Mbowe: Na wao waache uhuni

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewajibu Halima Mdee na wenzake 18 kuhusu uamuzi uliofanywa usiku wa kuamkia leo na Baraza Kuu la chama hicho, waliouita wa ‘kihuni’, akiwataka na wao kuacha uhuni. 


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewajibu Halima Mdee na wenzake 18 kuhusu uamuzi uliofanywa usiku wa kuamkia leo na Baraza Kuu la chama hicho, waliouita wa ‘kihuni’, akiwataka na wao kuacha uhuni. 

Usiku wa kuamkia leo Alhamisi Mei 12, 2022 Baraza Kuu lenye wajumbe zaidi ya 400, lilitupilia mbali rufaa za wabunge wa viti maalumu 19, huku Mbowe akisema wamesikitika na hawakufurahi hali hiyo, lakini ilibidi. 

Badaa ya uamuzi huo, Mdee alisema; “huwa nakwepa kuzungumza maneno makali kwa sababu naheshimu viongozi wangu, lakini sikujua kama Chadema kunaweza kufanyika uhuni kwa kiwango hiko.Nitaendelea kuwa Chadema vizuri tu, lakini kichofanyika pale ni uhuni wa kiwango cha hatarii hata Mbowe mwenyewe anajua,” amesema Mdee.

Hata hivyo, Mbowe akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kumalizika kikao hicho, amesema Baraza Kuu limekaa na wao walikuwa mashuhuda kwa kila hatua.

“Wajumbe wamekuja leo na wamefanya uamuzi wakishuhudia na kura zimepigwa mbele yao waache mambo ya ‘kihuni,” amesema Mbowe.

Baraza Kuu liliketi jana Jumatano Mei 11, 2022, likiwa na ajenda saba ikiwemo ya kusikiliza na kutoa uamuzi wa rufaa za wabunge 19 wakiongozwa na Halima Mdee, Grace Tendega, Ester Bulaya

Agnesta Lambert, Jesca Kishoa, Ester Matiko, Salome Makamba na Nusrat Hanje.

Wamo Tunza Malapo, Conchestar Rwamlaza, Naghenjwa Kaboyoka, Hawa Mwaifunga, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Asia Mohammed, Sophia Mwakagenda, Cecilia Pareso, Kunti Majala na Felister Njau.

Wote hao wamevuliwa nyadhifa za uongozi na uanachama mwaka 2020 baada ya kubainika kwenda kinyume na msimamo wa Chadema kula kiapo cha kuwa wabunge wa viti maalumu bila baraka za Chadema. 

Hata hivyo, licha ya kufukuzwa uanachama, walikata  rufaa katika baraza kuu la chama hicho lenye wajumbe zaidi ya 437 linaloketi jana na usiku wa kuamkia leo lilitoa uamuzi wa kutupilia mbali rufaa za Mdee na wenzake 18 kwa kupiga kura ya wazi.

Katika upigaji wa kura jumla ya wajumbe 423 walishiriki, kati yao 413  sawa na asilimia 97.6 walikubaliana na uamuzi wa kamati ya kuu ya Chadema ya kuwavua uanachama, wakati watano sawa na asilimia 1.2 hawakukubalina na uamuzi wa kuwafukuza huku wasiofungamana na upande wowote wakiwa watano sawa na asiliamia 1.2.