Miili 13 ajali iliyoua 18 Nzega yatambuliwa na kuchukuliwa

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian (aliyejifunga ushungi) akimjulia hali mmoja wa majeruhi wa ajali ya basi la Alfa kuogongana uso kwa uso na lori la mafuta. Watu 18 walifariki katika ajali hiyo huku wengine 60 wakijeruhiwa.

Muktasari:

Miili 13 ya watu waliofariki katika ajali ya basi kugongana uso kwa uso na lori la mafuta imetambuliwa na kuchukuliwa huku miili ya watu watano ikiwa haijatambuliwa.

Tabora. Miili 13 ya watu waliofariki katika ajali ya basi kugongana uso kwa uso na lori la mafuta imetambuliwa na kuchukuliwa huku miili ya watu watano ikiwa haijatambuliwa.

Kutokana na miili hiyo kutotambuliwa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian ametoa wito kwa watu ambao hawajawaona ndugu zao kujitokeza kutabua miili ya watu watano inayoendelea kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Nzega.

Dk Burian ametoa wito huo leo Oktoba 25, 2023 alipowatembelea na kuwajulia hali baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo iliyotokea Octoba 21, 2023 katika eneo la Undomo Uchama wilayani Nzega.

"Wale ambao hawajawaona au hawafahamu walipo ndugu zao wafike chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Nzega kutambua miili ya watu watano ambao hawajatambuliwa hadi sasa,’’ amesema Dk Burian

Ajali hiyo ilitokea Octoba 21, 2023 baada ya basi la Alfa lilikuwa linatoka jijini Mwanza kwenda jijini Dar es Salaam kugongana uso kwa uso na lori la mafuta eneo la Undomo Wilaya ya Nzega.

Watu 18 walifariki huku wengine 60 wakijeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea kati ya Saa 5: 30 na Saa 6:00 asubuhi.