Miaka 20 panyarodi bado ni walewale

Mkazi wa Kunduchi Mji Mpya, Grace Michael akionyesha majeraha aliyoyapata baada ya kushambuliwa kwa mapanga na panya road waliovamia mtaani kwao, jijini Dar es Salaam,  juzi. Picha na Loveness Bernald

What you need to know:

  • Ni jioni yapata saa 1:00 jioni, wakazi wa Tabata wanakimbia huku na huko kwa hofu ya kushambuliwa na kuporwa na vijana wadogo wanaosemekana wana visu na mapanga.

Ni jioni yapata saa 1:00 jioni, wakazi wa Tabata wanakimbia huku na huko kwa hofu ya kushambuliwa na kuporwa na vijana wadogo wanaosemekana wana visu na mapanga.

Baadhi ya watu wanakodisha bodaboda kwenda mbele zaidi ya walipo. Kadri muda unavyokwenda ndivyo utulivu unavyorejea.

Kadri utulivu unavyoongezeka watuwanajitokeza na kuulizana maswali mengi kuhusu tukio hilo. Hakuna majibu yenye kutoa picha halisi ya wahusika wa uporaji huo kwa kuwa wengi walikimbia na kujificha mbali na wahalifu hao.

Ndivyo zilivyo picha za maeneo mengi ambayo huvamiwa na panyarodi. Wahalifu vijana hao huibuka sehemu zenye mikusanyiko mikubwa na kutumia nguvu kupora wapita njia na wale wanaoonyesha kupambana nao japo kidogo, hujikuta wakikatwa na mapanga, kuchomwa visu au kupigwa na magongo na hivyo kusalimisha mali zao.

Matukio hayo huchukua muda mfupi na ni nadra sana-- kama si kutokuwepo kabisa-- polisi kuyawahi matukio hayo ya uporaji na kukamata wahusika. Haijulikani vijana hao hutokea wapi na huweza kutoweka eneo la tukio kwa namna ipi.

Yapo magenge mengine ya panyarodi ambayo huvamia mitaa usiku wa maanani. Haya pia hayachukui muda mrefu kufanya uhalifu na huvamia nyumba zaidi ya moja kupora fedha na vitu vidogo vya thamani kama simu na televisheni. Kujaribu kupambana na vijana wa magenge hayo, ni hatari kwa kuwa akinyoosha panga juu halirudi, ndivyo wengi waliovamiwa wanavyosimulia.

Kila baada ya taharuki inayotokana na vitendo vya panyarodi, polisi huibuka na taarifa nyingi za mikakati ya kudhibiti vitendo hivyo na takwimu za vijana waliokamatwa kwa tuhuma za kuhusika katika uhalifu huo.

Kila wakati makundi hayo yanapoibuka, Jeshi la Polisi hueleza sababu tofauti za chanzo cha panyarodi; kuanzia ngoma maarufu za Kangamoja, Baikoko na Kigodoro zinazofanyika usiku kuwa chanzo cha uhalifu huo; jamii kutowaripoti vijana waovu; wazazi na walezi kutotekeleza majukumu yao ipasavyo; hadi wahalifu wanaopata msamaha magerezani kuwa ndio wahusika wakuu.

Lakini wakati mwingine taarifa za polisi hugubikwa na utata. Mwaka 2015, Jeshi la Polisi mkoani Dar es Salaam lilitangaza kukamata vijana 510 kwa tuhuma za kuhusika katika uporaji unaofanywa na panyarodi. Kamanda wa polisi wa Dar es Salaam wa wakati huo, Suleiman Kova aliwaonyesha waandishi wa habari picha ya baadhi ya vijana waliokamatwa, akiwemo Justine Mwacha. Lakini kijana huyo aliibuka siku iliyofuata na kukanusha kwamba amekamatwa, akisema anaendelea na kazi yake ya kuosha magari pembeni ya kituo cha polisi cha Chang’ombe.

Kuhusu picha hiyo, Mwacha alieleza kuwa ilichukuliwa kituoni hapo asubuhi ya siku ambayo walikamatwa usiku wakati wakinywa pombe baa ya Sugar Ray, Temeke. Huo ndio ukawa mwanzo wa mwisho wa sakata hilo.

Matukio ya hivi karibuni yaliyokuzwa na kuuawa kwa mwanafunzi wa uandishi wa habari wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Maria Basso, ni mwendelezo wa kuibuka na kutoweka kwa taharuki ya magenge ya panyarodi jijini.

