Mbu wa kutengeneza kuachiwa visiwa vya Keya nchini Marekani

Muktasari:
- Wakazi wa Florida wameingiwa na hasira wakati wanasayansi wakijiandaa kuachia mamilioni ya mbu wa ambao wamefanyiwa marekebisho ya jini, kuanza maisha katika maeneo yao, gazeti la The Telegraph limeandika.
Wakazi wa Florida wameingiwa na hasira wakati wanasayansi wakijiandaa kuachia mamilioni ya mbu wa ambao wamefanyiwa marekebisho ya jini, kuanza maisha katika maeneo yao, gazeti la The Telegraph limeandika.
Jaribio l utafiti, linaloongozwa na kampuni ya Oxitec, litahusisha takriban mbu milioni 750 watakaoachiwa kuishi katika visiwa vya Keys kwa kipindi cha miaka miwili ijayo katika jitihada za kudhibiti idadi ya aina mpya ya viumbe wavamizi wanaobeba magonjwa na ambao wamepiga kambi maeneo hayo.
Lakini wakazi wengi hawajafurahishwa kuwa sehemu ya kile walichokiita “jaribio la Jurassic Park (wakirejea filamu ya mwaka 1993 iliyoongozwa na Steven Spielberg na kutayarishwa na Kathleen Kennedy na Gerald R. Molen ambayo inazungumzia jaribio la kuunda viumbe ambao baadaye walisababisha matatizo katika kisiwa cha Isla Nublar)”.
Wimbi la kwanza katika mradi huo litahusisha maelfu ya mbu watakaoachiwa katika maeneo sita wiki hii, huku mbu 144,000 wakitarajiwa kuachiwa huru katika wiki 12 za mwanzo.
Mradi huo umeanzishwa kukabiliana na mbu aina ya Aedes aegypti, ambao ni asilimia nne ya mbu wote walio visiwa vya Keys lakini wanaaminika kuwa wanasambaza kwa binadamu magonjwa ya dengue, Zika na homa ya manjano.
Pia wanaweza kusambaza magonjwa kama heartworm ambao husababisha matatizo katika mapafu, hasa kwa wanyama na mengine hatari kwa maisha.
Ni mbu wa kike tu ambao humuuma binadamu na kumuambukiza ugonjwa, kwa sababu wanahitaji damu kwa ajili kutaga mayai. Taasisi ya Oxitec imefanyia marekebisho jini za mbu wa kiume ili wawe na protini ambayo itaua watoto wa kike wa mbu kabla ya kufikia umri wa kumng'ata binadamu.
Mbu wa kiume, ambao wanategemea nekta kama chakula chao, hawatakufa na watarithisha jini hizo kwa vizazi vingine.
Matarajio ni kwamba mbu wa kiume waliofanyiwa marekebisho watawapanda mbu wa kike waliopo, na hivyo kupunguza taratibu idadi ya mbu aina ya Aedes aegypti.