Migodi mipya minne kuanzishwa nchini

Dar es Salaam. Wizara ya Madini imesema kuna uwezekano wa kuongeza migodi mipya minne hadi kufikia mwaka 2030, inayotarajiwa kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi nchini.

Mpango huo ulielezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali kwa washiriki wa mkutano wa uwekezaji wa The London uliofanyika Uingereza wiki iliyopita.

"Azimio letu pia linahusu kuanzisha angalau migodi minne mipya ifikapo mwaka 2030 kwa kuvutia wahusika wakuu kama vile Rio Tinto, BHP, Vale, Glencore, Anglo-American, na Zijin na kulenga kuiweka Tanzania kama kitovu muhimu cha madini," alisema Mahimbali.

Oktoba 2023, Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kuzindua mitambo ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico), alisema sekta hiyo iliyochangia asilimia 7.2 kwenye pato la Taifa, mwaka 2020/21 iko katika mwelekeo mzuri katika kujenga uchumi.

Alipoulizwa na washiriki wakati wa Mkutano wa ‘The London’ kuhusu kinachomkosesha usingizi katika wizara hiyo, Mahimbali alisema ni harakati za kupata vyeti vya Taasisi ya Viwango Duniani (ISO) kwa Shirika la Madini la Taifa (Stamico), Tume ya Madini na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST).

“Ni maono yetu kuinua Stamico kupitia ushirikiano wa kimkakati na sekta binafsi unaovuka mipaka ya Tanzania. Safari hii inahusisha kuunda ushirikiano na viongozi wa sekta kama vile S&P Global na Taasisi ya Fraser, kushiriki kikamilifu katika matukio muhimu kama vile Chatham House London Conference, Africa Down Under, Investing in Africa Mining Indaba, na FT Mining Summit,” alisema.

Mbali na mkutano huo, Mahimbali na ujumbe wake pia walikutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Helium One inayojihusisha na uchimbaji wa masuala ya nishati, Lorna Blaisse.

"Pamoja na timu yangu, tulipokea wasilisho zuri kuhusu kazi inayofanywa na kampuni yake (Helium one) katika kuendeleza sekta ya gesi ya helium. Tuliwapongeza na kuwahakikishia kuendelea kuwaunga mkono katika juhudi zao,” alisema Mahimbali.