Lakini hali sasa inaonekana kuwa mbaya zaidi. Taarifa ya mwisho ya Jeshi la Polisi inaonyesha magenge hayo sasa yanatumia zana nzuri zaidi kama magari kufanikisha uhalifu wao, tofauti na awali yalipopachikwa jina la panyarodi kurejea njia zisizo rasmi zinazotumiwa kuvuka mipaka ya nchi kukwepa mamlaka. Au kupitisha bidhaa kwa njia isiyo rasmi kwa lengo la kukwepa ushuru na tozo nyingine.

Kwa kuwa kundi hilo limekuwa likipita mitahani kuzua taharuki na kupora wapitanjia na wenyeji, au kuibuka majumbani usiku wa maanani na kufanya unyang’anyi kwa kutumia zana za asili, lilipachikwa jina la panyarodi.

Lakini taarifa ya Kamanda Muliro inaonyesha magenge hayo sasa yanaweza kukaa chini, kupanga uhalifu na kusafiri umbali mrefu kwa kutumia magari na kupita barabarani kwenda kutekeleza mipango yao miovu.

Watuhumiwa sita waliouawa wiki iliyopita, walikuwa wanatumia gari kutoka Mabibo wilayani Ubungo kwenda Goba Kinzudi-- umbali wa takriban kilomita 11, kufanya uhalifu huo. Walipofika Makongo, walizuiwa na gari la polisi, ndipo waliposhuka na mapanga na kutishia kuwashambulia askari.

“Na katika mazingira hayo, askari walijihami kwa kufyatua risasi kadhaa hewani lakini wahalifu hao waliendelea kukaidi na kutaka kuwajeruhi polisi. Ndipo walishambuliwa, kujeruhiwa na baadaye walipelekwa haraka hospitali lakini walipoteza maisha,” alisema Kamanda Muliro, akisisitiza kuwa hata kama hawakuwa na silaha za moto, walitakiwa kujisalimisha kwa polisi.

Muliro pia alihusisha watuhumiwa hao na mauaji ya Maria Basso, kwa mujibu wa taarifa zao za kiintelijinsia, ingawa hakutaka kueleza kwa mapana ilivyokuwa.

Hakuna shaka, kwa kuangalia mwenendo wa matukio mengine yaliyopita, panyarodi watapoa tena kwa muda kusubiri wakati sahihi wa kuibuka upya, huku hekaheka za kuwasaka zikitulia tena kusubiri kuibuka upya.

Hata hivyo, zaidi ya miaka 17 tangu tukio lile la Tabata, taarifa za kuibuka na kutoweka kwa panyarodi pamoja na operesheni za muda mfupi za kukabiliana nao zimekuwa zilezile. Hii inaonyesha hakujawa na mkakati madhubuti wa kuondoa kabisa panyarodi na kwa ujumla uhalifu dhidi ya wananchi.

Bado panyarodi hawajulikani ni watu gani hasa, huibukia wapi, na kutowekea wapi na hupangaje mipango yao miovu. Sababu zinazotolewa na Jeshi la Polisi kuhusu kuibuka kwao hazitoshi kuwa ndio majawabu ya tatizo hilo.

Taarifa za kuwashambulia na kuwakamata panyarodi hazijaweza kuwaondoa. Pengine vyombo vya habari havijafuatilia kesi zao hadi mwisho, au Jeshi la Polisi halijafanya jitihada za kuhakikisha kesi hizo zinaripotiwa hadi mwisho ili wahusika waone kuna dhamira ya dhati ya kupambana nao.

Na pengine kukamatwa kwa watuhumiwa hakuambatani na ushahidi wa kutosha wa kuwatia hatiani mahakamani na hivyo kesi zao kuishia hewani.

panyarodi wanabakia kuwa panyarodi na wanaweza kuibuka wakati wowote wautakao kwa kuwa hawajatambulika bado.

Kuliondoa tatizo hakuwezi kufanikiwa kutokana Jeshi la Polisi kufanya kazi kulingana na matukio, bali kufanya uchunguzi wa kimkakati kujua namna panyarodi wanavyojipanga hadi kutekeleza uhalifu wao. Vitengo vya uchunguzi vya polisi ndivyo vinapaswa kuwajibika zaidi katika janga hili.

Mbali na dhamana hiyo kwa Jeshi la Polisi, Rais Samia Suluhu Hassan anaona jukumu liende mbali zaidi.

“Dunia iko mbele, wazazi tuko nyuma. Kwa hiyo niombe sana, panyarodi tunaowazungumza leo ni watoto wetu, tumewazaa majumbani kwetu, wana dini zao lakini hawakukuzwa kwa misingi ya kidini,” alisema Rais hivi karibuni.

Pamoja na ukweli huo, Jeshi la Polisi limepewa kazi kubwa ya kulinda wananchi na mali zao na hivyo halina budi kuwa mstari wa mbele kusaka dawa sahihi ya kuondoa upanyarodi.