Prime
Mikopo kwa dhamana ya mafao yaibua maswali, waziri afafanua
Muktasari:
- Mikopo hiyo itakuwa mahsusi kwa ajili ya mambo matatu ya kujenga nyumba ya kuishi isiyohamishika, kununua nyumba ya kuishi au kufanya marekebisho au ukarabati nyumba ya kuishi.
Moshi. Serikali imetunga kanuni mpya za mifuko ya Hifadhi ya Jamii zitakazomwezesha mwanachama kutumia mapema sehemu ya mafao anayostahili, kama dhamana ya kukopa kwenye taasisi za fedha zikiwemo benki kwa ajili ya ujenzi au uboreshaji wa makazi.
Hata hivyo, kanuni hizo zilizotangazwa kupitia Gazeti la Serikali (GN) namba 141 iliyotolewa Machi 8, 2024 zimeweka masharti ya aina ya mikopo, ambayo mwanachama ataruhusiwa kukopa kwa dhamana ya michango yake kwenye mifuko hiyo, huku zikiibua maswali ya wanachama.
Mikopo hiyo itakuwa ni mahsusi tu kwa ajili ya mambo matatu – kujenga nyumba ya kuishi isiyohamishika, kununua nyumba ya kuishi au kufanya marekebisho au ukarabati nyumba ya kuishi.
Hata hivyo, uamuzi huo wa Serikali umepokelewa kwa hisia tofauti na wanasheria na wanachama wa mifuko hiyo, baadhi wakiona kama ni janja ya Serikali kuzima fukuto la wanachama nchi nzima kupinga kikokotoo cha asilimia 33.
Kumekuwepo na vuguvugu la kupinga kikokotoo hadi mafao cha asilimia 33 kulipwa kwa mkupuo na asilimia 67 kulipwa kidogokidogo kama pensheni, kilichowekwa kwa mifuko yote miwili, wa umma (PSSSF) na ume wa Binafsi (NSSF).
Awali baadhi ya watumishi kwenye sekya za umma walikuwa wanalipa asilimia 50 kwa 50 huku wale wa NSSF wakilipwa asilimia 25 mkupuo na asilimia 75 nyingine pensheni.
Pamoja na kuanza kwa kanuni mpya, kelele bado zimeendelea kupingwa na baadhi ya viongozi wakiwemo wabunge, vyama vya siasa, viongozi wa vyama vya wafanyakazi, polisi na wanaharakati wakitaka malipo ya mkupuo yawe asilimia 50.
Kanuni mpya ya dhamana
Wakati hali ikiwa hivyo, tangazo la Serikali Na. 141 lililotangazwa na kusainiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako, limetoa ruksa kwa mwanachama kutumia mafao yake kama dhamana ya mkopo.
Hata hivyo, kifungu cha 3(1) cha kanuni hiyo, kinasema dhamana ya mkopo itakayoruhusiwa na mifuko kwa taasisi za fedha kwa niaba ya mwanachama, itakuwa ni kwa ajili ya kujenga nyumba ya kuishi, kununua nyumba au kuiboresha nyumba ya mwanachama.
Kwa mujibu wa kifungu cha 3(2) cha kanuni hizo, mifuko haitatoa dhamana zaidi ya moja kwa wakati mmoja na kifungu cha 3(3) kinasema dhamana hiyo itatolewa baada ya mwanachama mwenyewe kuomba kwenye mfuko.
Kifungu cha 4(1) (a) kinasema kiwango cha dhamana kwa ajili ya nyumba ya makazi kilichopo kwa mwanachama hakitazidi asilimia 50 ya mafao anayostahili kulipwa mwanachama, wakati anapowasilisha maombi yake kwa mfuko husika.
Pia kifungu cha 4(1) (b) kimeweka sharti kuwa bei ya kununulia nyumba haitapaswa kuzidi thamani ya soko la nyumba inayohusika kwa wakati husika.
Kulingana na kifungu cha 5, mwanachama anayestahili kupata dhamana hiyo ni lazima awe ni Mtanzania, mwanachama anayestahili na muda wa uhai wa dhamana hautazidi muda wa kisheria wa mwanachama kustaafu kwa lazima.
Mbali na vifungu hivyo, kifungu cha 7 (1) kinataka taasisi ya fedha inayotaka kutoa mkopo hiyo, iwasilishe ombi hilo kwa maandishi na ndani ya siku 30, mfuko utatoa idhinisho la maandishi na endapo utakataa utatoa sababu kwa maandishi.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Cyprian Luhemeja alipozungumza na Mwananchi kuhusu kanuni hizo, alisema ni kweli kanuni zipo na zimeanza kutumika Machi 8, 2024.
