Mbunge aombwa kusaidia kukomesha vijana ‘Manyigu’ Mpanda
Muktasari:
- Kikundi cha mchezo wa ngumi Mpanda (Ushu) chaomba Mbunge kuwezeshwa vifaa vya mazoezi kupunguza vijana wahalifu maarufu kama ‘damu chafu’ au ‘Manyigu mtaani’
Katavi. Kikundi cha mchezo wa ngumi wilayani Mpanda (Ushu) kimemuomba Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi kukiwezesha vifaa vya kufanyia mazoezi ili kusaidia kupunguza vijana wanaofanya vitendo vya uhalifu maarufu kama ‘damu chafu’ au ‘Manyigu’.
Mwanzilishi wa kikundi hicho ambaye pia ni mkufunzi wa mafunzo ya ngumi kwa vijana 30 sasa Moud Abibu (44) amesema kilianzishwa 1999 ili kuendeleza mchezo huo kimkoa.
“Nimetoa kero yangu kwa Mbunge Kapufi (Serbastian) atununulie vifaa vya mchezo huu, hii itasaidia kupunguza wimbi la vijana wasiojitambua mtaani wanaofanya uhalifu,”amesema Abibu.
Twaha Lubenga aliyepo mafunzoni ambaye pia ni mjasiriamali amesema mafunzo hayo yanasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kukomesha uhalifu kwa vijana mtaani.
“Pia inapunguza migogoro ya ndoa unarudi mwili upo vizuri usingizi mnono, kelele ndani ya nyumba hakuna familia zinafahamu,”amesema Lubenga.
Mbunge wa Mpanda Mjini Sebastian Kapufi akiwa kwenye mkutano wa hadhara kusikiliza kero na kuzitafutia ufumbuzi kata ya Nsemlwa ameahidi kutoa msaada wa vifaa hivyo.
Amesema kundi la vijana ni nguvu kazi ya Taifa hivyo wanapoimarishwa kimwili na kimaadili inawapa mbinu za kuepukana na vitendo viovu.
“Rai yangu kwa wazazi na walezi imarisheni malezi kwa watoto ili tudhibiti kundi la vijana wanaohatarisha maisha ya watu mtaani,”amesema Kapufi.