya utawala wa viongozi serikalini.

“Kama kuna chimbuko la kwanza la umasikini na uonevu katika nchi hii,  ni namna tunavyowapata viongozi wa Serikali. Sisi Chadema mapendekezo yetu kwenye mabadiliko ya katiba tunasema tufute vyeo vya wakuu wa wilaya, hawana kazi, tufute vyeo vya wakuu wa mikoa, hawana kazi, tuchague magavana wachaguliwe kwa kura za wananchi,” amesema Mbowe.

Amesema Tanzania ina viongozi wa aina mbili, wa kuchaguliwa na wananchi na wanaoteuliwa na Rais.

“Tunakwenda kwenye kampeni, Rais anaomba kura, wabunge wanaomba kura na madiwani wengine wanaomba kura,  lakini angalau wale wagombea wanakuja kwenu kuomba kura mkawachagua, mkimaliza kuchagua mnasikia taarifa ya habari Rais amemchagua fulani kuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga. Unajiuliza huyu aliyechaguliwa kuwa mkuu wa mkoa ameomba lini kuwa mkuu wa mkoa? mtu hamumjui, anakuja kusimamia maisha yenu, anasimamia rasilimali zenu mnamsikia kwenye taarifa ya habari, hii hapana,” amesema Mbowe.

Huku akitaja sera ya Chadema ni kuwa na serikali yenye majimbo manane, Mbowe amesema hata mataifa yanayojielewa kama yanataka ustawi wa watu, yanaweka mfumo wa kuchagua viongozi wao.

Amesema mfumo wa sasa ukichambuliwa kwa kina, anadai kuwa una upungufu mkubwa kwa madai kuwa wakuu wa wilaya na mikoa hawafanyi kazi kwa ajili ya wananchi,  bali kwa ajili ya mamlaka iliyowateua.

“Baada ya kuzungumza na wenzetu wa CCM tukawaambia, tunafikiri mahali ambapo nchi hii imekwama pa kuanzia kwanza ni Katiba inayoongoza nchi yetu. Kwenye vikao vya ndani wanasema ni kweli, lakini sisi hatutachoka kumwambia Mama Rais (Samia Suluhu Hassan) Lazima tuanze na Katiba..tukikaa vikao vya ndani wanakubali, wakienda vikao vyao wanasema tukibadilisha katiba tunakufa,” amedai mwenyekiti huyo.

Amesema safari ya kuibadilisha Tanzania si rahisi kama wengi wanavyofikiri.

“Tuliamini tunaweza kuzungumza kama Nyerere alivyozungumza tukapata uhuru. Tuna kazi ya kufanya, msikae vijiweni mnacheza pool table halafu mnategemea mabadiliko, lazima mteseke, lazima maisha yawatandike, tupate akili. Siku Watanzania mkipata akili CCM ni wepesi hawa..leo tutaandamana tunarudi nyumbani, kuna siku ya kura tutaandamana hatutotoka kituoni,” amesema.

Awageukia vijana

Akizungumzia suala la vijana, Mbowe amesema hatima ya nani aongoze kuanzia serikali za mitaa mwaka huu au Serikali kuu kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani,  ipo mikononi mwao akidai ndilo kundi kubwa lenye wapiga kura.

“Uchaguzi wa mwaka huu na wa mwakani utaamuliwa na ninyi vijana ambao hamtaki hata kuoa, mpo mpo tu akipita Mwajuma mnamuangalia mnasema Mwajuma bwana! Oa uone kama utamlisha kokoto.”

Awali akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi,  amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili wakazi wa mkoa huo,  ni kufidiwa fedha kidogo kulinganisha na thamani ya mashamba yao endapo yatabainika kuwa na madini ya dhahabu.

Kero nyingine aliyoiwasilisha kwa Mbowe ni madai ya wastaafu kuteswa na mafao, kikokotoo, wafanyabiashara kulalamikia kutozwa tozo kubwa hasa za huduma.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti Chadema, Gimbi Masaba,  amesema miongoni mwa changamoto inayowatesa wakazi wa Kahama ni miundombinu mibovu katika stendi ya mabasi pamoja na wajawazito kutozwa Sh10,000 ya kadi ya kliniki.

“Stendi kubwa ya mabasi miaka nenda rudi ina mlango mmoja, miundombinu ni mibovu wakati mabasi yanaingia na kutoka na yanatozwa ushuru, ‘’ amesema Masaba.