Uamuzi umechelewa
Kiongozi wa Chama cha wanasheria wa tanganyika (TLS) Kanda ya Kaskazini, David Shillatu alisema kimsingi uamuzi huu unakuja ukiwa umechelewa kwa kuwa fedha kwenye mifuko ya hifadhi ya Jamii ni za wanachama na si za Serikali.
“Kimsingi mwanachama anapaswa kunufaika na pesa hizi akiwa na nguvu zake akijiandaa na maisha ya kustaafu. Kuna wengine hata wanakufa wala hawajawahi kufaidi hili jasho lao. Tunashukuru kwa maamuzi haya ya busara,” alisema Shillatu.
“Labda mimi nihoji tu, kwa nini hiyo GN imeweka ukomo wa asilimia 50 badala ya kuruhusu wafanyakazi wajitwalie asilimia zote 100?” alihoji Shillatu ambaye ni wakili.
Mwanasheria mwingine, Elia Kiwia alisema hasara ya kanuni hiyo kwa mwanachama ni kwamba akichukua mkopo analipa riba, hivyo kiasi alichokopa atalipa zaidi na ametahadharisha wanachama kusoma vyema masharti ya riba.
“Lakini kuna faida, mtumishi ataweza kukopa na kufanya shughuli yake ya kimaendeo mapema kabla ya kustaafu, hivyo kutatua na kukuza uchumi wake mapema akiwa na nguvu bila usumbufu wa marejesho ya kila siku,” alisema.
Pia, Wakili Aloyce Komba alisema kanuni hizo mpya zina faida zaidi kwa kuwa mfanyakazi kwa kuwa anatumia akiba yake kujijengea maisha na hivyo "ni mpango mzuri sana."
Wanachama nao wafunguka
Kwa upande wake Mwalimu Stephen Mnguto, mwanachama wa mifuko hiyo, alisema uamuzi huo ni jambo jema ila anaona kama Serikali imeleta kanuni hiyo kufunika kilio cha kikokotoo.
“Ni jambo jema ila binafsi naona ni kama kujikosha kwa Serikali kwa kutafuta kichaka cha kujificha baada ya kelele nyingi za kikokotoo ambacho kinawaumiza wafanyakazi,”alisema Mnguto ambaye ni Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) katika moja ya wilaya jijini Dar es Salaam.
“Suala si kumsaidia mtu kukarabati nyumba au kujenga, suala ni kurudisha kikokotoo cha zamani ili mnufaika aamue mwenyewe namna ya kutumia fedha zake, sio kupangiwa namna ya kuzitumia,”alisisitiza Mnguto.
Hata Wilfred Mauki, mwanachama mwingine, alisema kanuni hiyo haiwezi kuwa msaada na faida kwa watumishi kwa kuwa mkopo huo una riba na bado watumishi wanapata malipo ya mkupuo ya asilimia 33 ya mafao, pale anapostaafu.
“Hili tu la asilimia 33 limekuwa kilio kwa watumishi wengi. Hili la mkopo sioni kama ni nia njema, muhimu Serikali iwawezeshe watumishi wake mikopo yenye riba nafuu wakiwa katika ajira zao na wenye nguvu na uwezo wa kulipa,” alisema.
“Huu mkopo wa mifuko ya hifadhi ya jamii ni hatari kwa wastaafu, upo mstari mwembamba sana kati ya uhai na kifo kwa mkopo huu. Ni kupunguza Life span (muda wa kuishi) ya wastaafu, wawe wa umma au binafsi,” alisisitiza.
Akitoa ufafanuzi wa hoja hizo, Waziri Ndalichako alisema kanuni hizo zimetengenezwa kwa lengo la kuongeza wigo wa mafao ili kuleta manufaa kwa wanachama wa mifuko hiyo.
Alisema kilichofanyika ni matokeo ya maombi ya wanachama waliohitaji mikopo hiyo, kwa kuwa wanashindwa kumudu riba zinazotolewa na taasisi za fedha.
“Tumekuja na hili kwa sababu yamekuwepo maombi ya wanachama na tumezingatia suala la riba ambayo itakuwa nafuu, ikilinganishwa na mikopo mingine. Halafu mikopo hii ni hiari si kila mtu analazimishwa kuchukua, wapo waliohitaji wataichangamkia.
“Lengo ni kuboresha mafao, haina uhusiano na kikotoo na sijui kwa nini wamewaza hivyo, kwa kuwa maboresho haya tumeyafanya pia hata kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) tumeweka fao la mafunzo kwa mfanyakazi, ambaye amepata ajali na kupoteza kiungo chake lakini bado anaweza kufanya kitu kwa viungo vilivyosalia,” alisema Profesa Ndalichako.